Mji wa Zhongxiang ulioko katikati ya mkoa wa Hubei una ardhi yenye rutuba na unazalisha mazao mbalimbali ya kilimo. toka zamani hadi leo, wakulima wa huko wanafurahia na kuridhika na maisha yao kwenye ardhi hiyo. Lakini katika miaka ya hivi karibuni, mabadiliko yasiyotarajiwa yametokea kwamba wakulima wengi zaidi wanaenda Japan kujifunza ufundi wa kilimo, na kurudi nyumbani na teknolojia za kisasa na uzoefu wa usimamizi walizojifunza, ili kuvumbua mustakabali mpya kwa ardhi hiyo.
Kijiji cha Suiwan cha mji wa Zhongxiang ni moja ya maeneo sita ya ufugaji wa nguruwe yaliyothibitishwa na idara ya usimamizi wa shughuli za ufugaji ya huko, hivi sasa familia zaidi ya 100 zinashugulikia shughuli hizo katika kijiji hicho. Hali hiyo inatokana na uongozi wa mwanakijiji Bw. He Jiaguo, na mafanikio yake yanatokana na ujuzi aliopata katika mafunzo ya kilimo nchini Japan. Bw. He Jiaguo akiwa ni mkulima wa kwanza wa mji huo aliyeenda kusoma nchini Japan, alisema:
"nilishangaa sana niliposikia kuwa China ilikuwa inatuma wakulima kushiriki kwenye mafunzo ya kilimo nchini Japan, nikiwa ni mkulima, katika maisha yangu kamwe sikufikiri kuwa naweza kwenda nchi ya nje kujifunza."
Bw. He Jiaguo alienda Japan mwaka 1998 kujifunza teknolojia ya upandaji wa matikiti na strobeli kwenye wilaya ya Ibaraki-ken nchini humo. Katika muda wa mwaka mmoja alipokuwa anasoma nchini Japan, si kama tu alijifunza teknolojia ya upandaji wa wa matikiti na strobeli na kufahamu kuhusu kilimo cha kisasa cha nchi hiyo, bali pia aliweza kuona michango muhimu iliyotolewa na jumuia ya ushirikiano wa kilimo ya Japan, ambayo ilianzishwa na wakulima wenyewe wa nchi hiyo, katika kazi za kilimo za wakulima na shughuli za kuongeza mapato na kubana matumizi ya raslimali katika kazi hizo.
Jumuia hiyo ya ushirikiano inalenga kutoa huduma mbalimbali kwa wakulima, zikiwemo kutoa raslimali za kazi, huduma za fedha, bima na uelekezaji wa usimamizi. Bila kujali wasiwasi wao, wakulima wanatakiwa tu kufanya kazi kwa bidii mashambani.
Uzoefu huo ulimpa wazo Bw. He Jiaguo kuwa la anaweza kuhamisha na kutumia utaratibu wa jumuia hiyo katika maskani yake au la.
Baada ya kurudi mjini Zhongxiang, Bw. He Jiaguo alishirikisha familia zinazofuga nguruwe kijijini na kuanzisha shirikisho la ufugaji na kusaini makubaliano na kila familia kuwa wanatakiwa kulipa Yuan mia mbili kama fedha ya dhamana, na kufuata kanuni na usimamizi wa shirikisho hilo, na shirikisho hilo litawanunulia kwa jumla chakula cha mifugo na kutoa mafunzo kila baada ya muda kuhusu teknolojia ya ufugaji.
Hivi sasa idadi ya wanachama wa shirikisho hilo imeongezeka hadi kufikia zaidi ya familia 200 kutoka familia 7 mwanzoni. Manufaa yaliyoletwa na shirikisho hilo kwa wafugaji yanaonekana moja kwa moja. Hivi sasa wastani wa pato la mwanachama kwa mwaka umezidi Yuan elfu 25.
Kwenye kijiji cha Jindian mjini Zhongxiang, mkulima mwengine anayeitwa Bw. Zhang Guangming pia alienda kupewa mafunzo nchini Japan. Mwaka 2005 alipofika Japan kwa muda mfupi tu kila kitu nchini humo kilikuwa kinamvutia sana, hasa teknolojia za kisasa na mashine mbalimbali za kilimo zinazotumika nchini humo. Baada ya kusoma kwa mwaka mmoja, Bw. Zhang Guangming alikuwa na mpango wa kuanzisha shughuli zake baada ya kurudi maskani yake. Mkewe Bi. Shu Xiaohong alipozungumzia jambo hilo, alifurahi sana akisema:
"naona alikuwa na mabadiliko makubwa baada ya kujifunza kwa mwaka mmoja nchini Japan, alijifunza teknolojia za kisasa za huko, ambazo zimesaidia kuongeza pato la familia yetu, pia tumenunua mashine mbalimbali za kilimo. Nadhani nilistahili kujifunza kwa mwaka mmoja nchini Japan."
Imefahamika kuwa, kabla ya wakulima kufunga safari kwenda Japan, wanapewa mafunzo ya lugha ya kijapani kwa miezi mitatu. Kwenye kituo cha mafunzo cha shirikisho la ushirikiano wa kilimo cha mji huo, mwandishi wetu wa habari pia aliwakuta wanafunzi 10 hivi wanawake waliotaka kujifunza teknolojia ya ufugaji wa ng'ombe nchini Japan. Mojawapo ni Bi. Wang Ping, alisema:
"nataka kwenda Japan kwa malengo mwili, ya kwanza ni kuboresha mazingira ya familia yangu, ya pili ni kujifunza teknolojia ya kisasa ya kilimo."
Bi. Wang Ping alisema, zamani kwa wanawake wa vijijini kama yeye hawakufikiri kwenda nchi za nje. Lakini hivi sasa amepata fursa ya kutembelea nchi za nje na kujionea dunia ya nje. Hivi sasa mji wa Zhongxiang yametuma makundi 79 yenye wakulima zaidi ya 1,100 kwenda Japan kujifunza teknolojia za upandaji na ufugaji. Meya wa mji huo Bw. Tian Wenbin alisema:
"shughuli hiyo imeongeza pato la wakulima wa mji huo, muhimu zaidi ni kwamba wamejifunza teknolojia za kisasa, uzoefu wa usimamizi na mtizamo wa uendeshaji wa Japan, shughuli hiyo si kama tu imehimiza mawasiliano ya kiuchumi, kiutamaduni na kihisia kati ya watu wa China na Japan, bali pia imetatua kwa kiasi upungufu wa nguvukazi nchini Japan, na imetimiza hali ya kunufaishana."
|