Msikilizaji wetu Eva Malicha Manko wa Klabu ya wasikilizaji wa Kemogemba S.L.P 71 Tarime, Mara nchini Tanzania anasemaana furaha kubwa kutoa maoni yake juu ya michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008. Beijing kama mji mkuu wa kale wa enzi zote zote za China ambao pia ni mji mkuu ndio mwenyeji wa michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008, licha ya historia yake ya miaka mingi zaidi ya 3000. Bi Eva anasema ana imani kubwa kuwa michezo ya Olimpiki ya Beijing italeta changamoto kubwa kwa watu wa China na dunia nzima. Anatarajia kuwa mambo mengi yatajiri katika sherehe za ufunguzi hapo tarehe 8 mwezi August na kutokana na maandalizi bora, upendo, bidii na kiwango cha teknolojia, na ana hakika kuwa michezo ya Olimpiki ya Beijing itakuwa kwenye kiwango cha juu kabisa. Dunia moja ndoto moja ni kauli mbiu nzuri sana inayowakumbusha watu kuwa wote wako pamoja, hivyo kila mtu awe na wazo moja la kuwa pamoja.
Msikilizaji wetu huyu anaendelea kusema kuwa, China ni nchi inayoendelea kwa kasi na ni rafiki mkubwa wa Tanzania, anategemea kuona walau mtanzania mmoja atakayetembelea Beijing ili kuwaletea wasikilizaji habari kuhusu michezo na viwanja vya Olimpiki, ikiwemo uwanja wa michezo wa taifa ambao pia unaitwa kuwa ni "kiota", ambao ni uwanja uliojengwa kwa maajabu sana. Licha ya hayo Bi Eva anatarajia kuwa kutakuwa na ulinzi wa kutosha kwa wachezaji, watazamaji, na waandishi wa habari watakaoshiriki kwenye michezo ya Olimpiki ya Beijing. Ana matumani pia kuwa CRI itasimama kidete kuwapa wasikilizaji wake habari kuhusu michezo ya Olimpiki, na anamalizia barua yake kwa kuwatakia kila la kheri wanamichezo wote wa China waweze kupata medali nyingi za dhahabu na kuweza kuipa China heshima.
Msikilizaji wetu mwingine Gulam Haji Karim wa S.L.P 504 Lindi Tanzania ametuandikia barua akianza kwa kutoa salamu za urafiki kwa wafanyakazi, watangazaji na wasikilizaji wote wa Idhaa ya kiswahili ya Radio china Kimataifa. Baada ya salamu anasema ni mataumaini yake kuwa wafanyakazi wote ni wazima wanaendelea na kazi kwa furaha na amani. Bw. Karim anasema anasikitika kwa kutoandika barua kwa muda mrefu, hii ni kutokana majukumu mengi aliyonayo kila siku. Hata hivyo anasema bado anaendelea kusikiliza matangazo kama kawaida, na amepokea zawadi zote alizotumiwa. Kuhusu michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008, tayari ameshatuma majibu ya fomu namba 3 inayohusu michezo hiyo, ambayo itafunguliwa tarehe 8 mwezi nane mwaka huu na kufungwa tarehe 24 mwezi nane mwaka huu. Anawatakia mafanikio wafanyakazi wote wa Radio China kimataifa na wanamichezo wote watakaoshiriki kwenye michezo ya Olimpiki, na anaomba michezo hiyo ianze kwa usalama na kumalizika kwa amani.
Tunawashukuru kwa dhati wasikilizaji wetu Eva Malicha Manko na Gulam Haji Karim kwa barua zao za kueleza matumaini yao kwa Michezo ya Olimpiki ya 2008 itakayofanyika hapa mjini Beijing. Na hivi sasa pilikapilika za maandalizi ya kipindi cha mwisho ya Michezo ya Olimpiki zinafanyika mjini Beijing, sote tuna matarajio kuwa Michezo ya Olimpiki ya Beijing itaandaliwa vizuri, na wanamichezo kutoka nchi mbalimbali duniani watapata mafanikio kwenye michezo hiyo.
Msikilizaji wetu Damas Bundara ambaye barua zake zinatunwa na Fabian wa S.L.P 46116 Da es salaam nchini Tanzania, ametuandikia barua akianza kwa salamu na kututakia furaha, amani na baraka na kila la kheri katika mwaka mwaka huu wa 2008. Baada ya salamu Bw Bundara anatoa pongezi kwa juhudi kubwa zilizooneshwa na CRI kwa mwaka 2007. Anasema Cri imefanya juhudi kubwa katika kuboresha vipindi, usikivu wa matangazo na pia Tovuti ya idhaa ya kiswahili katika mtandao wa internet. Hayo yote yanaononyesha kuwa kazi za CRI zinastawi na nakupata maendeleo zaidi, anatoa wito juhudi hizi ziendelee. Anasema amefurahishwa sana na huduma za mwaka 2007 na ana matumaini kuwa, kwa mwaka 2008 Radio China kimataifa itaendelea kuboresha huduma zaidi, na yeye pamoja na wasikilizaji wengine watazidi kushirikiana na Radio China Kimataifa kutoa maoni na mapendekezo na ana imani kuwa vitaandaliwa vipindi vilivyo bora zaidi. Anamalizia kwa kutoa shukrani kwa kutumiwa kalenda ndogo ya mwaka 2008, na ameifurahia sana kalenda hiyo. Mungu aibariki China katika maandalizi ya michezo ya Olimpiki ya Beijing, ili michezo hiyo iwe yenye umaalamu na ya kiwango cha juu, hata kuvunja rekedi za michezo mingine ya Olimpiki ya miaka iliyopita.
Msikilizaji wetu mwingine Yaqub Said Idambira ambaye barua zake zinahifadhiwa na msikiti wa Jamia S.L.P 124 Kakamega Kenya, ameanza barua yake kwa kuwapa mkono wa heri baraka na fanaka watangazaji, viongzi na wafanyakazi wote wa idhaa ya kiswahili ya radio China kimataifa katika mwaka huu wa 2008. Anaendelea kusema kuwa bila shaka wafanyakazi wote wameanza mwaka huu kwa kheri na wakiwa na matarajio makubwa ya kupata ufanisi na matokeo bora katika kazi mbalimbali za kutoa huduma, huku wengine wakitarajia kupanda ngazi katika nyadhifa za juu na kupata nyongeza za mishahara. Lakini pia anasema anawapa pole kwa kazi na majukumu mengi yanayowakabili. Bw Idambira pia anawapa pole wasafiri wote nchini China walioathiriwa na hali mbaya ya hewa wakati mikoa kadhaa nchini China ilipokumbwa na maafa ya mvua, theluji na barafu, ambapo miundo mbinu mingi iliharibika. Hata hivyo anawapa hongera sana viongozi wa serikali ya China na watu wote kwa hatua madhubuti na za haraka walizochukua kudhibiti hali hiyo.
Msikilizaji wetu huyu anatoa shukrani kwa idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa kuwatembelea wasikilizaji wake wa wilayani Kakamega kusini ambapo waliwahimiza kudumisha amani na ushirikiano bila kusahau kuitegea sikio Radio China Kimataifa kwa habari motomoto zinazoelimisha na kuburudisha. Msikilizaji wetu anapenda kutoa rai kuhusu mashindano ya chemsha bongo, hasa katika uchaguzi na uorodheshaji wa washindi, yeye anaona kidogo si wa kuridhisha kwani kuna wasikilizaji ambao huwa na uhakika kwamba wamejibu maswali kwa ufasaha, lakini orodha inapotolewa majina ya washindi yanakuwa ni yaleyale ya washindi wa waliotajwa kuwa washindi katika chemsha bongo zilizopita, hivyo baadhi ya wasikilizaji wanaona kama hawatendewi haki. Hivyo msikilizaji wetu anaiomba idara husika kutafuta njia nyingine ya kuwajumuisha wasikilizaji kwa kuwapa nafasi sawa na kuondoa usumbufu.
Tunawashukuru msikilizaji wetu Damas Bundara na Yaqub Said Idambira kwa barua zao za kueleza matumaini yao kuwa Idhaa ya Kiswahili yia Radio China Kimataifa itaendelea na juhudi zake za kuboresha vipindi vyake ili kuwafurahisha zaidi wasikilizaji wake. Kutokana na Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 itakayofanyika mjini Beijing, siku hizi mpango wa vipindi vyetu unabadilika badilika, hakika tutajitahidi kuboresha zaidi matangazo yetu, kama ikiwezekana, mbali na matangazo yetu nchi Kenya, matangazo yetu huko Zanzibar hata nchini Tanzania pia yataboreshwa, sisi sote tungekuwa na matarajio na uvumilivu pia.
Bi Peris Shipenzi ambaye barua zake zinahifadhiwa na Bw Mbarak Mohamed Abusheri S.L.P 792-50100 Kakamega nchini Kenya, ameanza barua yake kwa kutoa mkono wa baraka na fanaka kwa watangazaji, viongozi na wafanyakazi na wasikilizaji wote wa idhaa ya kiswahili ya radio china Kimataifa kwa mwaka huu 2008, yeye anatarajia kuwa wote ni wazima wakiendelea kuchapa kazi kwa uwezo wake mwenyezi Mungu. Anasema yeye na wengine huko Kenya ni wazima buheri wa afya na wanaendelea na shughuli za ujenzi wa taifa baada ya kwisha kwa vurugu zilizotokea baada ya Uchaguzi mkuu uliopita.
Msikilizaji wetu Bi Peris Shipenzi anapenda kuishukuru Radio China Kimataifa kwa hatua yake ya kutangaza hali ilivyo ya vurugu hizo nchini Kenya, hatua ambayo ilisaidia wahisani na wachina wanaoishi nchini Kenya kutoa misaada yao kwa watu walioathiriwa na vurugu. Bi Peris anatoa shukrani za dhati kwa Radio China kimataifa na wachina wote kwa misaada yao ambayo imeonyesha utu, ubinadamu na hali ya kujali binadamu wengine wenye shida.
Msikilizaji wetu huyu pia anapenda kutoa taarifa kuwa amepokea kidadisi na kadi za salamu alizotumiwa, na anatoa shukrani zake za dhati, kwani hiyo imeonyesha kuwa amepokelewa rasmi kama msikilizaji na mwanachama wa Radio China Kimataifa. Anapenda kuhakikisha kuwa atajitahidi kutoa maoni na mapendekezo yake, ili kuboresha matangazo ya idhaa ya kiswahili ya radio china kimataifa. Na mwisho anawatakia wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa kila la kheri katika maisha, huku akitarajia kuendelea kwa ushirikiano mkubwa katika mawasiliano.
Tunamshukuru msikilizaji wetu Bi Peris Shipenzi kwa barua yake ya kueleza mchango wa matangazo yetu katika kuwahamasisha wachina na wahisani wengine kutoa misaa kwa wakenya walioathiriwa na vurugu zilizotokea nchini Kenya. Tunafurahi kuwa hivi sasa hali ya nchini Kenya imekuwa shwari, na makundi makubwa mawili ya kisiasa yamefikia makubaliano kuhusu masuala mbalimbali na kujitahidi kufufua kazi ya ujenzi wa taifa.
|