Maonesho ya magari ya kimataifa ya Beijing ya mwaka 2008 yalimalizika hivi karibuni, maonesho hayo yamefanyika kwa awamu 10 kila baada ya miaka miwili. Makampuni makubwa ya magari ya kimataifa, makampuni ya vipuri vya magari na makampuni maarufu ya magari ya China yalionesha bidhaa na teknolojia mpya kwenye maonesho hayo. Ikilinganishwa na awamu zilizopita, magari ya chapa zenye hakimiliki ya ubunifu ya China yamekuwa kivutio kwenye maonesho ya awamu hii.
Kwenye maonesho hayo, makampuni ya magari ya China kwa jumla yalionesha aina 50 za magari mapya yenye hakimiliki ya ubunifu ya China, ambazo zinawakilisha maendeleo yaliyopatikana katika uwezo wa uvumbuzi wa sekta ya utengenezaji wa magari ya China. Kwa mfano kampuni ya magari ya Dongfeng ya China ilionesha gari la kwanza la aina ya hatchback linalotumia teknolojia ya turbo; kampuni ya magari ya Chery ilionesha aina 5 za magari yenye msukumo mdogo (automobile with small output volume), baada ya marekebisho ya teknolojia magari ya aina hizo yamefikia kiwango cha juu cha usalama. Mbali na hayo, kampuni ya magari ya BYD na kampuni ya magari ya Jianghuai yote yalitoa aina mpya za magari. Kuhusu hali hiyo, naibu mkurugenzi wa shirikisho la viwanda vya magari la China Bw. Dong Yang alisema:
"kila kampuni imetoa aina mpya za magari yenye hakimiliki, na kila aina, magari makubwa au madogo, yote ni magari mapya. Hali hii inaonesha ustawi wa viwanda vya magari."
Katika hali ambayo mtizamo wa kuhifadhi mazingira na kubana matumizi ya nishati na kupunguza utoaji wa uchafuzi umeenezwa kote duniani, makampuni mengi ya magari ya China yameanza kuweka mkazo kwenye matumizi ya teknolojia ya nishati safi katika sekta ya utengenezaji magari. Kwenye maonesho hayo, kampuni ya magari ya BYD ilionesha gari la aina ya F6 ambalo ni gari la kwanza linaloendehwa kwa betri yenye chuma nchini China. Mfanyakazi wa kikanda cha kampuni ya BYD kwenye maonesho hayo Bw. Wang Dawei alisema:
"mifumo yote ya gari hilo inasukumwa kwa betri yenye chuma, hivyo kinadharia gari hilo halitoi hewa chafu."
Bw. Wang alisema, betri za nishati ya kemikali za alkaline manganese dioxide na Nickel-Hydrogen zinazotumika sasa haziwezi kukidhi mahitaji ya magari yanayohitaji umeme mwingi, lakini betri za chuma zinaweza kutoa umeme mwingi mara 3 hadi 10 kuliko ule wa betri za kawaida, ambazo zinafaa zaidi kutumiwa kwa ajili ya magari. Ikilinganishwa na betri za Lithium ambazo pia zinaweza kutoa umeme mwingi, betri hizo za uchuma zina gharama za chini zaidi. Aidha, kutokana na kuwepo kwa raslimali nyingi ya madini ya chuma ardhini, betri zenye chuma hazileti uchafuzi kwa mazingira wala hazina haja kurudishwa au kushghulikiwa baada ya kutumika. Sifa hizo zimeyafanya magari yanayotumia betri zenye chuma yawe na nguvu kubwa ya ushindani, kampuni ya BYD imesema, magari ya aina hiyo mpya yanatarajiwa kutolewa sokoni mwaka huu.
Mbali na kampuni ya BYD, kampuni ya Chery pia imetoa aina mpya za magari yanayosaidia uhifadhi wa mazingira, ambayo yote zinatumia mafuta ya dizeli au nishati mseto; kampuni ya Chang'an ilionesha aina mpya za magari yanayotumia nishati mseto, na kampuni ya Geely ilionesha magari yanayotumia nishati mpya ikiwemo methanol. Naibu katibu mkuu wa shirikisho la uhandisi wa magari la China Bw. Fu Yuwu alisema, kutokana na maendeleo ya miaka mingi, teknolojia za makampuni ya kutengeneza magari ya yanasonga mbele katika matumizi ya teknoloji za kubana matumizi ya nishati na kuhifadhi mazingira. Bw. Fu Yuwu alisema:
"maendeleo ya magari yanayotumia nishati mpya ni suala linalofuatiliwa kwa pamoja na viwanda vya magari vya nchi mbalimbali, kwa upande huo, China haiko nyuma sana na kiwango cha kimataifa."
Katika muda mrefu uliopita, magari yaliyotengenezwa na makampuni ya China yalilenga soko la kiwango cha kati na cha chini, na kujipatia soko kubwa zaidi kwa bei nafuu. Lakini kwenye maonesho ya magari ya kimataifa ya mwaka 2008, makampuni mengi ya China yametoa magari ya kiwango cha juu na kugombea soko na makampuni ya nchi za nje na ya ubia ya China na nchi za nje.
Kampuni ya magari ya Hongqi chini ya kampuni ya FAW ya China ilitoa aina mpya ya gari la SUV. Gari hilo imefikia kiwango cha juu cha kimataifa, aina hiyo ya magari ina mfumo wa kuwasha injini bila ufunguo, kioo kikubwa, viti vinavyoweza kurekebishwa kwa pande nyingi, kiyoyozi kinachojiendesha katika mstari wa mbele na mstari wa nyuma, pamoja na mfumo wa kisasa wa breki na zana za kisasa za usalama.
Mbali na magari mazima, makampuni ya magari pia yalionesha vipuri vipya vya magari kwenye maonesho hayo. Kwa mfano wa injini, kampuni ya FAW ilimaliza utafiti na usanifu wa injini kutoka ujazo wa lita moja hadi lita 13, ambazo zinaweza kukidhi mahitaji ya magari ya aina zote. Kampuni ya magari ya Ukuta Mkuu ya China ilionesha aina mpya ya gia boksi iliyosanifiwa kwa kutumia software ya kisasa. Gia boksi ya aina hiyo si kama tu inainua ufanisi wa kubadilisha nguvu ya msukumo, bali pia inahakikisha utulivu wa kubadilisha gia na kupunguza kelele.
Wachambuzi wanaona kuwa, kutoka kuunda magari kwa kutumia vipuri vilivyoagizwa kutoka nchi za nje hadi kutengeneza magari mazima yaliyosanifiwa na wachina wenyewe, na kutoka magari ya kiwango cha chini hadi ya kiwango ya juu, hadi magari ya kisasa yanayotumia nishati safi, sekta ya utengenezaji wa magari ya China imepata maendeleo makubwa. Katika siku za baadaye, pamoja na uchumi, sayansi na teknolojia za China kuendelea kuimarika, shughuli hizo zitaendelea kwa kasi zaidi.
|