Katika mji wa Erlianhaote wa mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani, mfanyabiashara wa Mongolia Bibi Dedbilig ni "mkwe" wa China, ambaye pia ni mtu maarufu kwenye shughuli za kibiashara kati ya China na Mongolia. Yeye anafanya juhudi za kuhimiza mawasiliano ya kiuchumi na kibiashara kati ya China na Mongolia, pia amewahi kuwaandikia maofisa wa serikali ya huko barua ya mapendekezo, ili kuendeleza soko la biashara ya mpakani la mji wa Erlianhaote. Bibi Dedbilig ana umri wa miaka 36. Alipokuwa na umri wa miaka 17, kutokana na mradi wa Mongolia wa kwenda kusoma nje ya nchi, alijifunza mambo kuhusu vyombo vya umeme vya viwandani katika Chuo Kikuu cha sayansi na teknolojia cha Shanghai, kilichopo mashariki mwa China. Lakini baada ya miaka miwili, Bibi Dedbilig alikumbwa na tatizo kubwa la kushindwa kulipa ada yake. Ili kuendelea na masomo nchini China, Bibi Dedbilig alianza kufanya kazi za vibarua.
"Usiku nilifanya kazi ya vibarua kwenye kiwanda kimoja kidogo mjini Shanghai, ambacho pia kilikuwa kinashughulikia vyombo vya umeme vya viwandani, ambapo nilifanya kazi ya kufunga swichi, na siku ya pili niliweza kupata Yuan 50."
Kwa kutegemea pesa alizochuma kutokana na kufanya kazi ya kibarua, Bibi Dedbilig alimaliza masomo yake bila matatizo. Mwaka 1992 alipohitimu masomo yake ndipo China ilipofanya mageuzi na kufungua mlango na kuingia katika kipindi kipya cha maendeleo, Bibi Dedbilig aliona nguvu ya maendeleo ya jamii ya China. Wakati huo, wanafunzi wengine wa Mongolia waliokuwa wanasoma nchini China pamoja na Bibi Dedbilig walirudi nchini Mongolia, lakini Bibi Dedbilig aliamua kubaki nchini China. Baadaye Bibi Dedbilig alikwenda mjini Wenzhou mkoani Zhejiang, mashariki mwa China. Alifanya kazi ya kibarua katika kiwanda cha swichi, na kila siku alipata Yuan zaidi ya 1,000. Bibi Dedbilig alifurahia kuchuma pesa, lakini pia aliona ugumu wa maisha. Alisema:
"Wakati ule niliishi kwenye nyumba ndogo, na hali ya hewa huko ilikuwa ya unyevunyevu. Hali ya hewa ilikuwa baridi, lakini nilitokwa na jasho jingi, na nilifanya kazi hiyo kwa miaka miwili katika hali hiyo mbaya."
Kutokana na juhudi zake, maisha ya Bibi Dedbilig nchini China yalikuwa yameanza kutulia. Anapenda sana nchi ya China, mvuto wa mazingira mazuri ya kimaumbile, mila na desturi pekee na nguvu kubwa ya maendeleo ya China unamfanya aipende China. Lakini Bibi Dedbilig aliyeondoka maskani yake alipokuwa na umri wa miaka 17, alikuwa anakumbuka maskani yake siku hadi siku. Hivyo Bibi Dedbilig alifikiria njia nzuri, yaani kwenda mji wa Erlianhaote, kaskazini mwa China.
Mji wa Erlianhaote uko kati ya mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani, ambao ni bandari pekee ya reli inayopakana na nchi ya Mongolia, pia ni sehemu muhimu ya usambazaji wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje na kuuzwa kwa nchi za nje kwa mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani na hata nchini China. Bibi Dedbilig aliona kuwa, kuishi katika mji huo ni mwafaka kabisa kwake. Alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, sababu ya kuchagua kwenda kujiendeleza katika mji wa Erlianhaote ni kwamba, ingawa hatarudi nchini Mongolia, lakini mji wa Erlianhaote ni karibu na Mongolia, anaweza kuwasiliana na nchi yake, na kutoa mchango kwa nchi yake.
Mwanzoni Bibi Dedbilig alitumia nguvu yake bora ya lugha kufanya ukalimani kwa wafanyabiashara wa China na Mongolia. Baadaye alifanya biashara mwenyewe kati ya nchi hizo mbili. Kadiri shughuli zake zinavyoendelea, Bibi Dedbilig alianzisha kampuni yake, na kushughulikia uagizaji wa madini kutoka nje na uuzaji wa madini kwa nchi za nje. Wakati huohuo alikutana na mchumba wake, kijana mmoja hodari wa China. Baadaye Bibi Dedbilig akawa "mkwe wa China", na kweli China imekuwa maskani yake ya pili.
Baada ya hapo, Bibi Dedbilig alifanya juhudi zaidi kwa ajili ya maendeleo ya pamoja ya nchi hizo mbili. Kutokana na kazi yake, viwanda na makampuni mengi ya China yameingia Mongolia kushughulikia ujenzi wa barabara, uendelezaji wa nyumba na utengenezaji wa vifaa vya ujenzi. Lakini kadiri kazi za kuhimiza mawasiliano ya kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizo mbili zinavyoendelezwa, Bibi Dedbilig pia aligundua baadhi ya matatizo yanayoathiri maendeleo ya soko la mji wa Erlianhaote. Alisema,
"Zamani wafanyabiashara wa Mongolia waliagiza bidhaa mbalimbali kutoka mji wa Erlianhaote. Lakini kuanzia mwaka jana hadi mwaka huu, asilimia 80 ya wafanyabiashara hao waliagiza bidhaa kutoka sehemu za ndani za China."
Hivyo kuanzia hapo, katika maisha na shughuli zake za kila siku, Bibi Dedbilig aliwauliza wafanyabiashara wa Mongolia tathmini yao kwa mazingira ya uchumi ya mji wa Erlianhaote, na kukusanya maoni yao kuhusu soko la mji wa Erlianhaote. Mwezi Aprili mwaka 2007, Bibi Dedbilig alimwandikia barua ofisa wa serikali ya mji wa Erlianhaote Bw. Zhang Guohua. Kwenye barua hiyo alijumuisha sababu za soko la mji wa Erlianhaote kushindwa kuwavutia wafanyabiashara wa Mongolia, na alitoa mapendekezo kuhusu namna ya kutatua matatizo hayo.
Mfanyabiashara wa kigeni kumwandikia barua ofisa wa serikali ya China, na kuzungumzia matatizo yaliyopo kwenye soko la China, jambo hili ni nadra kutokea kabla ya hapo, lakini hata Bibi Dedbilig hakutarajia kuwa Bw. Zhang Guohua aliyepata barua yake angetilia maanani sana hali aliyozungumzia, na kujadili matatizo hayo kwenye mkutano wa serikali ya mji wa Erlianhaote.
Kuhusu matatizo hayo yaliyotolewa na Bibi Dedbilig, Bw. Zhang Guohua alitoa agizo kuzitaka idara husika zitoe ufumbuzi, na kuchukua hatua zenye ufanisi, ili kupata uaminifu wa wafanyabiashara wa kigeni. Bw. Zhang Guohua pia alimwandikia E-mail Bibi Dedbilig, na kutaka kumwajiri Bibi Dedbilig kuwa msimamizi wa sifa za bidhaa za mji wa Erlianhaote. Bibi Dedbilig pia alifurahi sana kuwa serikali ya mji wa Erlianhaote inatilia maanani sana maoni yake.
Sasa shughuli za kampuni ya Bibi Dedbilig zimeenea nchini Russia, hivyo yeye husafiri kati ya nchi tatu za China, Mongolia na Russia. Mabinti zake mapacha wana umri wa miaka 11, na wanaelewa na kuunga mkono kazi za mama yao. Bibi Dedbilig alisema hivi sasa mume wake ambaye ni mchina anampenda, na mabinti zake wanamwelewa na kumuunga mkono, hivyo bila kujali ugumu wa kazi akiwa nje, akiwakumbuka wao anaona furaha. Na anafurahi sana kuyafanya maisha yake yawe na thamani katika taifa lake na maskani yake ya pili.
|