Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-05-08 15:47:27    
Beijing yaanzisha shughuli nyingi za utamaduni kukaribisha Michezo ya Olimpiki

cri

Tarehe 8 Agosti mwaka huu Michezo ya Olimpiki ya 29 itazunduliwa mjini Beijing. Ili kuikaribisha michezo hiyo Kamati ya Maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing iliamua kufanya shughuli nyingi za utamaduni mjini Beijing kuanzia mwezi Machi hadi Septemba. Wasanii zaidi ya elfu 20 kutoka nchi zaidi ya 80 watafanya maonesho zaidi ya 260 ya michezo ya sanaa, na kati ya hayo maonesho 160 yatakuwa makubwa. Kwa madirio watazamaji watafikia milioni nne.

Kuunganisha michezo na shughuli za utamaduni ni desturi ya jadi ya Michezo ya Olimpiki. Kwa mujibu wa katiba ya Olimpiki, Michezo ya Olimpiki inafanyika kwa sehemu tatu, yaani michezo, shughuli za utamaduni na elimu. Kwa kufanya shughuli za utamaduni Beijing ikiwa ni mwenyeji wa michezo hiyo, itatangaza utamaduni wa nchi yake na kuingiza utamaduni kutoka nchi za nje na kustawisha maingiliano ya kiutamaduni ya kimataifa. Shughuli za utamaduni wakati Michezo ya Olimpiki ilipofanyika Sydney mwaka 2000 na shughuli za utamaduni wakati michezo hiyo ilipofanyika Athens mwaka 2004, zote zilikuwa na mafanikio. Hivi sasa wasanii wa China wamepiga mbiu ya kuanzisha shughuli hizo za utamaduni hapa Beijing wakichangia ufanisi wa michezo hiyo.

Shughuli za utamaduni kwenye Michezo ya Olimpiki ya Beijing zina sehemu mbili, moja ni sehemu ya utamaduni wa nchini China na nyingine ni sehemu ya utamaduni wa nchi za nje. Sehemu ya utamaduni wa nchini China ilianzishwa mwezi uliopita, na sehemu ya utamaduni wa nchi za nje itaanzishwa tarehe 23 Juni. Maonesho mengi ya michezo ya sanaa na ya utamaduni, mihadhara na mabaraza yatawaletea watu wa nchini na wa nchi za nje mazingira mazuri ya kiutamaduni.

Ofisa wa Wizara ya Utamaduni ya China Bw. Yang Xong alieleza kwamba wasanii wa makundi mbalimbali nchini China wana hamu kubwa ya kushiriki kwenye maonesho yao kwa kuwasilisha orodha ya michezo yao. Baada ya kuchagua, michezo itakayooneshwa ni 150, na kati ya michezo hiyo licha ya kuwepo kwa opera ya Kibeijing, pia kutakuwa na opera za aina mbalimbali za kisehemu, na licha kuwepo kwa muziki wa simfoni, pia kutakuwa na opera ya muziki na michezo ya kuigiza kwa kuimbwa, na makabila zaidi ya 50 ya China yataonesha utamaduni wao wa kipekee. Bw. Yang Xiong alisema ili kuwawezesha watu wengi zaidi kutazama michezo ya sanaa na maonesho hayo serikali imepunguza bei za tikiti kwa hatua za kulipa kodi ya matumizi ya majumba na kuwapa wasanii marupurupu. Yang Xong alisema,

"Maonesho hayo ya michezo ya sanaa yana sifa tatu. Moja ni upana wake, maana makundi zaidi ya 100 kutoka sehemu mbalimbali nchini China yataonesha michezo ya sanaa zaidi ya 150 kwa mara zaidi ya 600, kila mkoa una makundi yake yatakayoshiriki kwenye maonesho hayo. Pili kiwango cha sanaa cha michezo ya sanaa ni cha juu. Tatu, watu wengi wanaweza kunufaika kutokana na bei ya chini ya tikti, kwani serikali inataka bei ya tikiti iwe kati ya Yuan 50 hadi 280, na serikali itawapatia tikiti baadhi ya watu wakiwemo wajenzi wa majumba ya michezo ya Olimpiki."

Kuanzia tarehe 10 Juni opera za kisehemu 12 kutoka mikoa ya Fujian, Sichuan, Anhui, Guandong, Tibet na mikoa mingine zitaoneshwa mjini Beijing. Mkurugenzi wa kituo cha kuhifadhi utamaduni usioonekana Bw. Zhang Qingshan alisema,

"Michezo hiyo ya sanaa inavutia kutokana na utamaduni wa kipekee wa kikabila, na kati ya michezo hiyo mingi ni ya utamadunu wa jadi usioonekana ikiwa ni pamoja na ngoma na michezo ya vikaragosi, tumewaalika wasanii wazee wanaorithisha utamaduni huo kuonesha michezo yao ya ajabu."

Licha ya kuonesha utamaduni wa nchini, utamaduni kutoka nchi za nje pia utaoneshwa. Makundi ya wasanii kutoka Hispenia, Marekani, Italia, Russia yataonesha michezo yao ya sanaa. Meneja mkuu wa Kampuni ya Maingiliano ya Kimataifa ya Michezo ya Sanaa ya China Bw. Zhang Yu alisema, wamefanya maandalizi ya michezo hiyo ya sanaa kwa mwaka zaidi ya mmoja, na michezo hiyo inawakilisha aina nyingi za utamaduni duniani. Alisema,

"Michezo ya Olimpiki ni ya dunia nzima, tumekusanya maonesho michezo ya sanaa tofauti katika maonesho matano makubwa ya nyimbo na dansi, maonesho hayo ni ya Asia, Afrika, Latin Amerika, nchi za Kiarabu na mchanganyiko wa maonesho ya michezo ya sanaa ya sehemu hizo. Kwa kuzingatia uzoefu wa nchi zilizowahi kuandaa michezo ya Olimpiki tumeshirikisha makundi mengi hodari ya wasanii na kufanya maonesho hayo kama ni tamasha kubwa la kimataifa la utamaduni."

Balozi wa Ugiriki nchini China Bw. Michael Cambanis alisema, tarehe 23 Juni maonesho ya michezo ya sanaa ya nchi yake yanayoitwa "Salaam kutoka Olimpia" yatafanyika katika Ukumbi Mkuu wa Umma mjini Beijing, wasanii wataonesha sherehe ya kuwasha mto mtakatifu na opera ya jadi.

"Ugiriki ikiwa nchi yenye heshima katika Michezo ya Olimpiki, maonesho ya michezo yake ya sanaa sio tu ina maana ya kuonesha utamaduni wake bali pia inaonesha uhusiano mzuri kati yake na China, kwa hiyo Wizara ya Utamaduni ya Ugiriki inazingatia sana michezo itakayooneshwa mjini Beijing na maonesho ya michezo hiyo ya sanaa yote inaoneshwa na wasanii wakubwa wa nchi yetu."

Msaidizi wa waziri wa utamaduni wa China Bw. Ding Wei alisema, shughuli za utamaduni kwa ajili ya kukaribisha Michezo ya Olimpiki ya Beijing ni kubwa na zenye kiwango cha juu na zitakuwa na muda mrefu zaidi katika shughuli za utamaduni mwaka huu mjini Beijing, shughuli hizo licha ya kuwa na mada itakayotakiwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki yaani "amani, urafiki na maendeleo", pia zinaonesha matumaini mema ya "dunia moja na ndoto moja". Alisema,

"Kuwaalika wasanii elfu 20 wakusanyike mjini Beijing kutoka sehemu mbalimbali duniani na kuonesha maendeleo makubwa waliyopata katika utamaduni wao kunadhihirisha kuwa serikali ya China inatetea, inaheshimu na inakaribisha aina tofauti za utamaduni duniani."

Idhaa ya kiswahili 2008-05-08