Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-05-29 15:45:17    
Maelezo kuhusu polisi wawili wa kike

cri

Mjini Pengzhou mkoani Sichuan kuna polisi mmoja wa kike anayeitwa Jiang Min. Yeye ni mtu wa kabila la Waqiang, na wazazi wake pamoja na binti yake mwenye umri wa miaka miwili walipoteza maisha yao kwenye tetemeko la ardhi. Lakini katika hali hii, yeye alivumilia uchungu mkubwa, na bado aliendelea kufanya kazi ya uokoaji kwenye mstari wa mbele. Alisema,

"Wakati ule binti yangu na wazazi wangu walikuwa wamelala nyumbani, majengo yalibomoka na vitu vyote vilitoweka."

Bibi Jiang Min alishika zamu yake katika shule ya sekondari ya Tianpeng mjini Pengzhou, huko kulikuwa na watu zaidi ya 1,400 waliopoteza maskani yao. Alfajiri ya tarehe 18, walikuja watu wa familia moja waliokumbwa na tetemeko la ardhi, Bibi Jiang Min aliwawekea mahema mara moja. Baada ya kuwekewa mahema, watu hao wakapumzika, lakini Bibi Jiang Min alikwenda kumbeba mtoto mikononi aliyekuwa amelala fofofo, na alimfunika kwa mfarishi, akatazama sura ya mtoto kwa muda mrefu. Alisema,

"Nilimkumbuka binti yangu, hasa ninapowaona watoto wenye umri wa miaka kama binti yangu, nikiwa mama namkumbuka sana."

Wakati huo Bibi Jiang Min amefanya kazi ya uokoaji katika mstari wa mbele kwa siku 5 mfululizo. Wakati tetemeko la ardhi lilipotokea mkoani Sichuan, alikuwa anashika zamu ofisini, baada ya kutokea kwa tetemeko la ardhi, mara moja alishiriki katika kazi za uokoaji, lakini hakupata habari hata moja kuhusu jamaa zake.

"Niliwapigia simu lakini sikuweza kuwasiliana nao, lakini bado nilikuwa na matumaini, nina matumaini kuwa bado wako hai."

Siku ya pili baada ya kutokea kwa tetemeko la ardhi, Bibi Jiang Min alipata habari kuwa jamaa zake walikufa kwenye tetemeko la ardhi, lakini alivumilia kwa uchungu mkubwa, akiendelea kufanya kazi yake kimya kimya. Mwishoni alizirai katika sehemu aliyofanya kazi. Mwenzake alisema,

"Alianza kula chakula tarehe 19, katika siku zilizopita hakurudi nyumbani kutokana na habari hizo mbaya, alikuwa anafikiri jambo hilo moyoni na hakula chakula, lakini bado aliendelea kufanya kazi."

Akiwa mtoto aliyefiwa na mama yake na pia akiwa mama aliyefiwa na mtoto wake, Bibi Jiang Min alihamishia upendo na kumbukumbu zake kwa watu waliokumbwa na maafa, aliwapa pole na kuwasaidia, ili watu hao waweze kupata faraja. Alisema anataka kufanya kila awezalo ili watu waliokumbwa na tetemeko la ardhi wapate faraja.

"Naona kuwa wakati huu sisi sote ni ndugu, kama jamaa zangu wasingekufa, ninaamini kuwa wakati huu hakika wangekuwa wanapokea misaada kutoka kwa watu wengine."

Katika sehemu zilizokumbwa na tetemeko kubwa la ardhi huko Wenchuan mkoani Sichuan, kuna polisi wengi wa kike kama Bibi Jiang Min. Mjini Jiangyou mkoani Sichuan kuna polisi wa kike anayeitwa Jiang Xiaojuan. Akiwa mama anamnyonyesha mtoto wake, lakini kutokana na kazi ya uokoaji, alimkabidhi mtoto wake ambaye hajatimiza umri wa nusu mwaka kwa wazazi wake ili wamtunze, yeye mwenyewe alikuwa anawatunza na kuwanyonyesha watoto walionusurika kwenye maafa.

Baada ya kutokea kwa tetemeko la ardhi, mji wa Jiangyou ulipokea watu zaidi ya 10,000 kutoka sehemu zilizokumbwa na maafa hayo, kadiri watu walivyomiminikia kwenye mji huo, ndivyo vyakula na maji ya kunywa mjini Jiangyou vilivyokuwa vinapungua. Lakini baadhi ya watoto wachanga walifiwa na mama zao, baadhi ya watoto hao mama zao walijeruhiwa, na baadhi ya mama hawakuwa na maziwa ya kuwanyonyesha watoto kutokana na kupata mshtuko. Wakati huo Bibi Jiang Xiaojuan alikwenda huko kubeba jukumu la mama. Kuanzia tarehe 14, kwa ujumla Bibi Jiang Xiaojuan aliwatunza watoto wanane wachanga kutoka sehemu zilizokumbwa na tetemeko la ardhi. Aliwachukulia kama watoto wake mwenyewe, na kuwafariji. Alisema kuwalea watoto hao kunamfanya amkumbuke zaidi mtoto wake.

"Mtoto wangu sasa anakunywa uji na maziwa ya unga, kusema kwa kweli nina shinikizo, mtoto wangu hawezi kunyonya maziwa yangu, lakini ikilinganishwa na watoto hao wa sehemu zilizokumbwa na maafa, mtoto wangu ana bahati zaidi."

Hivi sasa Bibi Jiang Min na Bibi Jiang Xiaojuan bado wanafanya kazi za uokoaji pamoja na polisi wengine wengi kwenye mstari wa mbele, kutokana na misaada yao, watu wa sehemu zilizokumbwa na maafa wameanza kuishi maisha yenye utulivu na utaratibu hatua kwa hatua.