Filamu ya kiserikali ya michezo ya Olimpiki ya Beijing mwaka 2008 ilianza kupigwa mwezi Agosti mwaka jana, tarehe 12 Machi mwaka huu sherehe ya kuanza kupiga filamu hiyo nje ya China ilifanyika, na kundi la kwanza la wapiga filamu hiyo liliondoka Beijing kwenda nchi za nje, kisha makundi mengine yameondoka pia kwa nyakati tofauti. Filamu hiyo ilianza kupigwa wakati moto mtakatifu wa michezo ya Olimpiki ulipowashwa huko Stockholm, Sweden.
Tokea mwaka 1912 filamu ya kwanza ya kiserikali ilipopigwa, kila michezo ya Olimpiki inapofanyika huwa kunakuwa na filamu yake ya kiserikali, na hii imekuwa sehemu muhimu ya kazi ya kamati ya maandalizi ya michezo hiyo. Jukumu la filamu ya kiserikali ni kurekodi hali ya michezo ya Olimpiki kwa pande zote, kuonesha mashindao yanayosisimua na kutoa maelezo kuhusu wachezaji. Filamu hiyo itakuwa kumbukumbu adimu katika historia ya michezo ya Olimpiki na kuhifadhiwa kwenye jumba la makumbusho la Lausanne, Uswisi, ili kuhamasisha na kuonesha ushujaa kwa vizazi vya baadaye. Mtengenezaji wa filamu hiyo Bw. Wu Qi alisema,
"Filamu ya kiserikali ya michezo ya Olimpiki inapigwa kutokana na maagizo ya Kamati ya Kimataifa ya Michezo ya Olimpiki ili kurekodi hali ya mashindano na shughuli zinazohusika. Filamu kuhusu michezo hiyo huwa nyingi, lakini inayotambuliwa ni filamu inayopigwa kutokana na maagizo ya kamati hiyo tu na kutunzwa katika jumba la makumbusho, hii ndiyo filamu ya kiserikali. Sehemu za filamu hiyo ni pamoja na ufunguzi, mbio za mwenge, kurusha njiwa n.k. yote hayo ni ya lazima, na sehemu nyingine zilizobaki ni kwa ajili ya mambo ambayo nchi mwenyeji inataka kuonesha."
Filamu ya michezo ya Olimpiki ya Beijing mwaka 2008 ni filamu ya 22 ya kiserikali, na pia ni filamu ya kwanza ya kiserikali inayopigwa na China. Mwongozaji wa upigaji wa filamu hiyo Bi. Gu Jun ana uzoefu wa kupiga filamu za kumbukumbu. Kabla ya hapo amepiga filamu ya hali ya maandalizi ya michezo ya Olimpiki yaliyoanza mwaka 2001. Filamu ya kiserikali ya michezo ya Olimpiki ya Beijing ni tofauti na filamu nyingine za kawaida, nafasi iliyomruhusu mwongozaji wa upigaji wa filamu apige kwa mtazamo wake ni ndogo, hata hivyo Bi. Gu Jun alisema atajitahidi kuonesha usanii wake katika filamu hiyo. Alisema,
"Filamu hiyo ya michezo ya Olimpiki ya Beijing mwaka 2008 itawaonesha wachezaji wanaotoka nchi na sehemu tofauti na makabila tofauti ambao wanawakilisha tamaduni tofauti duniani. Licha ya kuwaeleza ufanisi wao wa kuweza kushiriki kwenye michezo hiyo na kueleza hadithi za washindi pia itaeleza jinsi walivyojitahidi na kupata ushindi."
Kabla ya hapo filamu 21 za zamani kuhusu michezo ya Olimpiki zilielezea jinsi wachezaji wengi walivyofanya juhudi na kuonesha moyo wa Olimpiki. Kuanzia mwaka 1984, kutokana na kuwa hali ya michezo hiyo inatangazwa papo hapo kwenye televisheni wakati michezo inapofanyika, filamu ya kiserikali inapokamilishwa michezo itakuwa imemalizika, kwa hiyo mkazo unaotiliwa katika filamu ya kiserikali sio hali ya mashindano yenyewe bali ni hadithi inayosisimua kabla ya wachezaji kushiriki kwenye mashindano. Muda wa filamu ya kiserikali ni saa mbili tu, katika muda huo mfupi haiwezekani kuonesha mambo yote bila kuchagua sana na kuyafupisha.
Filamu za zamani kuhusu michezo ya Olimpiki zilitiliwa mkazo zaidi kwenye mashindano, lakini filamu ya michezo ya Olimpiki ya Beijing inapigwa mapema kabla ya mashindano, mwongozaji wa upigaji wa filamu hiyo Bi. Gu Jin alieleza kwamba filamu ya kiserikali ilianza kupigwa tarehe 12 Machi mwaka huu, makundi kumi ya wapigaji filamu yalikwenda kukusanya habari katika nchi za Marekani, Ujerumani, Italia, Sweden, Iran, Jamaica, Brazil, Ethiopia na Athens nchini Ugiriki. Filamu hiyo ilianza kupigwa tokea tarehe 24 moto mtakatifu wa michezo ya Olimpiki ulipowashwa.
Kutokana na mambo mengi yanayotakiwa kupigwa, mpigaji filamu Bw. Wang Jing alisema,
"Mada ya filamu hiyo ni upatanifu, na upatanifu sio neno tupu bali linamaanisha uvumilivu kati ya tofauti, michezo ya Olimpiki ni fursa ya kuonesha uvumilivu huo."
Filamu ya michezo ya Olimpiki itapigwa zaidi katika siku 16 ambapo michezo inapofanyika. Kutokana na makadirio filamu hiyo itaweza kuoneshwa mwishoni mwa mwaka 2008. Filamu hiyo itarekodi hali ya michezo yenyewe kwa pande zote na kuonesha moyo wa Olimpiki na utamaduni pekee wa michezo hiyo inayofanyika nchini China. "Dunia moja na ndoto moja" ni kaulimbiu ya michezo hiyo, na pia ni mwongozo wa fikra za upigaji wa filamu hiyo.
|