Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-05-13 17:50:28    
Kilimo cha mazao ya kitropiki mkoani Hainan

cri

Kutokana na uzalishaji mkubwa wa mboga na matunda, mkoa wa Hainan umasifiwa kuwa ni mkoa unaozalisha mboga na matunda kwa wingi nchini China. Mazao yanayozalishwa mkoani humo si kama tu yanauzwa katika miji zaidi ya 100 nchini China, bali pia yanauzwa katika nchi na sehemu zaidi ya 20 duniani ikiwemo Marekani, Ulaya, Russia, Japan na nchi za Asia ya Kusini Mashariki. Mwaka 2007 mazao ya kilimo ya mkoa huo yaliyouzwa katika nchi za nje yalikuwa karibu tani milioni 4.5, na thamani ya uuzaji wa mazao hayo ilikuwa ni zaidi ya dola za kimarekani milioni 400. Hivi sasa kuendeleza kilimo cha mazao ya kitropiki kumekuwa ni moja kati ya mikakati muhimu ya kuhimiza maendeleo ya uchumi wa mkoa huo.

Mwishoni mwa karne iliyopita, Bw. Guo Zhiyao kutoka mkoa wa Henan alifanya uchunguzi mbalimbali kuhusu masoko ili kufanya biashara. Aligundua kuwa mboga zinazozalishwa mkoani Hainan zina sifa nzuri, na zinanunuliwa vizuri katika masoko ya sehemu za ndani za China. Hivyo aliamua kuanzisha shughuli zake mkoani humo. Alisema,

"Nilipofanya uchunguzi kuhusu masoko ya mazao ya kilimo ya sehemu za ndani za China kabla ya kuja hapa Hainan, niligundua kuwa kutokana na mwangaza wa jua wa kutosha na hali ya hewa ya fufutende katika majira ya baridi, sifa ya mboga zinazozalishwa mkoani Hainan ni nzuri, hivyo bei za mboga hizo zikiwemo pilipili na mabiringani ni kubwa kwa asilimia 30 kuliko bei za mboga zinazozalishwa mkoani Guangdong kwa asilimia 30. Niliamua kuja hapa kuwekeza baada ya kutambua sifa ya Hainan."

Mwaka 1999, Bw. Guo Zhiyao alianzisha kampuni ya maendeleo ya kilimo mkoani Hainan. Anawaongoza wakulima kupanda mazao husika kwa mujibu wa mahitaji ya mazao kwenye masoko ya sehemu za ndani za China, na shughuli zake zinapata maendeleo siku hadi siku. Hivi sasa eneo la kituo cha uzalishaji cha kampuni yake ni karibu hekta 200. Licha ya kuzalisha mboga katika majira ya baridi, pia wanapanda matunda mbalimbali ya kitropiki. Mazao yanayozalishwa na kampuni yake yanauzwa katika nchi mbalimbali zikiwemo Ufaransa, Ujerumani na Canada.

Msemaji wa idara ya kilimo ya mkoa wa Hainan Bw. Chen Yongwang alisema kuna makampuni mengi yanayoshughulikia uzalishaji wa mazao ya kilimo mkoani Hainan kama kampuni ya Bw Guo Zhiyao. Mengi kati ya makampuni hayo yalianzishwa katika miaka ya tisini ya karne iliyopita, ambapo serikali ya mkoa huo ilifanya uamuzi wa kuendeleza kilimo cha mazao ya kitropiki, na kuwahimiza wakulima kupanda mboga na matunda katika majira ya baridi, alisema,

"Baada ya mkoa wa Hainan kuanzishwa mwaka 1988, serikali ilitambua kuwa kutokana na kuwa na idadi ndogo ya watu, masoko ya mkoa wetu ni madogo, hivyo tulizingatia njia ya kuendeleza uzalishaji wa mazao ya kilimo katika majira ya baridi. Wakati huo uuzaji wa mazao ya kilimo masokoni ni mdogo katika majira ya baridi, mabanda ya kupanda mazao hayajatumiwa kwa wingi sehemu za kaskazini mwa China, na utoaji wa mazao haukuweza kukidhi mahitaji masokoni. Kutokana na hali ya hewa ya fufutende katika majira ya baridi, mwangaza wa jua wa kutosha na mvua nyingi mkoani humo, tulitoa mpango wa mageuzi ya utaratibu wa kupanda mazao, na kuendeleza kilimo katika majira ya baridi. Hatua hiyo ikiwa ni njia muhimu ya kuongeza mapato ya wakulima imewanufaisha sana wakulima."

Mwanzoni kutokana na ongezeko kubwa la watu wanaopanda mazao ya kilimo, matatizo mbalimbali yalitokea. Kutokana na kutokuwepo kwa usimamizi wa jumla, sifa ya mazao ilitofautiana, na bei za mazao hayo ilikuwa ya chini. Tena maafa ya wadudu waharibifu yakitokea, mkulima mmoja hakuwa na uwezo wa kukabiliana nayo. Ili kutatua matatizo hayo, mkoa wa Hainan ulianzisha jumuiya za ushirikiano za kilimo. Wilaya ya Chengmai ambayo ni moja kati ya wilaya 10 zenye maendeleo makubwa zaidi ya kilimo nchini China ilianzisha jumuiya za ushirikiano za kilimo mapema zaidi. Makampuni husika yanaagiza, kununua, kutengeneza na kuuza mazao ya kilimo, na kutoa mafunzo ya ufundi wa kilimo kwa wakulima.

Mkuu wa shirikisho la uchukuzi na uuzaji wa matunda na mboga la wilaya ya Chengmai Bw. Wang Meizhi alisema,

"Tunawapatia wakulima mbegu, na kununua mazao yao. Tunawaongoza wakulima kupanda mazao, kuwafundisha njia ya kusimamia mashamba wakati hali ya hewa inapokuwa baridi au mvua inaponyesha mvua. Tunawapatia ufundi mbalimbali, kwa sababu wengi wao hawana ufundi. Tunawaelekeza wakati wa kupanda na kuvuna mazao yao, na wapande mazao gani ili kukidhi mahitaji ya masoko."

Hivi sasa zaidi ya asilimia 90 ya matunda na mboga zinazozalishwa mkoani humo katika majira ya baridi zinauzwa katika sehemu nyingine. Serikali ya wilaya ya Chengmai inaona kuwa, jumuiya za ushirikiano za kilimo zimefanya kazi kubwa. Mkurugenzi wa idara ya kilimo ya wilaya hiyo Bw. Wang Xirui alisema, serikali imeanza kutoa msaada wa kifedha ili kuhimiza maendeleo ya jumuiya hiyo, alisema,

"Tunapoendeleza upandaji wa mboga na matunda katika majira ya maridi, jumuiya ya ushirikiano ya kilimo inashughulikia kuwaelekeza wakulima kuhusu mazao ya kupanda na mahali pa kuyauza, hivyo kilimo cha hapa kimepata maendeleo mazuri. Kuanzia mwaka jana, serikali ya wilaya inatenga yuan 3000 kila mwezi ili kuiunga mkono jumuiya ya ushirikiano za kilimo, na kama maafa ya kimaumbile yakitokea, serikali pia inatenga fedha za msaada. Mwaka huu hali ya hewa ni baridi, uchukuzi na uuzaji wa mboga na matunda unakabiliwa na matatizo, na serikali imetenga yuan milioni 2 ili kuisaidia."

Mkuu wa wilaya ya Chengmai Bw. Yang Sitang alisema, katikati ya miaka ya 90 ya karne iliyopita, baadhi ya nchi zilianza kuweka vigezo vya kilimo, hivyo walianza kupanda mazao yasiyo na uchafuzi.

Wakati huo huo, serikali ya mkoa wa Hainan inafanya juhudi kubwa kuendeleza huduma za sayansi na teknolojia ya kilimo, na kuanzisha vituo vya huduma za ufundi wa kilimo katika sehemu mbalimbali.