Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-05-30 21:18:57    
:Kuwalinda wanafunzi bila kujali kuhatarishwa kwa usalama wa maisha yao wenyewe

cri

Baada ya kutokea tetemeko kubwa la ardhi tarehe 12 wilayani Wenchuan, mkoa wa Sichuan, sehemu ya kusini magharibi ya China, mambo mengi kuhusu watu walivyokuwa wanajitahidi kujiokoa, na wakazi waliokumbwa na maafa walivyokuwa kusaidiana, yamewavutia watu wote wa China. Saa 8 na dakika 28 ya adhuhuri ya tarehe 12, muda wa mapumziko ya adhuhuri uliisha, wanafunzi 483 wa shule moja ya msingi ya wilaya ya Beichuan, mkoani Sichuan, bado walikuwa wakicheza kwenye kiwanja cha shuleni, ambapo baadhi ya wanafunzi walikuwa wakipumzika kwenye madarasa yao yaliyoko kwenye gharofa ya pili. Ghafla ardhi ilianza kutetemeka, milango na madirisha yaliyumba kwa nguvu. "Tetemeko la ardhi!" Waalimu walisema kwa kupaza sauti na kutaka wanafunzi wakimbilie kiwanjani. Baada ya kupita sekunde kumi na kidogo, tetemeko la ardhi lilikuwa kali zaidi, baadhi ya nyumba za wakazi wa huko zilianza kubomoka. Waalimu walitaka wanafunzi wakusanyike kwenye sehemu ya katikati ya kiwanja, katika tetemeko kali hilo baadhi ya watu walijilaza chini. Hapo hapo, baadhi ya waalimu walikimbilia kwenye vyumba vya madarasa na kuwatafuta wanafunzi kutoka darasa moja hadi darasa lingine, ili kuwatoa wanafunzi walioshindwa kuondoka.

Vumbi lililorushwa angani na tetemeko la ardhi, liliwafanya waalimu na wanafunzi kupumua kwa shida sana. Na kutokana na kukabiliwa na matetemeko madogo yaliyofuata, mwalimu mkuu wa shule hiyo Bw. Xiao Xiaochuan alifanya haraka kuwaelekeza wanafunzi wote wa shule hiyo wakimbilie kwenye mlima unaotazamana na shule yao. Hali iliyomfurahisha Bw Xiao Xiaochuan ni kuwa hakukuwa na mwanafunzi hata mmoja aliyejeruhiwa katika tetemeko hilo la ardhi! Siku hiyo alasiri, wazazi wa wanafunzi walianza kufika kwenye mlima huo kuwachukua watoto wao. Lakini ilipofika saa 11 ya alasiri ya siku hiyo, bado kulikuwa na wanafunzi 71, ambao hakuna wazazi wao kwenda kuwachukua.

Asubuhi ya siku ya pili, waalimu 9 waliokuwa wanawalinda wanafunzi hao usiku kucha, walikuwa na mkutano mdogo, waliamua kuondoka huko haraka ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi hao. Lakni haikuwa rahisi kupata njia ya kuondoka kutoka huko. Mwalimu mmoja wa shule hiyo alisema,

"Njiani tuliona mawe yaliyoviringika chini kwenye miteremko ya milima, chini ya miguu yao kulikuwa na udongo laini na matope, hivyo walishindwa kutembea kwa miguu ila tu waliweza kutambaa kwa miguu na mikono."

Kwa namna hii, waalimu 9 na wanafunzi 71 walinusurika katika maafa. Kati ya wanafunzi hao mwanafunzi mdogo zaidi ana umri wa miaka 5 tu, na mkubwa kabisa ana umri wa miaka 14. Baada ya kupatwa na shida nyingi na kutembea kwa umbali wa zaidi ya kilomita 50 kwenye njia ya milimani, waalimu na wanafunzi hao wakisaidiwa na waokoaji, walifika kwenye shule ya sekondari ya mji wa Mianyang, ambapo maisha yao yaliweza kupangwa vizuri. Kati ya walimu 9 waliowaongoza wanafunzi 71 kuhamia kwenye sehemu ya nje, wanne walifahamu kuwa kulikuwa na watu wa familia zao ambao walikufa kwenye maafa. Mwalimu mmoja alifiwa na jamaa 7; na waalimu wengine, hadi hivi sasa bado hawajapata habari yoyote kuhusu watu wa familia zao.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Bw. Xiao Xiaochuan alisema,

"Baba yangu amekuwa na umri wa miaka 81, hadi sasa bado sijapata habari yoyote kuhusu yeye."

Mambo ya kuvutia kama hayo pia yalitokea kwenye sekondari ya Juyuan mjini Dujiangyan. Alasiri ya tarehe 12 mwezi Mei, mwalimu kijana wa somo la jiografia wa shule hiyo, Bw. Pu Bin alikuwa darasani kama kawaida. Wakati lilipotokea tetemeko la ardhi mwalimu Pu alikuwa akifundisha kwenye darasa lililoko kwenye ghorofa ya chini, endapo akienda mita 2 tu, aliweza kunusurika kabisa, lakini hakukimbia, bali aliwaelekeza wanafunzi kukimbia darasani.

Kutokana na jitihada ya mwalimu Pu, wanafunzi 56 kati ya 76 walinusurika, lakini mwalimu huyu mwenye umri wa miaka 28 alikufa katika maafa kwa ajili ya kuwanusuru wanafunzi wake. Wakati watu walipoona mwili wa mwalimu Pu baada ya kuondoa kifusi kilichomfukia, chini ya mwili wake waliona miili ya wanafunzi kadhaa. Waokoaji walisema,

"Huenda wakati wanakimbia jengo lilikuwa linabomoka, alinyoosha mikono na kuwafunika miili yao."

Wanafunzi waliookolewa na mwalimu Pu, walipoeleza kuhusu mwalimu wao walisema huku wakitokwa na machozi.

"kama mwalimu asingefika kutuelekeza, ningekuwa nimelazwa au ningekuwa nimefariki dunia."

"Asante, mwalimu Pu!"

Watu waliohuzunika si walimu na wanafunzi tu. Mke wa mwalimu Pu, ambaye alichumbiana naye kwa miaka 8, na walifunga ndoa katika sikukuu ya mwaka mpya, sasa hawezi kuishi tena pamoja na mumewe, akiwa na uchungu mwingi, alisema,

"Unaniacha hivi hivi tu, sina chochote hata mtoto."

Mama wa Pu Bin pia alihuzunika sana. Akisema,

'Mwanangu amefariki, nina masikitiko makubwa, lakini kwa kuwa amewaokoa wanafunzi 56, ameleta furaha kwa kina mama 56. Ninamjivunia mwanangu."

Wanafunzi wamenusurika, lakini mwalimu wao amefariki. Wakati lilipotokea tetemeko la ardhi, waalimu waliwanusuru wanafunzi kwa akili na ushujaa wao, na hata kwa maisha yao. Jambo muhimu zaidi ni kuwa waalimu waliwafundisha wanafunzi wao kwa moyo wa ushupavu, na wanafunzi watanufaika katika maisha yao yote.