Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-05-29 15:46:33    
Opera ya Kunqu yakaribishwa tena nchini China

cri

Opera ya Kunqu inasifiwa kama ni chimbuko la opera za jadi za aina zote nchini China, lakini opera hiyo ambayo imekuwepo kwa miaka zaidi ya 600 iliwahi kuwa hatarini kutoweka. Katika miaka ya hivi karibuni kutokana na juhudi za pamoja, wasanii wamefufua opera hiyo na mchezo wa opera hiyo uitwao "Kibanda cha Peony" unapata watazamaji wengi bila kupungua, na hata katika jamii imetokea wimbi la watu kupenda utamaduni wa opera ya Kunqu, na vitabu na sahani za DVD kuhusu utamaduni huo zinauzwa kwa wingi.

Waigizaji vijana wa Kundi la Opera ya Kunqu la Suzhou na msanii mkubwa wa Japan Bw. Tamasaburo Bando walionesha mchezo huo wa "Kibanda cha Peony" kwa siku kumi mfululizo kwenye Jumba la Huguang mjini Beijing, ambapo wengi walitazama maonesho ya mchezo huo.

Bw. Tamasaburo Bando alijifunza Kichina kwa miaka mingi na aliwahi kufundishwa na msanii mkubwa wa opera ya Kunqu Bi. Zhang Jiqing na baada ya kufanya mazoezi kwa zaidi ya mwaka mmoja ametimiza ndoto yake ya miaka zaidi ya ishirini ya kufanya maonesho ya opera ya Kunqu nchini China. Bw. Tamasaburo Bando aliigiza mhusika mkuu wa opera hiyo Bi. Du Liniang.

Bw. Tamasaburo Bando alimheshimu sana msanii mkubwa wa opera ya Kibeijing wa China Bw. Mei Lanfang, na babu yake Bando pia aliwahi kufanya maonesho ya opera ya Kibeijing kwenye Jumba la Huguang. Jumba hilo ni maarufu na lenye historia ndefu sana mjini Beijing. Kwenye mkutano na waandishi wa habari alieleza jinsi alivyotimiza tumaini lake la kufanya maonesho ya opera ya Kunqu. Alisema,

"Nilikuja Beijing kwa mara ya kwanza miaka 20 iliyopita, na nilikwenda kwenye Jumba hilo la Huguang kwa mara ya kwanza miaka 10 iliyopita, na miaka miwili iliyopita nilikuwa na tumaini la kuonesha hadithi ya "Kibanda cha Peony" kwenye jukwaa, na miezi mitatu iliyopita nilitimiza tumaini hilo mjini Tokyo Japan, na sasa nimepata fursa ya kuonesha opera ya Kunqu mjini Beijing. Nina matumaini kuwa nitafanikiwa kuigiza kwa juhudi zangu zote."

Kabla ya opera hiyo kuoneshwa Bw. Tamasaburo Bando alisema ingekuwa bora kama mazingira ya kutazama maonesho ya opera hiyo yawe kama ya zamani. Kutokana na ushauri wake huo ndani ya ukumbi wa kuonesha opera hiyo ziliwekwa meza zilizofunikwa kwa kitambaa chenye maua ya peony na juu ya meza yaliwekwa majagi yenye maua ya peony. Baada ya maonesho ya opera kumalizika watazamaji waliokuwa na furaha walimsifu sana kiasi kwamba hata alitoa shukrani mara tatu, makofi yaliyomshangilia yalimfanya atokwe machozi.

Opera ya Kunqu ina historia ndefu kuliko opera ya Kibeijing, hadi sasa imekuwa na historia ya miaka zaidi ya 600. Lakini kutokana na kujitokeza kwa aina nyingi za burudani katika jamii ya sasa, opera ya Kunqu ilikuwa kwenye hatari ya kutoweka. Mwaka 2001 sanaa ya opera hiyo ilichaguliwa na UNESCO kuwa ni "mwakilishi wa utamaduni usioonekana" na kupewa uzito na umma na serikali ya China. Kati ya hadithi zinazooneshwa kwa opera ya Kunqu hadithi ya "Kibanda cha Peony" ni ya kwanza kuoneshwa jukwaani. Hadithi hiyo ilihaririwa kuwalenga watazamaji vijana na iliwavutia sana.

Opera ya Kunqu ya "Kibanda cha Peony" ilihaririwa kwa mujibu wa hadithi ya kale yenye jina hilo hilo, ikieleza mapenzi ya kusikitisha kati ya kijana Liu Mengmei na msichana Du Liniang. Msichana Du Liliang wa familia ya maofisa alikutana na msomi maskini Liu Mengmei katika bustani ya nyumbani kwa bibi Du Liniang na wakapendana, lakini kutokana na upinzani wa familia ya Du Liniang na hadhi tofauti ya kijamii wapenzi hao wawili hawakuweza kuoana kama walivyo Romeo na Julieta.

Msomi na mwandishi wa vitabu wa Taiwan Bw. Bai Xianyong alitoa mchango mkubwa katika juhudi za kufufua opera ya Kunqu. Kwa nyakati tofauti alishirikiana na wasanii wa China bara, kisiwani Taiwan na Hong Kong kuhariri opera hiyo, alichagua waigizaji hodari, kuwasiliana na kuomba wasanii wa opera ya Kunqu waandae waigizaji vijana, na kusaidia opera hiyo kuoneshwa katika kisiwa cha Taiwan, Hong Kong, Marekani na Uingereza. Anaona kuwa huu sio mchezo tu, bali pia ni jaribio la kuokoa sanaa ya opera hiyo. Alisema,

"Opera ya Kunqu ya 'Kibanda cha Peony' haikupatikana kwa urahisi, tulifanya juhudi nyingi ikiwa ni pamoja na misaada ya hali na mali kutoka wataalamu, makampuni na serikali. Tulipohariri mchezo huo tuliona tunafanya juhudi za kuokoa sanaa ya opera hiyo."

Bw. Bai Xianyong alisema katika zama za leo ambapo utamaduni wa jadi wa China unamomonyolewa na utamaduni wa nchi za nje, sanaa inayowakilisha utamaduni wa jadi wa China inahitaji kulindwa zaidi. Kazi yao ni kuandaa waigizaji wa sanaa hiyo na kuieneza miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu.

Mwigizaji mwenye umri wa miaka 30 wa Kundi la Opera ya Kunqu la Suzhou Bw. Yu Jiulin aliigiza kama kijana Liu Mengmei kwenye opera ya Kunqu hadithi ya "Kibanda cha Peony". Alisema, anaheshimu sana mwalimu wake na wasanii wazee jinsi walivyojitahidi kuokoa sanaa hiyo. Alisema,

"Wasanii wa opera ya Kunqu walitumia miaka mingi kushughulika na sanaa hiyo, wamejibebesha jukumu la kurithisha sanaa hiyo na kutufundisha kila kitu bila kuficha."

Juhudi zao hazikuwa bure. Opera ya "Kibanda cha Peony" ingawa imeoneshwa kwa zaidi ya mara 100, lakini hadi leo inavutia watazamaji wengi bila kupungua na baadhi ya wanafunzi wameitazama mara kadhaa. Mwanafunzi Bi. Zhang Hui alisema, opera hiyo inamkumbusha mazingira mazuri ya kimaisha kusini mwa China na nyimbo za opera hiyo zinampatia raha ya aina pekee tofauti na opera za aina nyingine. Mwezi Machi mwaka huu opera hiyo ilioneshwa nchini Japan mara 20 na kila mara watazamaji walijaa kwenye jumba lenye nafasi 1,600.