Q: Bw. Sun, kwanza tafadhali ujijulishe.
A: Mimi ninaitwa Sun Baohua, mwalimu wa Kiswahili, kuanzia mwaka 1973. Sasa nina umri wa miaka 61, kwa kweli nimefikia umri wa kusaafu, lakini kwa kutokana na upungufu wa walimu katika ofisi yetu, ninaendelea kuajiriwa.
Q: Bw. Sun, lini ulianza kujifunza lugha ya Kiswahili? Kwa nini ulichagua kozi hiyo wakati ule?
A: Mimi nilianza kujifunza Kiswahili tangu mwaka 1965, na nilichagua kozi hiyo kwa kweli sikuwa na habari yote juu ya lugha hiyo, ila tu nikasema kuingia chuo kikuu cha lugha za kigeni cha Beijing, basi inatosha. Mimi sikuja kujifunza lugha yoyote, wakati ule nilikuwa na imani kwamba baada ya kuhitimu chuo hiki, kila mtu atapata ajira, hana shida yoyote.
Q: Ujulishe hali yenu ya kujifunza Kiswahili wakati ule?
A: Tulipoingia kwenye chuo hiki, na tukaanza kujifunza lugha ya Kiswahili katika hali ngumu sana. Tulikuwa hatuna kitabu, na kila wiki tunafundishwa vipindi kumi na mbili, walimu wa Kichina wanafundisha vipindi kumi, na mtaalumu kutoka Tanzania anafundisha vipindi viwali.
Q: Nilisikia kuwa kabla ya kuwa mwalimu wa Kiswahili wa chuo kikuu cha lugha za kigeni cha Beijing, ulijifunza lugha ya Kiswahili kwa miezi minane tu, ndiyo?
A: Baada ya kuwa mwalimu nilikutana na shida nyingi sana, kwa kuwa nilikuwa nimesoma Kiswahili kwa miezi minane tu, yaani kuanzia miaka 1965 Septemba mpaka mwezi Mei mwaka uliofuata. Kwa hivyo sisi wanafunzi tulikuwa tukakatishwa masomo kama watoto walivyokatishwa maziwa. Kwa kweli masomo ya miezi minane haitoshi kwa kazi ya walimu, haitoshi kabisa! Mwalimu akitaka kusimama katika chuo kikuu cha lugha za kigeni cha Beijing, lazima awe na ujuzi mwingi, asipokuwa na ujuzi mwingi, atazomewa na wanafunzi.
Q: Baadaye ulikwenda nchi za Afrika ya Mashariki kwa mara nyingi, safari hizo zilihimiza kiwango chako cha lugha ya Kiswahili, Je, unakumbuka safari yako ya kwanza barani Afrika?
A: Mara ya kwanza nilipokwenda Afrika, nilikwenda Tanzania visiwani, huko Pemba. Kwa kweli maisha ya huko ni magumu sana, sisi wataalamu tunaishi katika vibanda, si nyumba hasa. Lakini nilifanya kazi huko kwa mwaka mmoja na miezi mitano. Katika muda huo naona Kiswahili changu kimeendelea, hata mswahili mmoja aliniambia hivi, Sun, sasa Kiswahili chako hakuna shida tena, lakini ulipokuja hapa mwanzoni uliongea Kiswahili cha vitabuni tu, lakini sasa umeshaongea kama sisi.
Q: Mwaka 1990 ulikwenda Kenya kwa mara ya kwanza, wakenya wanaongea kwa lugha ya Kiswahili au lugha ya Kiingereza?
A: Safari hiyo nilikuwa na madhumuni kwamba nataka kujua Kiswahili kinavyotumika katika nchi hiyo. Maana kabla ya hapo watu waliniambia kuwa Kiswahili hakitumiki nchini Kenya, lakini mimi nataka kujua hali ilivyo. Basi nikaenda, nilipofika katika kiwanja cha ndega cha Nairobi, na kufanya shughuli za custom nikaongea na mfanyakazi wa huko. Je, mnazungumza kwa Kiswahili? Yeye akaniambia tunazungumza sana. Basi kuanzia hapo moyo wangu ukatulia. Katika miaka yote miwili ya huko, nilitumia Kiswahili.
Q: Niliambiwa wakati ulipokuwa ni mwanafunzi, mlikuwa hamna vitabu vya Kiswahili, baadaye wewe na walimu wengine mlitunga vitabu vya Kiswahili vya kwanza nchini China, ujulishe jambo hili?
A: Masomo ya vitabu vya Kiswahili ni muhimu sana kwa kazi hiyo ya kufundisha, pia ni kwa wanafunzi na walimu. Kabla ya miaka ya 90 ya karne iliyopita tulikuwa hatuna vitabu, masomo yalikuwa hayaendelei kwa utaratibu. Baada ya hapo tukazingatia zaidi masomo ya Kiswahili, kwa hivyo tukaamua kutunga vitabu vya Kiswahili kuanzia kipindi cha matamshi, na tulihariri vitabu vinne kwa jumla katika muda wa miaka minne hivi. Sasa bado yanatumika katika vyuo mbalimbali hapa nchini.
Q: Tafadhali tujulishe hali ya kutumika kwa vitabu hivyo mlivyotunga.
A: Vitabu hivi vilikaribishwa na wanafunzi na walimu wa vyuo vingine. Mpaka leo bado wanaendelea kuvitumia. Nafikiri ndio mchango tuliotoa katika kazi hiyo ya kufundisha. Kama tujavyo vyuo vilivyofungua kozi ya Kiswahili ni vitano hivi, ni chuo kikuu cha lugha za kigeni cha Beijing, chuo kikuu cha radio cha Beijing, chuo kikuu cha lugha za kigeni cha Tianjin, chuo kikuu cha ualimu cha Tianjin, na chuo kikuu cha lugha za kigeni cha Luoyang.
Idhaa ya kiswahili 2008-05-02
|