Mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya Ndani wa China una eneo kubwa, na hali duni ya mawasiliano ya barabara iliwahi kutatatiza sana maisha ya wakulima na wafugaji wa mkoa huo, lakini sasa hali imebadilika. Leo tunawaletea maelezo kuhusu barabara za kuleta neema mkoni humo.
Wapendwa wasikilizaji, mliousikia ni wimbo wa wafugaji wa Mongolia ya Ndani unaohusu msichana mmoja atakayeolewa kwenye sehemu ya mbali. Kutokana na barabara mbovu na umbali wa maelfu ya kilomita, je ataweza kurudi tena na kuwaona wazazi wake? alikuwa na huzuni kubwa hata akatokwa na machozi. Hali hiyo iliyoimbwa katika wimbo huo ilikuwa ni ya miaka ya 40 ya karne iliyopita mkoani humo. Baada ya kuanzishwa kwa China mpya, barabara nyingi zimejengwa kwa nyakati tofauti katika mkoa huo, na barabara hizo zimewaletea neema na maisha bora wakazi wa Mongolia ya Ndani.
Mwaka 2001, watu wa mji wa Alashan ulioko magharibi mwa mkoa wa Mongolia ya Ndani walifurahi sana kama sikukuu imewadia, kwa kuwa barabara nzuri ya lami inayounganisha makao ya serikali ya mji huo na nje ilikuwa imekamilika. Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita zaidi ya 700 ilimaliza historia ya kutokuwa na barabara kubwa kwa mji huo ulioko mpakani, na magari yalianza kufika huko. Wakazi wa sehemu hiyo walikuwa na furaha kubwa, walivaa nguo rasmi wanazovaa wakati wa sikukuu na kutembea kwenye barabara hiyo kwa ngamia, mara kwa mara waliteremka kukanyaga barabara hiyo wakitaka kujua ikoje. Mkazi mmoja wa huko aitwaye Bayaer alikumbusha hali ilivyokuwa kwa wakati huo, akisema,
"Barabara hii inatufanya tuwe na furaha kubwa. Wazee wenye umri wa miaka zaidi ya 80 waliwahi kusema hawataweza kuona barabara mpya kabla ya kufariki dunia, lakini sasa wemeiona. Barabara hiyo haitunufaishi sisi wenyewe tu, bali pia itawanufaisha watoto wetu."
Baada ya mji wa Alashan kumaliza historia ya kutokuwa na barabara ya lami, wilaya 101 zote za Mkoa wa Mongolia ya Ndani zilikuwa na barabara za magari, na urefu wa jumla wa barabara mkoani humo umefikia karibu kilomita laki 1.3, ambao ni mara 60 kuliko wakati mkoa huo ulipoanzishwa. Zamani hakukuwa na barabara ya mwendo wa kasi hata moja, lakini sasa barabara za kasi mwendo wa zimejengwa katika mkoa huo.
Wafugaji wengi wa mkoa wa Mongolia ya Ndani ambao zamani hawakutoka kwenye mashamba yao ya kufugia wanyama, sasa wanaweza kutoka nje kwa magari kwa urahisi, na wanawake walioolewa kwenye sehemu za mbali pia wanaweza kurudi kuwatembelea wazazi wao bila matatizo. Bibi Wurinile kutoka Hohhot, mji mkuu wa mkoa wa Mongolia ya Ndani alisema,
"Zamani nikitaka kuwatembelea wazazi wangu, nilipanda garimoshi kwanza, halafu nilibadilisha na kupanda gari, kisha kupanda mkokoteni wa ng'ombe, safari hii ilinichukua siku nne hadi tano. Lakini sasa barabara ya moja kwa moja imejengwa, inanichukua siku moja tu kuwafikia wazazi wangu."
Maendeleo ya mawasiliano ya barabara mkoani Mongolia ya ndani, yametoa mchango mkubwa kwa ustawi wa uchumi na utamaduni na kuboresha maisha ya wakazi. Barabara zinazoenea kwenye eneo kubwa la mkoa huo pia zimeleta ustawi wa biashara. Mmiliki mmoja wa hoteli Bw. Li Guoqi alisema,
"Barabara imesababisha imetuletea wateja wengi, kwa kuwa watu wanaopita wameongezeka."
Mtandao mzuri wa barabara umerahisisha safari ndefu, sasa kila mwaka watu wengi kutoka nchini na nchi za nje wanakwenda kwenye mkoa huo wenye mbuga kubwa kufanya utalii. Bw. Zhangqi kutoka mji wa Beijing alisema,
"Mawasiliano ya barabara ni mazuri, na wakazi wa Beijing wanapenda kutalii kwenye mkoa wa Mongolia ya Ndani."
Baada ya kuingia karne ya 21, kwa mujibu wa mkakati wa serikali ya China wa kuendeleza sehemu ya magharibi mwa China, serikali ya mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani iliharakisha ujenzi wa barabara. Ofisa wa Idara ya Mawasiliano ya mkoa huo Bw. Hao Jiye alisema,
"Wakati huo tulipanga kujenga barabara za mwendo wa kasi zenye urefu wa kilomita karibu 800, barabara za ngazi ya kwanza zenye urefu wa kilomita 1600, na barabara nyingi vijijini. Mkoa wa Mongolia ya Ndani una mikoa minane jirani, huo ndio mpango mkubwa sana."
Sasa mpango huo umetimizwa. Mwaka 2003 ulikuwa mwaka ambao serikali ya mkoa wa Mongolia ya Ndani ilijenga barabara nyingi zaidi na kutenga fedha nyingi zaidi kwa ajili ya ujenzi wa barabara. Barabara ni dalili ya maendeleo, na zinawasaidia watu wa makabila mbalimbali wanaoishi kwenye mkoa huo kutimiza lengo la ujenzi wa jamii yenye maisha bora lililowekwa na serikali kuu ya China.
Barabara hizo zimeleta matumaini na neema kwa wakazi wa mkoa wa Mongolia ya Ndani, na kupunguza pengo la maendeleo kati ya mkoa huo na sehemu zilizoendelea nchini China. Mkurugenzi wa idara ya mawasiliano ya mkoa huo alieleza kuwa, hadi kufikia mwaka 2010, serikali ya Mongolia ya Ndani itakamilisha kujenga barabara za mwendo wa kasi na barabara ya ngazi ya juu kati ya mji mkuu na miji mingine ya mkoa huo, barabara za ngazi ya pili kati ya miji na wilaya, barabara za lami kati ya tarafa mbalimbali, na barabara kubwa kati ya vijiji mkoani humo. Tunaamini kuwa hadi kufikia wakati huo, mtandao wa barabara kwenye mkoa wa Mongolia ya Ndani utakuwa wa kisasa zaidi, na maisha ya watu wa makabila mbalimbali pia yataboreshwa zaidi.
Idhaa ya kiswahili 2008-03-31
|