Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-05-12 16:31:57    
Twende kuwaangalia korongo katika majira ya baridi

cri

Kwenye mkoa wa Guizhou, kusini magharibi mwa China kuna ardhi oevu iliyoko kwenye uwanda wa juu, wakazi wa huko wanaiita "bahari ya majani". Kila ikifika siku za baridi, ndege zaidi ya laki moja hufika huko kutoka sehemu ya kaskazini ili kukwepa baridi kali ya maskani yao. Korongo wenye shingo nyeusi ni ndege adimu wa ngazi ya kwanza wanaolindwa na taifa.

"Bahari ya majani" iko kwenye wilaya inayojiendesha ya makabila ya wayi na wahui, sehemu ya kusini magharibi ya China, sehemu hiyo ya ardhi oevu ni ya mfumo wa kutegemeana kwa viumbe iliyoko kwenye uwanda wa juu, na ni moja kati ya maziwa matatu makubwa yenye maji baridi kwenye uwanda wa juu. Kuna viumbe wengi wa majini na kuna mwangaza mwingi wa jua kwenye "bahari ya majani", hivyo kila mwaka kuna ndege wengi wanaoishi huko katika majira baridi. Takwimu zinaonesha kuwa, ndege wanaoishi huko katika majira baridi wanafikia aina 203, na idadi yao ni zaidi ya laki 1, hivyo "bahari ya majani" inasifiwa kuwa ni "bahari ya majani na mahali penye furaha kwa ndege".

Mwanzoni mwa mwaka huu, Bw. Chen Jian, mshabiki wa wanyama alifika kwenye "bahari ya majani" ili kuangalia ndege. Alisema,

"Tulipanda mashua moja ndogo, tulikwenda sehemu ya ndani ya "bahari ya majani". "Bahari ya majani" ni ziwa lenye eneo la kilomita 25 za mraba, ingawa halina mawimbi makubwa kama ya baharini, lakini ziwa hilo ni kubwa na maridadi sana."

Mandhari nzuri iliyo kama picha, ilimvutia sana Bw. Chen Jian, na kumfanya asitake kuondoka huko, lakini hakusahau lengo lake muhimu la safari yake, yaani kuangalia Korongo wenye shingo nyeusi. Bw. Chen Jian alisema, korongo wenye shingo nyeusi, ambao ni ndege adimu pekee wanaoishi nchini China, ni ndege adimu waliochelewa zaidi kugunduliwa, na pia ni aina ya pekee ya ndege adimu wanaoishi kwenye uwanda wa juu. Korongo wenye shingo nyeusi walipata jina hilo kutokana na kuota manyoya mengi meusi yanayong'aa kwenye shingo zao maridadi. Hivi sasa, sehemu kubwa ya korongo wa aina hiyo ambao wamebaki wachache humu duniani, wako kwenye uwanda wa juu wa Qinghai na Tibet, uwanda wa juu wa Yunnan na Guizhou na sehemu ya kaskazini ya mkoa wa Sichuan. Wakati alipokuwa akisema, milio ya ndege kutoka kwenye ziwa ilimvutia Bw. Chen.

Bw. Chen alisema, hii ni milio ya kipekee ya korongo wenye shingo nyeusi. Kweli, ukiangalia upande ilikotoka milio ya ndege, unaweza kuona korongo kadhaa wakitembea taratibu kwa madaha, tena mara kwa mara wanainamisha shingo kutafuta chakula kwenye maji na majani yanayoota kwenye kando ya ziwa. Wanatembea kwenye kando ya ziwa kama mabwenyenye, tena wanaangalia kila mahali mara kwa mara. Bw. Chen alisema,

"Sasa nimeona korongo wenye shingo nyeusi watano au sita hivi, tulikuwa tukiwasogelea. Niliwaona Korongo wawili wakipumzika kwenye shamba la mpunga, ndege hao ni maridadi sana, vichwa vyeusi na miili myeupe, hasa manyoya yao ya rangi nyeusi yanapendeza sana, wanaishi maisha ya furaha na uhuru."

Habari zinasema tokea mwezi Januari, korongo wenye shingo nyeusi waliofika kuishi katika majira ya baridi kwenye "bahari ya majani" ya mkoa wa Guizhou kutoka uwanda wa juu wa Qinghai na Tibet, kwa mara ya kwanza wamezidi 1,200, sasa "bahari ya majani" imekuwa ni sehemu muhimu sana ya kuishi katika majira ya baridi kwa korongo wenye shingo nyeusi wa nchini China. Hali hii inatokana na sera za hifadhi zinazotekelezwa na serikali ya huko. Ofisa wa idara ya hifadhi ya mazingira ya wilaya ya Wining, Bw. Wang Liang alisema,

"Tunatekeleza sera kadhaa: ya kwanza, kuwafahamisha wakazi wa huko kuhusu umuhimu wa "bahari ya majani" na kuwalinda korongo wenye shingo nyeusi; ya pili, serikali inaweka chakula kingi zaidi kwa korongo wenye shingo nyeusi na kutatua tatizo la ukosefu wa chakula la korongo wa aina hiyo; na la tatu, kuongeza adhabu kwa wahalifu wanaowakamata na kuwaua Korongo wenye shingo nyeusi. Tunaweza kusema kuwa katika miaka ya karibuni, hakujatokea watu wanaowawinda, na tumehakikisha nafasi ya kuishi na kuzaliana kwa korongo wenye shingo nyeusi."

Kwa upande mwingine, serikali ya huko inazidisha nguvu za kuwafahamisha wakazi kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira, na mwamko wa kuishi katika hali ya kupatana kati ya binadamu na mazingira ya asili, na kati ya binadamu na ndege. Sasa wakulima wa sehemu hiyo wamebadilisha mawazo, wanatilia maanani kulinda ndege hao, na baadhi yao ambao hapo zamani hawawapendi ndege, sasa wamejitolea kuwalisha. Mwanakijiji Bw. Jiang Fuhai alisema,

"Miaka michache iliyopita tuliwachukia ndege hao, ambao mara kwa mara walikuwa wanakuja kula mazao yetu. Baada ya serikali kutufahamisha umuhimu wa kuwahifadhi ndege, tumefahamu kuwa korongo wenye shingo nyeusi ni ndege adimu sana. Tunafikiri, tuwaache wale mazao kidogo, hivyo hatuwafukuzi tena. Baadhi ya nyakati, tukitoka mashambani, wanatufuata nyuma, hawatuogopi tena. Hali ya hewa ilikuwa baridi sana mwanzoni mwa mwaka huu, korongo wenye shingo nyeusi walikosa chakula, wakafika kwenye mashamba yetu, tulimwaga kidogo mahindi ya kuwalisha, na tena tuliwawekea maji ya kunywa. Ninaona nikiwa mwanakijiji ninapaswa kufanya hivyo."

Habari zinasema katika majira ya baridi ya mwaka huu, mkoa wa Guizhou ulipatwa na maafa ya baridi kali na theluji, wakazi wa huko kila siku walitoa wastani wa kilo 1,500 za mahindi kuwalisha korongo wenye shingo nyeusi, kwa jumla tulitoa zaidi ya tani 30 za chakula. Kutokana na juhudi za wakazi wa huko, sasa idadi ya korongo wenye shingo nyeusi inaongezeka karibu kwa 4% kwa mwaka.

Shule za sekondari na msingi za wilaya ya Wining zimeweka elimu ya hifadhi ya mazingira katika masomo ya wanafunzi. Wito wa kuwaelimisha watu kuhifadhi mazingira unatekelezwa kwa kuanzia kuwaelimisha watoto katika wilaya hiyo. Mwanafunzi Tang Jiao wa shule ya mwingi ya kwanza ya wilaya ya Wining, alisema, kulinda ndege adimu ni azma ya watu wote wa familia yao.

"Shughuli moja iliyoanzishwa shuleni kuhusu uhifadhi wa mazingira, ilinifanya nitambue umuhimu wa kuhifadhi mazingira, kulinda ndege na wanyama, hata kama hao siyo wanyama wa ngazi ya kwanza wanaolindwa na taifa. Tunapaswa kulinda viumbe vyote."

Hivi sasa, mkoa wa Guizhou unaimarisha hifadhi kwa "bahari ya majani", mazingira ya kuishi kwa viumbe yameboreshwa kwa udhahiri. Hivi sasa idadi ya ndege wanaokwenda huko kuishi katika majira baridi kila mwaka inazidi laki 1.

Idhaa ya kiswahili 2008-05-12