Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-04-15 17:03:22    
Bw. Brain A. Hodge kutoka Canada anayeishi mjini Fuzhou

cri

Bw. Brain A. Hodge kutoka Canada anaishi katika mji wa Fuzhou ambao ni mji mkuu wa mkoa wa Fujian ulioko kusini mashariki mwa China.

Bw. Hodge mwenye umri wa miaka 72 ni mkuu wa kampuni ya dawa ya Rocky Mountain ya Fuzhou. Katika miaka mingi iliyopita, amefanya juhudi kuhimiza mawasiliano kati ya makampuni ya China na Canada, hivyo alipewa tuzo ya urafiki ya kitaifa na serikali ya China. Bw. Hodge pia anapenda kushughulikia elimu wakati wa mapumziko. Amewahi kuwa mwalimu wa Kiingereza kwenye shule kadha wa kadhaa mjini Fuzhou, ili kuwasaidia wanafunzi wa China kujifunza Kiingereza. Alisema,

"Wasikilizaji wapendwa, nafurahi kupata fursa hii kutoa maoni yangu kuhusu maisha na kazi yangu nchini China."

Ingawa Bw. Hodge ana umri zaidi ya miaka 70, anapenda kuongea na watu. Alipozungumzia kampuni yake, alisema,

"Kampuni yetu inashughulikia dawa, tunaagiza ginseng kutoka Canada, kuzitengeneza na kuziuza kwenye masoko ya China."

Kampuni ya dawa ya Rocky Mountain ya Fuzhou ni tawi la kampuni ya ginseng ya Rocky Mountain ya Canada. Kampuni hiyo ni kampuni maarufu duniani, ambayo ina mashamba makubwa ya ginseng nchini Canada. Katika miaka ya 80 ya karne iliyopita ambapo China ilianza kutekeleza sera ya mageuzi na ufunguaji mlango, Bw. Hodge ambaye alikuwa mkurugenzi wa idara ya biashara ya kimataifa ya maendeleo ya uchumi ya mkoa wa BC wa Canada, aliwahi kutembelea China. Hivyo alijua vizuri mabadiliko ya China yaliyoletwa na sera ya mageuzi na ufunguaji mlango, alisema,

"Mwaka 1984 nilitembelea China kwa mara ya kwanza. Wakati huo China ilikuwa maskini na ilikuwa nyuma. Hata sikuweza kuamini. Nilipotembelea China tena mwaka 1987, niligundua kuwa mabadiliko makubwa yalitokea katika muda mfupi tu, na mwanzoni mwa miaka ya 90 ya karne iliyopita, hali nchini China iliendelea kuwa nzuri zaidi."

Katika miaka ya 90 ya karne iliyopita, Bw. Hodge aliyestaafu aliajiriwa na kampuni ya ginseng ya Rocky Mountain ya Canada na kuwa meneja wa ofisi ya Asia ya kampuni hiyo, alikuja tena China akatembelea mikoa mbalimbali iliyoko pwani mashariki mwa China, ili kuchunguza masoko ya ginseng. Baada ya uchunguzi, Bw. Hodge aligundua kuwa mkoa wa Fujian ni kiini cha shughuli za uzalishaji wa ginseng nchini China. Hivyo alitoa pendekezo la kujenga kiwanda cha kuzalisha ginseng mkoani humo, alisema,

"Nilipofanya kazi mjini Shanghai, nilitaka kuanzisha kiwanda mkoani Fujian. Kwa sababu masoko ya hapa ni makubwa, miundo mbinu imekamilika, na nguvu kazi ni nyingi. Mwanzoni serikali za mkoa wa Fujian na mji wa Fuzhou zilinipatia uungaji mkono mkubwa. Zilinipatia mshauri ili nifahamu sera na kanuni mbalimbali. Aidha zilinipatia habari nyingi ambazo nilizipeleka nchini Canada, na kuwasaidia watu wanaomiliki hisa za kampuni waamini kuwa China ni sehemu nzuri kwa uwekezaji."

Lakini uwekezaji haukuendelea bila ya matatizo. Bw. Hodge alikabiliwa na matatizo kadhaa, hakujua namna ya kufanya biashara nchini China, hivyo mwanzoni kampuni yake ilipata hasara, alisema,

"Mwanzoni kampuni yetu ilipata hasara. Mkuu wetu nchini Canada aliniuliza sababu yake, na aliniambia kuwa siwezi kufanya kazi kwa mbinu za kimagharibi tu, bali natakiwa kujua namna ya kufanya kazi nchini China na kufahamu mawazo ya wafanyabiashara wa China."

Baadaye Bw. Hodge alikutana na Bw. Jiang Shaoshu ambaye ni meneja mkuu wa hivi sasa wa kampuni hiyo. Bw. Jiang alimsaidia kuunda kikundi chenye wafanyakazi hodari, na kampuni hiyo ilianza kupata maendeleo hatua kwa hatua. Bw. Hodge alisema,

"Meneja mkuu wa hivi sasa ni meneja hodari ambaye ana uzoefu wa usimamizi wa miaka 17, alinisaidia kuunda kikundi cha wafanyakazi hodari, hivi sasa kampuni yetu imenunua ardhi na itajenga kiwanda kipya. Tumepata idhini mbalimbali kutoka serikalini, mpango wa ujenzi wa kiwanda kipya umemalizika, na fedha zitatumiwa. Hivyo mustakabali wa kampuni yetu ni mzuri."

Katika miaka mingi iliyopita, Bw. Hodge alifanya juhudi kuhimiza mawasiliano ya kiuchumi kati ya China na Canada, na kuyasaidia makampuni ya nchi hizo mbili kuwasiliana. Yeye ni naibu mkurugenzi wa shirikisho la makampuni yanayowekezwa na wafanyabiashara wa nje la Fuzhou. Akiwa ni mshauri wa mambo ya kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji wa serikali ya mji wa Fuzhou, anakutana na viongozi wa mji huo na kutoa mapendekezo yake mara kwa mara. Wakati wafanyabiashara wa nje wanapofanya uchunguzi mjini humo, serikali ya mji huo humwalika Bw. Hodge kukutana na wafanyabiashara hao, na yeye huwaalika wafanyabiashara hao kutembelea kampuni yake, na kuelezea uzeofu wake, ili kuwasaidia wajue kwa nini mji huo ni mahali pazuri pa uwekezaji. Bw. Hodge pia anaisaidia serikali ya Fuzhou kutuma ujumbe kutembelea Canada, na kukutana na wafanyabiashara wa huko, ili kueleza fursa za kibiashara mkoani Fujian na mjini Fuzhou, alisema,

"Nafikiri mimi ni mwenyeji wa Fuzhou. Kampuni yangu iko hapa, na familia yangu iko hapa. Nafikiri ninapokuwa hapa, ni lazima nifanye juhudi kuisaidia timu yangu. Hivyo nafurahi kuwa mshauri wa serikali ya hapa."

Kutokana na mchango wake, Bw. Hodge alisifiwa na serikali ya huko. Mwaka 1999 alipata tuzo ya urafiki ya mkoa wa Fujian. Mwaka 2001 hadi mwaka 2003 alipata tuzo ya urafiki ya kimataifa ya mji wa Fuzhou. Mwaka 2003 alipewa tuzo ya urafiki ya Jamhuri ya Watu wa China na serikali ya China. Bw. Hodge anapenda michezo na kutembelea vijiji wakati wa mapumziko. Kila ifikapo majira ya joto, katika wikiendi anapenda kupumzika wilayani Yongtai ambayo inasifiwa kuwa ni bustani ya Fuzhou. Aidha, anapenda kushughulikia elimu, anawasiliana na idara za elimu kwa karibu, kuwasaidia watoto kujifunza Kiingereza, na kuwasaidia walimu wa China kufanya mazoezi ya kuzungumza Kiingereza. Bw. Hodge alisema,

"Watoto wengi wanakuja nyumbani kwangu kufanya mazoezi ya kuzungumza Kiingereza wakati wa wikiendi. Wanaweza kusoma na kuandika Kiingereza vizuri, lakini hawawezi kuzungumza. Sababu muhimu ni kuwa walikuwa na hofu, hivyo mwanzoni walikaa kimya tu. Wakati huo nilijiuliza, nitafanya nini? Nilianza kucheza pamoja nao, ili kuwasaidia watambue kuwa Wachina na wageni wanatofautiana wakati wa kufikiri mambo. Walipopunguza hofu moyoni waliweza kuanza kuzungumza Kiingereza. Hivi sasa watoto hao wanatembelea nyumbani kwangu mara kwa mara, tumekuwa marafiki wakubwa, na mimi napenda maisha ya hapa."