Ghuba ya Xiangsha ni ya ajabu sana, umaalumu wake ni kuwa mchanga wake unapokauka, unateleza na kumiminikia kwenye sehemu ya chini kutoka kwenye mwinuko huku ukitoa sauti kubwa. Jinsi ilivyo ni kama ndege inavyopita angani, sauti yake inapasua hewa ya mlimani. Hebu tuwasimulie hadithi moja nzuri kuhusu ghuba ya Xiangsha. Inasemekana zamani za kale kulikuwa na mungu mmoja ambaye alikuwa anapita kwenye sehemu ile akiwa na mfuko mmoja wa mchanga. Kutokana na kutokuwa mwangalifu, mchanga uliokuwa ndani ya mfuko wake ulimwagika, na sehemu hiyo ikabadilika mara moja kuwa jangwa, mungu yule alijuta sana, hivyo alitenga mahali hapo kuwa ghuba ya mchanga kwenye sehemu ya mashariki ya jangwa hilo, na kumkaribisha mungu wa radi aje kuilinda sehemu hiyo ya ghuba ya Xiangsha, kwa maneno ya Kichina ni mchanga unaounguruma. Kuanzia hapo mchanga wa sehemu hiyo unaunguruma mara kwa mara. Hiyo ni hadithi nzuri, lakini ukweli ni kuwa hicho siyo chanzo cha kuunguruma kwa mchanga. Mtaalamu anayefanya utafiti kuhusu ghuba ya Xiangsha, Bw. Li Mingke alisema,
"Hivi sasa kuna matamko ya aina mbili ya nadharia ya utafiti wa wanasayansi kuhusu mlio wa mchanga. La kwanza linasema, mlio wa mchanga unatokana mkwaruzano wa mchanga kutokana na nguvu ya nje. Aina ya pili inasema, kutokana na kupigwa na upepo, chembe za mchanga karibu zina ukubwa wa namna moja, hivyo zinapokwaruzana zinaingia kwenye hali ya mtetemeko na kuzunguka. Lakini matamko hayo ya kinadharia bado hayajathibitishwa, kwa hiyo mlio wa mchanga kwa sasa bado bado ni suala lisilofahamika."
Ni ajabu hiyo imeifanya ghuba ya Xiangsha iwe sehemu ya kuvutia. Watalii wengi wanapenda kwenda kwenye mchanga ili waweze kusikia mlio wa mchanga. Wanavaa aina maalumu ya soksi, wanapanda kwenye mwinuko wa mchanga, kisha wanalala au kukaa chini huku wakijisukuma kwa mikono ili wateleze kutoka kwenye mwinuko. Hapo mlio wa mchanga unavyosikika ni kama mlio wa chura au kama mlio wa mawimbi ya baharini. Huku wanahisi hatari na furaha ya kuteleza kwenye mchanga, na huku wanaburudishwa kwa milio ya ajabu ya mchanga. Watalii wawili waliowahi kuteleza kwenye mchanga walisema,
"Mimi hii ni mara yangu ya kwanza kufika kwenye ghuba ya Xiangsha, nimefurahi sana, ninaona kitu kinachonivutia zaidi hapa ni kuteleza kwenye mwinuko mkubwa wa mchanga, ninajiona kama nimeota mabawa, inanifurahisha sana".
(mtalii wa pili) Ninapoteleza kwenye mchanga ninafurahi zaidi kuliko ninapokuwa kwenye mchezo wa kuteleza kwenye maji, najisikia kama ninarushwa juu mara kwa mara, nilisikia moyo unadunda haraka kutokana na hofu, lakini inanifurahisha sana."
Kwenye sehemu hiyo kubwa yenye mchanga kuna kundi moja la ngamia. Watalii wanaweza kupita kwenye sehemu hiyo kwa kupanda ngamia. Watu wanaweza kujionea hali ya shwari na ukimya wakienda taratibu kwenye ngamia, ila tu wanasikia milio ya kengele za ngamia, ambayo ni tofauti kabisa na kelele za mijini. Mfanyakazi wa sehemu ya utalii ya ghuba ya Xiangsha Bi. Bei Jiaona alisema,
"Watu wengi wanapofika kwenye jangwa wanapenda kupanda ngamia, watalii wengi hawajawahi kupanda ngamia, baada ya kupanda kwenye mgongo wa ngamia, ngamia anainuka mara moja, wakati huo mtalii anaona furaha na ajabu, ngamia anapotembea, mara anainama kwa mbele na mara anainama kwa nyuma, watalii wanayumbayumba na kufurahishwa sana na hali hiyo."
Sehemu ya mandhari ya ghuba ya Xiangsha iko kwenye mji wa Eerduosi, wa mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani wa China, eneo hilo wanakaa watu wa makabila mengi, hususan watu wa kabila la wamongolia wanaokaa huko kwa wingi. Huko licha ya kuburudishwa kwa mandhari ya jangwa kubwa, watalii pia wanaweza kushuhudia umaalumu wa utamaduni wa kabila la wamongolia. Katika kambi ya wakazi wa kabila la wamongolia, mwenyeji anachukua bakuli ya fedha mkononi huku akimpa mgeni kitambaa cheupe cha Hada. Kwa kufuata muziki unaopigwa kwa fidla za jadi zenye vinyago vya farasi za wamongolia, wasichana na wavulana wa kundi la sanaa la ghuba ya Xiangsha wanafanya maonesho kuhusu sherehe ya harusi ya Eerduosi ya kabila la wamongolia. Mtaalamu wa utafiti wa ghuba ya Xiangsha, Bw. Li Mingke alisema,
"Sherehe ya harusi ya Eerduosi ni kama ua moja zuri katika utamaduni wa kabila wa Eerduosi, ambayo imekusanya nyimbo na ngoma nyingi za kabila la wamongolia. Mchezo huo ni wenye furaha na uchangamfu mkubwa, bila kujali watalii walikuwa na hali gani, lakini baada ya kutazama mchezo wa sherehe ya harusi ya Eerduosi, watafurahi sana."
Baada ya kuona maonesho ya sherehe ya harusi, watalii wanaweza kwenda kwenye maduka ya sehemu ya ghuba ya Xiangsha kununua vitu vya sanaa vyenye umaalumu wa kabila la wamongolia, vikiwemo vyombo vya dhahabu, fedha na shaba, nguo zenye rangi mbalimbali pamoja na visu vyenye umaalumu vya kabila la wamongolia.
Sehemu ya utalii ya ghuba ya Xaingsha iko kwenye jangwa la Kubuqi, ya mji wa Eerduosi, mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani, umbali wa kilomita 30 kutoka mji wa Baotou, mji mkubwa wa Mongolia ya ndani. Licha ya michezo ya jangwani kama ile ya kupanda farasi na ngamia, sherehe ya kuwasha kuni wakati wa usiku na kwenda kwenye sehemu zenye hatari, pia imeweka michezo ya kushuka kutoka angani kwa kutumia miavuli, kupanda kwenye kikapu kilichotundikwa kwenye maputo makubwa yanayopaa angani, ambayo inawafurahisha sana watalii.
Idhaa ya kiswahili 2008-03-31
|