Mkoa wa Hainan ni mkoa ulioko kusini zaidi nchini China, ambao unatazamana na mkoa wa Guangdong. Kisiwa cha Hainan ni kisiwa kikubwa cha pili nchini China. Mkoa huo ulianzishwa rasmi mwaka 1988, na eneo maalum la uchumi la Hainan pia lilianzishwa wakati huo, ambalo ni eneo maalum kubwa zaidi la uchumi nchini China.
Kutokana na kuwa na idadi ndogo ya watu, na kuwa na mawasiliano magumu na sehemu za ndani za China, miaka 40 baada ya kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China, uchumi wa mkoa wa Hainan ulipata maendeleo pole pole, na pengo kati ya mkoa huo na mingine ya China lilikuwa kubwa. Thamani ya uzalishaji mkoani humo katika mwaka 1987 ilikuwa yuan bilioni 5 tu. Mtafiti wa Taasisi ya sayansi ya kijamii ya China Bw. Liao Xun alipofika Haikou, mji mkuu wa mkoa huo mwaka 1988, hali ya kuwa nyuma ya huko ilimshangaza sana, alisema
"Mji huo ulikuwa kama kijiji. Niliposhuka kwenye ndege, nilifiriki uwanja wa ndege ni kama kituo cha mabasi cha miji mingine iliyoko kaskazini mwa China. Wakazi walikuwa wanafuga kuku na nguruwe nyumbani. Ni barabara mbili au tatu tu za mji huo zilijengwa kwa saruji na lami, na nyingine zote zilikuwa zimejengwa kwa udongo. Kuku, bata, nguruwe na mbwa walionekana hapa na pale. Watu kutoka sehemu nyingine walishangaa sana, kwa nini mji mkuu wa mkoa uko nyuma sana."
Bw. Liao Xun alialikwa na serikali ya mkoa wa Hainan ili kuisaidia kutunga mpango na kuchukua hatua. Ingawa mkoa huo bado ulikuwa nyuma wakati huo, lakini mustakabali wa eneo hilo maalum la uchumi ulimfanya aache kazi yake mjini Beijing. Hivi sasa yeye ni naibu mkuu wa chuo cha utawala cha Hainan. Alisema watu walikuwa na imani kuwa, uchumi wa Hainan bila shaka utapata maendeleo makubwa kutokana na sera za kuunufaisha mkoa huo, alisema,
"Maendeleo makubwa ya mkoa huo yalitegemea sera za kuunufaisha. Sera zote zilifanyiwa utafiti, na kwa ujumla kulikuwa na sera 30. Sera ya uuzaji bidhaa nje ilitoa mchango mkubwa zaidi. Katika miaka mitatu ya mwanzo, ustawi wa biashara ya nje ulihimiza ustawi wa hoteli, mikahawa na utalii, na uchumi wa mkoa huo ulipata maendeleo mwaka hadi mwaka."
Bw. Liao Xun ni mmoja kati ya watu waliohamia mkoani Hainan. Wakati huo mkoa huo ulikuwa ni sehemu nzuri ya uwekezaji. Watu laki kadhaa waliingia mijini Haikou na Sanya. Mwanzoni mwa miaka ya 90 ya karne iliyopita, serikali ya China ilianza kufanya mageuzi ya nyumba, na kuendeleza masoko ya nyumba. Kutokana na ongezeko la idadi ya watu na maendeleo ya eneo maalum la uchumi mkoani Hainan, uwekezaji kwenye ujenzi wa nyumba ulistawi sana. Wakati uwekezaji ulipostawi zaidi, kulikuwa na makampuni elfu 20 kwenye kisiwa hicho chenye watu wasiozidi milioni 1.6.
Kwa wastani kila watu 80 walikuwa na kampuni moja ya nyumba, na katika miaka mitatu bei za nyumba ziliongezeka kwa zaidi ya mara nne. Uwekezaji wa ujenzi wa nyumba ulipita kiasi. Mwaka 1993, kutokana na maendeleo yasiyo na utaratibu ya masoko ya nyumba kwenye sehemu kadhaa, serikali ya China ilichukua hatua mbalimbali. Kutokana na udhibiti wa serikali kuu, uwekezaji wa kupita kiasi kwenye ujenzi wa nyumba mkoani Hainan uliweza kuzuiliwa.
Mkoa wa Hainan ulianza kutunga mpango wa maendeleo unaofuata hali halisi ya huko. Katikati ya miaka ya 90 ya karne iliyopita, kutokana na ongezeko la mapato na matumizi ya wakazi wa mikoa ya sehemu za ndani ya China, na hali ya hewa ya sehemu iliyoko karibu na Ikweta na mazingira mazuri ya mkoa wa Hainan, serikali ya mkoa huo ilitoa mpango wa miaka mitano ikiamua kuendeleza viwanda, kilimo cha mazao ya sehemu iliyoko karibu na Ikweta na shughuli za utalii.
Msemaji wa idara ya kilimo ya mkoa huo Bw. Chen Yongwang alisema mkoa huo ulitambua kuwa kutokana na kuwa na mwangaza wa kutosha wa jua na mvua nyingi, wakazi wa huko wanaweza kupanda matunda na mboga katika majira ya baridi na kuyauza kwenye masoko ya sehemu mbalimbali za China. Eneo la mashamba ya matunda na mboga mkoani humo la mwaka 2007 liliongezeka mara mbili kuliko mwaka 1987, na sehemu kubwa ya mapato ya wakulima inatokana na uuzaji wa mazao hayo, Bw. Chen alisema,
"Tulifanya marekebisho ya miundo ya kilimo, kuendeleza kilimo katika majira ya baridi, kuanzisha chapa maarufu, na kuanzisha kituo cha uzalishaji wa mazao cha mkoa wa Hainan. Mwaka 2007 uzalishaji wa matunda na mboga ulifikia tani milioni 4, hasa uzalishaji wa mazao katika majira ya baridi, ambao uliongezeka kwa kiasi kikubwa kuliko wakati wa kabla ya mkoa wetu kuanzishwa, hayo ni mabadiliko makubwa. kuanzia katikati ya mwezi Novemba hadi mwishoni mwa mwezi Mei ni kipindi kizuri cha kilimo na matunda na mboga katika majira ya baridi mkoani humo."
Kutokana na mpango mwafaka, shughuli za utalii zimepata maendeleo makubwa kwenye kisiwa cha Hainan. Hivi sasa hoteli zaidi ya 900 zimejengwa mkoani humo, ambazo zinaweza kuwapokea watalii milioni 20. Mwaka 2007 mkoa huo ulipokea wataalii milioni 18 wa China na kutoka nchi za nje. Mkurugenzi wa idara ya utalii ya Hainan Bw. Zhang Qi alisema lengo la maendeleo ya utalii la mkoa huo ni kuendeleza Hainan kuwa kisiwa cha utalii duniani, Bw. Zhang alisema,
"Katika siku za usoni mkoa wa Hainan utajenga kisiwa cha utalii duniani kutokana na maliasili yake ya kipekee, mazingira mazuri ya kimaumbile na viumbe. Tutafanya matangazo kuonesha kuwa mkoa wa Hainan ni kisiwa kilichoko kwenye ukanda wa Ikweta na sehemu nzuri ya mapumziko. Maliasili, mazingira ya asili na viumbe mkoani mwetu ni sawa na kwenyesehemu nyingine duniani. Tutafanya matangazo, usimamizi wa shughuli za utalii na ujenzi wa majengo ya kitalii kutokana na mpango huo."
|