Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-05-06 19:19:29    
Barua 0506

cri

Bw. Emanuel Mollel wa Dar es Salamu Tanzania ametuletea barua pepe akisema, ni matarajio yangu kwamba nyote hamjambo. Kwanza niwapongeze kwa kazi nzuri ya maandalizi ya Michezo ya Olimpiki 2008. Tumeuona Mwenge - umepokelewa hapa kwetu kwa amani na kukimbizwa vivyo hivyo. Kwa kweli tumefurahi na kuridhika na maandalizi. Nina imani kazi ya maandalizi kwa ajili ya michezo hiyo huko nyumbani yamekamilika kama ninavyokumbuka jinsi watu walivyokuwa wakichakarika usiku na mchana. Hata hivyo napenda niwape pole kwa matukio ya hivi karibuni ambayo yananuia kuipaka matope kazi nzuri iliyoanzishwa. Matukio hayo si mengine bali ni yale ya Tibet yaliyoongozwa na kibaraka Dalai Lama. Inasikitisha kwamba anaanzisha vurugu wakati shughuli zimeiva. Kwa maoni yangu sidhani kama ni uungwana. Kama mtu una jambo si unazungumza na wahusika? Kwa hakika njia aliyotumia si halali wala si ya mwafaka. Nawatakieni kila la kheri.

Tunamshukuru kwa dhati Bw. Emanuel Mollel kwa barua yake ya kueleza mbio za kukimbiza kwa kupokezana mwenge wa Michezo ya Olimpiki zilizofanyika huko Dar es Salaamu, hapa Beijing tumeona picha nyingi kuhusu watanzania wenye uchangamfu mkubwa waliofurahia mbio hizo, tumeona hali hii kweli imeonesha urafiki mkubwa wa jadi kati ya China na Tanzania.

Msikilizaji wetu Consalata W. Mng'ara wa S.L.P 5088 Nairobi nchini Kenya ameanza barua yake kwa kuwasalimu watangazaji na wasikilizaji wote wa idhaa ya kiswahili ya radio China Kimataifa. Baada ya salaamu hizo anasema anapenda kutoa shukrani zake kwa kazi nzuri ambayo imefanyika kwa mwaka wote wa 2007 hadi wakati huu. Bibi Consalata anasema, CRI imeweza kuonesha matumizi ya lugha sanifu ya kiswahili katika matangazo yake na matangazo yake ni ya kiwango cha juu.Lakini ombi lake ni kuwa, kama inawezekana CRI ingeanzisha kipindi maalum cha vijana kitakachokuwa kinachoelimisha na kutoa maoni kuhusu jinsi mtu anavyoweza kufahamu vipaji vyake mapema.

Bi Consolata pia anashukuru kwa zawadi alizotumiwa, kadi inayoonyesha ukuta mkuu wa Beijing, Sichuan mji mzuri wa panda na pia kadi za salamu na bahasha ziizolipiwa.zawadi zingine ni pamoja na michoro maraidadi na orodha ya wasikilizaji waliopata nafasi ya kwanza hadi ya tatu katika shindano la chemsha bongo kuhusu vivutio vya mkoa wa Sichuan maskani ya panda, anasema huo ni ukarimu mkubwa. Anamaliza barua yake kwa kuwatakia wafanyakazi wote wa idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa mafanikio na maendeleo katika kazi.

Tunamshukuru msikilizaji wetu Consalata W. Mng'ara kwa barua yake ya kueleza usikivu wake kuhusu matangazo yetu na kusifu juhudi zetu, lakini kwa kweli bado tunatakiwa kufanya bidii zaidi ili kukidhi mahitaji ya wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu mwingine Bwana Nundu Klala wa S.L.P 523 Bungoma, Kenya, anaanza barua ya kwa kutoa pongezi zake kwa moyo mkunjufu kwa kazi nzuri inayofanywa na idhaa ya kiswahili ya radio China Kimataifa. Anasema yeye pamoja na wasikilizaji wengine akiwemo Ayub Mutanda wakiwa huko Bungoma wanaendelea kuipigia debe idhaa ya kiswahili ya CRI, na wanawaombea wafanyakazi wote na wasikilizaji wote afya njema na baraka ili waweze kusukuma vyema gurudumu, anamalizia kwa wataendelea kuwa wasikilizaji wema".

Tunamshukuru sana Bwana Nundu Klala na wenzake huko Bungoma Kenya kwa juhudi zao za kusikiliza matangazo yetu, ni matumaini yetu kuwa tutadumisha mawasiliano na urafiki kati yetu.

Msikilizaji Jim Godfrey Mwanyama wa S.L.P 1097 Wundanyi Taita nchini Kenya ameanza kwa salamu kutoka kwake na kwa mashabiki wenzake waliopo huko Kenya, na kutoa pongezi nyingi kwa vipindi ambavyo vinarushwa kupitia idhaa ya kiswahili ya KBC. Anasema wanashukuru sana kwa matangazo hayo kwani yanawafahamisha mengi kutoka China na hata kutoka katika sehemu nyingine za dunia ikiwemo Afrika. Anaomba tuendelee vizuri na kazi hiyo, ili tuweze kuwapasha habari vizuri wakati wa michezo ya Olimpiki.

Msikilizaji wetu Bramwel Sirali wa S.l.P 1375 Kitale nchini Kenya, anaanza barua yake kwa kutujulisha kuwa wiki mbili zilizopita alipokea barua kwa furaha sana kutoka CRI. Pamoja na jarida hilo pia kulikuwa na Jarida la kingereza alilotumiwa la "China Today" ambalo anasema hadhani kama anaweza kulipata kutoka sehemu nyingine zaidi ya China kwenyewe, kweli huu ni upendo wa wa radio China Kimataifa kwa wasikilizaji wake. Anasema kupata jarida hilo linalohusu Hong Kong toleo la 56 namba 7 kwake ilikuwa kama ni kukutana marafiki wa zamani, kwani zamani aliwahi kuwasiliana na Radio moja ya Hong Kong, na aliburudishwa sana na wimbo mmoja kutoka Hong Kong. Mbali na hayo aliweza kujifunza mengi kuhusu Hong Kong kutokana na mawasiliano hayo. Anamaliza barua yake kwa kutoa shukurani sana kwa matokeo ya chemsha bongo ya "Sichuan Maskani ya panda" pamoja na zawadi nyingine alizopata ikiwemo jarida. Pendekezo lake ni kuwa kukiwa na uwezo wa kifedha basi angependa akumbukwe kwa kupewa cheti cha ushiriki wa chemsha bongo hiyo.

Msikilizaji wetu Daniel Ngoya wa S.L.P 172 Lwanda Bungoma nchini Kenya ametuandikia barua akisema ni matumani yake kuwa wasikilizaji wenzake na wafanya kazi wa Radio China Kimataifa tunaendelea vizuri. Anasema huko Lwanda wanaburidika na kuelimika na matangazo ya idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa. Aanasema alifurahi sana alipopata maswali kuhusu maandalizi ya michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008, na kwa sasa anafikiria kuhusu Michezo ya Olimpiki ya Beijing itakavyokuwa kuanzia talehe 8 hadi 24 mwezi wa nane. Sasa anaamini kuwa methali isemayo "mchumia juani hulia kivulini", na anamatumaini kuwa atakuwa mmoja wa washindi na kubahatika kuja kuangalia michezo ya Olimpiki. Mwisho anamalizia barua yake kwa kuomba kutumiwa majarida na zawadi kemkem zinazohusu michezo ya Olimpiki.

Na kwenye barua yake nyingine Bw Daniel Ngoya anasema anashukuru sana kwa barua aliyotumiwa, na anaendelea kuwa mvumilivu kusubiri majibu ya chemsha bongo. Kwenye barua yake pia anaomba kukumbusha kuwa tusimsahau kwa vizawadi, na pia anapenda kuwasalimu Ayub Sharif Mutanda, Bw John Ngoya, Mama yake Sarah Ngoya, Peter Simiyu na familia yake, Bw.Charles Jumah, Vitalis wasilwa, Ruth Nyongesa, Eliza wanyonyi, na Magrina nangeso wote wakiwa Lwanda.

Msikilizaji wetu mwingine Nyongesa J. Amos anayetunziwa baruza na Ayub Mutanda S.L.P 3479 Kitale nchini Kenya, anasema anaipongeaza Radio China Kimataifa kwa kazi zake za kila siku, anasema anafahamu kuwa vipindi na matangazo yanayorushwa kila siku si kazi rahisi. Bw.Amos ansema michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008 ipo moyoni mwake, ni matumatarajio yake kuwa michezo itafanikiwa na kuwa ya kipekee duniani. Pia angependa sana michezo ya olimpiki ihusishe mchezo wa raga au Rugby kwani ni mmoja kati ya michezo bora. Mwisho anaomba angalau waafrika kadhaa wajumuike au wafadhiliwe na CRI kwenda kushuhulia michezo ya Olimpiki na kwa wale watakaokosa uwezo, anaomba michezo ionyeshwe katika mtandao ili nao waweze kunufaika kutazama.

Na msikilizaji wetu mwingine Bw Nyamoge N. Ryoba wa S.L.P 71 Tarime, Mara nchini Tanzania, anaanza barua yake kwa kutoa salaam za dhati kwa wafanyakazi wote wa CRI, anasema yeye ni mzima na anaomba Radio China Kimataifa iendelee na vipindi vyake kwa sababu vipindi vinavutia sana katika bara zima la Afrika, na kwa kule Tanzania inawapa mambo mazuri sana kiasi kwamba kama angekuwa na uwezo mambo mengine angeyafuata nchini China kujionea yeye mwenyewe.

Bw. Ryoba pia anapendekeza kuwa CRI itangaze habari nyingi mpya za Afrika. Kinachomfanya aseme hivi ni kuwa idhaa za nyingine za Kiswahili huwa zina vipindi vingi vinavyohusu mambo ya Afrika, kwa hiyo aona ni vizuri kama tutaongeza vipindi vinavyohusu mambo ya Afrika. Na kuhusu Chemsha bongo mskilizaji wetu huyu anasema, kutokana na alivyojibu maswali ana matumaini kuwa atakuwa mshindi, na endapo kama mtu atashida kidogo basi anashauri apewe zawadi kidogo ili wasikilizaji wengine waweze kushuhudia kuwa kumbe wanachama wa klabu za wasikilizaji wanafahamu kitu wanachofuatilia ili pia watu wengine wawee kujiunga. Anamalizia kwa kuomba CRI iimarishe vipindi vizuri zadi, kwa mfano taarifa ya habari, habari za michezo na muziki wa kuvutia.

Wasikilizaji wapendwa tunapenda mufahamu kuwa si jambo rahisi kwa wasikilizaji wote kualikwa kushuhudia michezo ya Olimpiki ya Beijing, japo kuwa tungependa kufanya hivyo lakini raslimali zilizopo haizotosha kuwafanya wasikilizaji wetu wengi wasafiri kutoka huko waliko, na kuhakikishiwa malazi, chakula, usafiri na usalama wakati wa michezo ya Olimpiki. Pia mkumbuke kuwa CRI ina idhaa nyingi si rahisi kwa kila idhaa kuwaalika wasikilizaji wake waje Beijing kushughudia michezo hiyo, kwani Radio China Kimataifa ni radio ya serikali, bajeti ya radio ni yenye kikomo, ndio maana tumetoa shindano la chemsha bongo, ili walau kuonesha kuwa tunapenda baadhi ya wasikilizaji wetu wajumuike nasi kwenye michezo ya Olimpiki, lakini uwezo wetu ni wenye ukomo.