Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-05-26 21:16:40    
Matibabu ya kitibet nchini China yapata maendeleo makubwa

cri

Ikiwa ni sehemu muhimu ya matibabu ya jadi ya kichina, matibabu ya kitibet yamekuwa na historia ya zaidi ya miaka 2,300. Na sasa huduma za matibabu hayo zinatolewa kwenye kila tarafa kwenye mkoa unaojiendsha wa Tibet. Hivi sasa kwenye mkoa huo, kuna idara zinazohusika na hospitali kubwa zaidi ya 10 za matibabu ya kitibet, na maelfu ya watu wanajishughulisha na matibabu hayo.

Profesa Don Drup ni mkurugenzi wa taasisi ya utafiti wa sayansi na teknolojia ya matibabu ya kitibet ya mkoa wa Tibet, pia ni mmoja kati ya kikundi cha kwanza cha wanafunzi waliosomea kozi ya matibabu hayo kwenye vyuo vikuu tangu Tibet ilipokombolewa kwa njia ya amani miaka ya 50 ya karne iliyopita. Katika miaka 18 iliyopita, Bw. Don Drup aliendelea kufanya kazi zake zinazohusu matibabu hayo, na kila siku alitokea hapa na pale kuwatibu wagonjwa, kuwafundisha wanafunzi na kufanya utafiti. Hivi sasa jambo linalomfurahisha zaidi ni kuwa anaweza kuwafundisha wanafunzi wengi kwenye Chuo cha Udaktari wa Matibabu ya Kitibet cha Tibet, hivyo matibabu ya kitibet yataendelezwa na kustawi. Bw. Don Drup alisema,

"Zamani wanafunzi waliosoma kozi ya matibabu ya kitibet walikuwa zaidi ya 300 tu, lakini hivi sasa idadi ya wanafunzi hao imefikia zaidi ya 1,440, na matibabu hayo yatarithiwa vizuri."

Bw. Don Drup alifahamisha kuwa mabadiliko hayo makubwa yanatokana na uungaji mkono wa muda mrefu wa serikali ya China. China inatilia maanani sana matibabu ya kitibet, tangu itekelezwe sera ya mageuzi na ufunguaji mlango ianze kutekelezwa, serikali ya China kwa nyakati tofauti imetenga mamilioni ya Yuan ili kuzisaidia idara zinazohusika kufanya utafiti wa matibabu ya kitibet. Kabla ya Tibet kupata ukombozi mwaka 1959, mkoani kote Tibet kulikuwa na hospitali mbili za matibabu ya kitibet, na hospitali hizo hasa zilikuwa zinawahudumia makabaila na masufii wa ngazi ya juu, lakini sasa hali imebadilika sana, sasa kuna hospitali na zahanati nyingi mkoani Tibet, na huduma za matibabu ya kitibet zinatolewa kwa watibet wote.

Ili kuhimiza maendeleo ya dawa na matibabu ya kitibet, kuanzia mwaka 1985, serikali ya mkoa unaojiendesha wa Tibet na idara zake za afya zimetunga na kutekeleza sera zaidi ya 10 za kuokoa, kuendeleza na kusanifu matibabu ya kitibet. Katika miaka zaidi ya 20 iliyopita, elimu ya matibabu ya kitibet imesanifiwa hatua kwa hatua. Chuo cha Udaktari wa Matibabu ya Kitibet cha Mkoa wa Tibet, Chuo Cha Udaktari wa Matibabu ya Kitibet cha Mkoa wa Qinghai, idara ya matibabu ya kitibet ya Chuo Kikuu cha Dawa na Matibabu ya Kichina cha Mji wa Chengdu na idara ya matibabu ya kitibet ya Chuo Kikuu cha Dawa na Matibabu ya Kichina cha Mkoa wa Gansu vimewaandaa madaktari wengi wa matibabu ya kitibet kwa hospitali wa sehemu mbalimbali nchini China. Mbali na hayo, baadhi ya hospitali na idara zisizo za kiserikali zinawafundisha madaktari na wauguzi wa matibabu hayo kwa kuandaa semina, ili kukidhi mahitaji makubwa ya matibabu hayo vijijini. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2006, mkoani Tibet kumekuwa na idara 14 za matibabu ya kitibet, hospitali zaidi ya 60 za ngazi ya wilaya zinazoweza kutoa huduma za matibabu hayo, na madaktari na wauguzi zaidi ya 2,000 wa matibabu hayo. Licha ya Tibet, idara za matibabu ya kitibet pia zimeanzishwa kwenye miji zaidi ya 10 nchini China, ili kutoa huduma za matibabu za kitibet kwa wakazi wa miji hiyo.

Maendeleo ya kasi ya matibabu ya kitibet yanatiliwa maanani na watu wa hali mbalimbali kutoka nchini China na nchi za nje. Wageni kutoka nchi za nje duniani mara kwa mara wanatembelea hospitali ya matibabu ya kitibet, ambapo mara kwa mara ujumbe wa madaktari wa matibabu hayo pia unafanya ziara kwenye nchi za nje, ili kueneza elimu ya matibabu hayo.

Mwaka 1992 hospitali ya matibabu ya kitibet ya Beijing ilianzishwa, ili kuunga mkono na kuendeleza zaidi matibabu ya kitibet. Katika miaka ya hivi karibuni, hospitali hiyo iliwakusanya madaktari maarufu wengi wa matibabu hayo. Profesa Nyima Tsering wa hospitali hiyo alisema,

"Hivi sasa matibabu ya kitibet yamepata mabadiliko makubwa ikilinganishwa na wakati kabla Tibet haijakombolewa. Zamani hakukuwa na sehemu nzuri ya kufundisha elimu ya matibabu hayo, lakini sasa hata elimu ya juu kuhusu matibabu hayo imeanza kutolewa."

Imefahamika kuwa kila mwaka wageni kutoka nchi za nje wanaotembelea hospitali ya matibabu ya kitibet ya Beijing wanafikia zaidi ya elfu 20. Takwimu zinaonesha kuwa hadi sasa idadi ya wagonjwa waliotibwa kwenye hospitali hiyo imefikia milioni moja, na kati yao watu zaidi ya laki tatu walitoka nchi zaidi ya 60 duniani na sehemu za Hongkong, Makao na Taiwan.

Kwenye mkoa wa Tibet, shughuli za matibabu ya kitibet pia zimepata maendeleo makubwa, na njia za jadi za matibabu zimechanganyika pamoja na teknolojia ya kisasa. Hivi sasa dawa zaidi ya 20 za kitibet zimewekwa rasmi kweye kitabu cha orodha ya dawa za kichina, na dawa 336 zimefikia vigezo vya kitaifa, na zinauzwa katika nchi za nje. Profesa Nyima wa Chuo cha Udaktari wa Matibabu ya kitibet alisema,

"Mabadiliko makubwa yametokea katika shughuli za matibabu ya kitibet, wananchi wa nchi mbalimbali duniani wanatuandikia barua, na kueleza matumaini yao ya kujifunza na kutafiti matibabu ya kitibet."

Hivi sasa makampuni ya kutengeneza dawa za kitibet yameongezeka kutoka moja kabla ya utekelezaji wa sera ya mageuzi na ufunguaji mlango kuwa kumi na tisa ya sasa, na yanaweza kutengeneza dawa za aina zaid ya 360. Hivi sasa dawa za aina nyingi za kitibet zinauzwa nchini China na katika nchi za nje, na shughuli za dawa za kitibet zimekuwa moja kati ya nguzo za uchumi wa Tibet. Kutokana na mustakabali mzuri wa dawa na matibabu ya kitibet, mitaji ya kimataifa pia imeanza kuingia kwenye shughuli hizo.

Ili kuendeleza zaidi dawa na matibabu ya kitibet, China ilianzisha mada maalumu ya kuokoa na kukamilisha matibabu ya kitibet, na kutafuta na kuokoa njia za matibabu ya jadi na vyeti vya dawa zenye ufanisi vinavyokabiliwa na hatari ya kutoweka kwenye sehemu mbalimbali nchini China. Watu wanaojishughulisha na matibabu hayo wana imani kuwa, hatua hiyo bila shaka itahimiza maendeleo makubwa zaidi ya matibabu ya kitibet.