Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-04-30 20:16:14    
China yaimarisha udhibiti wa wadudu wanaoeneza magonjwa kwa binadamu kwa ajili ya michezo ya Olimpiki

cri

Majira ya joto wakati ambapo michezo ya Olimpiki itafanyika mjini Beijing mwaka huu, ni kipindi ambacho kuna kuwa na wadudu wengi wanaoweza kueneza magonjwa kwa binadamu, wakiwemo mbu, inzi, mende na panya. Ili kuhakikisha kuwa michezo ya Olimpiki haiathiriwi na wadudu hao na kupunguza kadiri iwezekanavyo madhara ya kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza, wizara ya afya ya China imeweka mpango kamili na kufanya maandalizi kwa makini.

wadudu wa kawaida wanaoeneza magonjwa kwa binadamu ni pamoja na mbu, inzi, panya, mende na chawa, wadudu hao wanaweza kueneza magonjwa mengi kwa binadamu yakiwemo tauni na homa ya dengue, kama wachezaji wakiumwa na wadudu hao, mashindano na mapumziko yao pia yataathiriwa kiasi. Kwa hivyo, hali ya udhibiti wa wadudu hao katika miji inayoandaa michezo ya Olimpiki itakuwa na athari fulani kwa ufanisi wa michezo hiyo. Mkurugenzi wa idara ya kinga na udhibiti wa magonjwa katika wizara ya afya ya China Bw. Qi Xiaoqiu alisema:

"wakati michezo ya Olimpiki itakapofanyika, wachezaji, makocha, waandishi wa habari na watalii wapatao laki 6 watakuja China kutoka nchi mbalimbali duniani. Wakati huo idadi ya watalii kutoka nchini inakadiriwa kufikia milioni 1.1. hali hiyo itatoa shinikizo kubwa kwa kazi za uhakikisho wa afya ya umma nchini China. Kwa hiyo kazi za udhibiti wa wadudu wanaoeneza magonjwa kwa binadamu, hasa kuinua uwezo na teknolojia za kuzuia na kudhibiti wadudu hao, zina umuhimu mkubwa kwa michezo hiyo."

Beijing ikiwa ni mji unaoandaa michezo ya Olimpiki, ulianza kufanya maandalizi mapema. Kuanzia mwaka 2005 idara za afya za Beijing zilianza kupima na kusimamia idadi ya wadudu hao kwenye sekta na sehemu muhimu kote mjini Beijing, hasa kwenye viwanja na majumba ya michezo na sehemu zilizo karibu nazo, pia zilifanya tathmini na kupata data muhimu kuhusu uwezekano na madhara ya matukio ya afya ya umma yanayoweza kusababishwa na wadudu hao katika muda wa michezo ya Olimpiki.

Mbali na hayo, Beijing pia ilijifunza uzoefu wa mafanikio ya hatua za udhibiti wa wadudu zilizochukuliwa kwenye michezo ya Olimpiki ya Sydney na Athens na kuweka mpango wa utekelezaji kuhusu udhibiti wa wadudu wanaoeneza magonjwa wa binadamu. Daktari mkurugenzi wa kituo cha kinga na udhibiti wa magonjwa cha Beijing Bw. Zeng Xiaopeng alisema, mpango huo ni pamoja na kuanzisha mtandao wa kazi za udhibiti wa wadudu hao kote mijini, kuunda kundi la kazi hiyo na kuweka mpango na utaratibu wa dharura wa udhibiti wa wadudu hao. Hivi sasa mpango huo umetekelezwa vizuri. Bw. Zeng Xiaopeng alisema:

"mpango huo umeweka malengo ya jumla, la kwanza ni kupunguza idadi ya jumla wadudu wanaoeneza magonjwa kwa binadamu kote mjini Beijing; la pili ni kupunguza kadiri iwezekanavyo hatari za magonjwa yanayoweza kuenezwa na wadudu hao; la tatu ni kuhakikisha viwanja na majumba ya michezo ya Olimpiki na sehemu zinazohusika zinaweza kufikia au kuzidi kiwango cha taifa. Kutokana hali ya utekelezaji ya hivi sasa, malengo hayo yametimizwa kimsingi."

Bw. Zeng Xiaopeng alisema, wizara ya afya ya China imefanya juhudi kubwa ili kuhakikisha kazi za udhibiti wa wadudu zinatekelezwa bila matatizo. Kwa mfano, ili kuchunguza aina za wadudu wanaoeneza magonjwa kwenye majira ya joto mjini Beijing na magonjwa yatakayoweza kuenezwa nao, idara za afya za Beijing zilifanya upimaji katika viwanja na majumba 31 ya michezo ya Olimpiki yaliyomilika kujengwa.

Wakati michezo ya Olimpiki inapokaribia siku hadi siku, hivi sasa kazi za maandalizi yake zimeingia kwenye kipindi cha mwisho, na idara za afya za Beijing pia zinafanya kadiri ziwezavyo kazi za udhibiti wa wadudu hao. Katika miezi ya Mei, Juni na Julai, idara za afya za Beijing zitafanya shughuli za kuangamiza wadudu kwenye maeneo yaliyoko kilomita 1 hadi 2 kutoka kwenye viwanja na majumba ya michezo, hoteli na hospitali wafadhili kwa ajili ya michezo ya michezo ya Olimpiki, pia zitatuma wataalamu kufanya upimaji na ukaguzi kwenye sehemu hizo.

Idara za afya za Beijing pia zitahamasisha wakazi wa mji huo kwenye shughuli za kuangamiza wadudu waharibifu, hasa kwenye sehemu zinazozunguka viwanja na majumba ya michezo ya Olimpiki, bustani, jumuiya za makazi na mifereji ya maji. Ofisa wa idara moja ya afya ya Beijing Bw. Sun Xianli alisema:

"mwaka huu kazi za udhibiti wa wadudu waharibifu kwa ajili ya michezo ya Olimpiki mjini Beijing zitaweka mkazo katika kuhamasisha wakazi na kufanya shughuli mbalimbali za kuzuia na kudhibiti wadudu hao, ili kupunguza kwa ufanisi idadi ya wadudu hao na kuweka msingi imara kwa michezo hiyo."

Aidha, mbali na Beijing, miji 5 inayoshiriki kwenye maandalizi ya michezo ya Olimpiki ikiwemo Qingdao na Shenyang, na miji 33 ya utalii nchini China pia imechukua hatua kudhibiti wadudu wanaoeneza magonjwa kwa binadamu na imepata ufanisi dhahiri, ili kuweka mazingira mazuri na safi kwa ajili ya michezo hiyo na kuhakikisha afya ya wachezaji, makocha na watalii kutoka nchini na nchi za nje katika muda wa michezo hiyo.

Wasikilizaji wapendwa, mlikuwa mkisikiliza maelezo kuhusu China inavyoimarisha udhibiti wa wadudu wanaoeneza magonjwa kwa binadamu kwa ajili ya michezo ya Olimpiki. Asanteni kwa kutusikiliza. Kwa herini!