Serikali ya mji wa Shanghai, mji wa pwani mashariki mwa China, inafanya juhudi nyingi kuwapatia wakazi wake huduma za kiutamaduni.
Mliyosikia ni sauti ya michezo ya sanaa iliyooneshwa bure kwa ajili ya wakazi wa mtaa wa Hongqiao. Katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya Shanghai imekuwa inatoa bure huduma za kiutamaduni kwa wakazi wake kwa michezo ya sanaa, mafunzo ya mazoezi ya kuimarisha afya na kufanya semina ya ujuzi wa kutembelea mtandao wa internet. Mkuu wa kituo kimoja cha huduma ya maisha ya kiutamaduni kilicho chini ya uongozi wa serikali ya mji wa Shanghai Bw. Ni Bing alisema kabla ya kuchagua makundi ya wasanii na michezo ya sanaa kwa zabuni wanakusanya maoni ya wakazi na kufahamu mahitaji yao. Alisema,
"Baada ya kukusanya maoni ya wakazi na kufahamu matakwa yao tulitangaza zabuni kwa makundi ya wasanii na idara za kufundisha mazoezi ya kujenga afya na kuwaomba wataalamu watusaidie kuchagua makundi ya wasanii kutuburudisha."
Bw. Ni Bing alisema kituo chake kinakusanya mambo ya utamaduni kwa njia nyingi, na shughuli za kuwaburudisha wakazi kiutamaduni pia ni aina nyingi. Alisema,
"DVD zilizopo kwenye kituo chetu ni za aina nyingi na pia magazeti na majarida mengi, licha ya hayo tunafanya manesho ya michezo ya sanaa kwa mzunguko, maonesho hayo yanawavutia sana na watu wanaoshiriki kwenye mazoezi ya kujenga mwili pia ni wengi."
Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2007 maonesho hayo ya michezo ya sanaa ikiwa ni pamoja na opera za Kishanghai, michezo ya kuigiza ya kuchekesha na michezo ya vikaragosi ilikuwa na aina 40 na kuoneshwa mara zaidi ya 1,000, kwa watazamaji laki 2.1. Kutazama michezo ya sanaa katika majumba yaliyopo kwenye sehemu za wakazi imekuwa sehemu muhimu ya maisha ya wakazi katika siku za mapumziko.
Kwa kushirikiana na jumuiya za kijamii, serikali ya Shanghai iliwaalika wanasayansi na wasanii kutoa mihadhara. Baada ya mhadhara uitwao "Mwezi wa Utamaduni wa China" kumalizika, mwandishi wa habari alizungumza na msikilizaji Bw. Yang.
"Kwako ni mara ya kwanza kusikiliza mhadhara kama huu?"
"Hapana, nimewahi kusikiliza mihadhara mara kumi hivi."
"Wasikilizaji wako wengi?"
"Wengi."
Mihadhara huwa na mada za aina mbili, moja ni elimu ya kijamii ikiwa ni pamoja na hali ya taifa, hali ya soko la hisa, maendeleo ya jamii, taaluma na ufafanuzi wa kiusanii. Serikali ya mji iliwaalika watu mashuhuri wa nchini na wa nchi za nje kufanya mihadhara.
Tokea mwezi Juni mwaka 2004 mihadhara hiyo ilifanywa mara 7,000, na wasikilizaji walifikia milioni 2.7. Mihadhara kama hiyo inavutia sana wakazi wa Shanghai. Kuhusu mihadhara hiyo Bw. Yang alisema,
"Mihadhara kama hiyo ya bure inasaidia sana kuinua ujuzi wa watu kuhusu utamaduni."
Mtandao wa internet ni moja ya vyombo vya habari inayoenea haraka katika miaka ya hivi karibuni, ili kuufanya mtandao huo uwanufaishe vizuri wakazi wa kawaida, vituo vingi vya kutoa huduma ya mtandao wa internet vilianzishwa katika sehemu nyingi za wakazi mjini Shanghai, lakini vituo hivyo si vya burudani na kutuma barua pepe tu. Mkuu wa bodi ya wakurugenzi wa Kampuni ya Kuhudumia Wakazi mjini Shanghai Bw. Li Zhiping alisema,
"Kituo cha kompyuta kina kazi tatu, ya kwanza ni kutoa huduma ya kutembelea mtandao wa internet, ya pili ni huduma ya kusikiliza matangazo na ya tatu ni kuwapatia wakazi mafunzo ya huduma za mawasiliano. Kila kituo kina kompyuta toka 30 hadi 50."
Hivi sasa kuna vituo kama hivyo zaidi ya 1,000 kwenye sehemu zote 19 za wakazi, na vinasifiwa kuwa ni dunia mpya ya maisha ya IT."
Kutokana na ongezeko la vituo hivyo, huduma za mtandao wa internet pia zimeongezeka zikiwemo huduma za maktaba ya vitabu, huduma kwa ajili ya wazee na watoto, mafunzo ya ustadi wa kazi kwa ajili ya watu kujipatia ajira, kutoa ushauri wa kutunza afya na kuuza tikti za utalii.
Vituo hivyo vinawafundisha wazee ujuzi wa kutumia kompyuta kuanzia mwanzo kabisa. Mkurugenzi wa kituo kimoja Bw. Sun Lijun alisema, kituo chake kinatoa mafunzo ya ujuzi wa kimsingi, na mafunzo ya ngazi ya juu kuhusu matumizi ya kompyuta. Alisema,
"Tuwafundisha wazee kuanzia ujuzi wa kimsingi kabisa, mwanzoni wazee hao hata walikuwa hawajui namna ya kufungua kompyuta. Baada ya kupata ujuzi wa kimsingi tunawafundisha kwa ujuzi wa kina."
Mzee mwenye umri wa miaka 67 aliyekuwa akitembelea mtandao alimwambia mwandishi wetu,
"Ninachotaka kusoma ni habari, hasa habari za kimataifa. Kutokana na kutembelea mtandao wa internet, fikra zangu zimekuwa pana, maisha yangu yamekuwa ya maana zaidi."
Kutokana na maamuzi ya serikali ya Shanghai, huduma zote ikiwa pamoja na kutembelea mtandao wa internet, kutazama michezo ya filamu na televisheni na mafunzo ya kimsingi zote ni bure. Kuhusu maendeleo ya vituo hivyo mkuu wa kampuni ya kuhudumia wakazi Bw. Li Zhiping alisema,
"Dhamira yetu ni kupanua zaidi maeneo ya huduma yetu na kuimarisha ushirikiano kati ya vituo, ili kuboresha zaidi huduma zetu."
Idhaa ya kiswahili 2008-04-10
|