Mradi wa kukarabati Hekalu la Tashi Lhunpo analoishi kiongozi wa kidini mkoani Tibet Banchan ulianza rasmi hivi karibuni. Mradi huo utagharimu pesa nyingi zaidi kuliko miradi mingine ya kuhifadhi mabaki ya utamaduni mkoani Tibet, iliyopangwa kufanyika kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2010, na pesa hizo zote zimetengwa na serikali kuu ya China.
Hekalu la Tashi Lhunpo liko chini ya mlima Nima ulioko kaskazini magharibi mwa mji wa Rikaze kwenye mkoa unaojiendesha wa Tibet, na lina eneo la mita za mraba laki 2.37. Hekalu hilo lilijengwa mwaka 1447, na lilianza kuwa hekalu la Banchan mnamo mwaka 1713. Baada ya ujenzi kwa mamia ya miaka, hekalu hilo sasa lina jumba kuu moja liitwalo Cuoqin, majumba makubwa mengine 6, majumba 56 ya misahafu, na nyumba zaidi ya 6,000 ya masufii. Kwenye hekalu hilo, kuna mabaki mengi ya utamaduni, na kati ya mabaki hayo sanamu ya buddha ya Qiangba yenye urefu wa mita 26.2 iliyojengwa mwaka 1914 ni sanamu ya budha kubwa zaidi duniani iliyotengenezwa kwa shaba na kupakwa na rangi ya dhahabu duniani. Mwaka 1961, Hekalu la Tashi Lhunpo liliwekwa kuwa sehemu muhimu ya utamaduni inayohifadhiwa. Lakini kutokana na kutokarabatiwa kwa miaka mingi, hekalu hilo linakabiliwa na hatari mbalimbali. Safari hii, majengo ya hekalu hilo yatakarabatiwa kwa pande zote, zikiwemo mfumo wa kinga ya moto na mfumo wa usalama. Mkurugenzi wa ofisi ya uhifadhi wa mabaki ya utamaduni ya idara ya mabaki ya utamaduni ya Tibet Bw. Liu Shizhong alisema,
"Serikali kuu ya China ilitenga Yuan milioni 120 kwa ajili ya mradi wa kukarabati Hekalu la Tashi Lhunpo. Mradi huo hasa ni kwa ajili ya kukarabati majengo muhimu ya hekalu hilo likiwemo jumba la kaburi la Banchan wa Nne, jumba linalohifadhi sanamu ya Qiangba na jumba kuu la Cuoqian, na ujenzi mwingine wa mfumo wa kinga ya moto na mfumo wa usalama."
Imefahamika kuwa, kutokana na kuwa mradi huo ni mkubwa unaogharimu pesa nyingi, serikali ya mkoa wa Tibet ilianzisha kikundi cha uongozi na uratibu mwezi Aprili mwaka 2007, na kuanzisha ofisi za uongozi kwenye miji minne ya Lhasa, Rikaze, Shannan na Ali. Ofisa mwandamizi wa mji wa Rikaze Bw. Xu Xueguang alisema, kanuni ya mradi huo ni kuvikarabati vitu vya kale bila kubadilisha sura ya vitu hivyo vya awali. Alisema,
"Tunapaswa kushikilia vizuri kanuni ya kukarabati mabaki ya kale ya utamaduni, kuheshimu mila na desturi, kutegemea teknolojia ya kisasa na kuchanganisha mbinu za kabila la Watibet na Wahan, ili kuhakikisha sifa za mradi huo."
Kuanzishwa kwa mradi wa kukarabati Hekalu la Tashi Lhunpo kumefurahisha masufii wa hekalu hilo. Naibu mkurugenzi wa kamati ya hekalu hilo Bw. Salung Phunlha alisema,
"Masufii wote wa Hekalu la Tashi Lhunpo watakumbuka msaada mkubwa kutoka serikali kuu, na watafanya vizuri shughuli za kidini kwa moyo wa kulinda taifa na kuwanufaisha wananchi na kuheshimu mafunzo ya Banchan wa 10 na wa 11, na pia watatekeleza kwa makini sera na sheria za China kuhusu shughuli za dini, ili kuhakikisha shughuli za dini za hekalu hilo zinafanyika kutokana na sheria."
Mkoa wa Tibet ni mmoja kati ya mikoa yenye mabaki mengi ya utamaduni ya kale. Mkoani humo kuna maelfu ya sehemu za mabaki ya utamaduni ya kale, na kati yao, sehemu tatu zimewekwa kwenye orodha za mabaki ya utamaduni za kimataifa. Tangu Tibet kukombolewa kwa njia ya amani katika miaka ya 50 ya karne iliyopita, hasa baada ya utekelezaji wa sera ya mageuzi na ufunguaji wa mlango, serikali ya China inatilia maanani sana kazi za kuhifadhi mabaki ya utamaduni ya kale, na hadi sasa kwa nyakati tofauti imefanya miradi ya kukarabati mabaki muhimu ya utamaduni mkoani Tibet yakiwemo Kasri la Potala, Hekalu la Norbulingka, na Hekalu la Sajia kwa kutenga Yuan zaidi ya milioni 700, na kuyahifadhi vizuri mabaki hayo kwa njia zenye ufanisi. Mkurugenzi wa idara ya mabaki ya utamaduni ya kale ya Tibet Bw. Yudawa alijulisha kuwa, mbali na kukarabati Hekalu la Tashi Lhunpo, serikali ya China pia itakarabati mabaki mengine ya kale ya utamaduni mkoani Tibet, likiwemo Hekalu la Jokhang na Hekalu la Ramoche, alisema,
"China imepanga miradi 22 ya kuhifadhi mabaki ya kale ya utamaduni mkoani Tibet kati ya mwaka 2006 hadi mwaka 2010. Kamati ya maendeleo na mageuzi na wizara ya fedha ziliipa Tibet sera ya upendeleo, na kutenga Yuan milioni 570 kwa ajili ya miradi hiyo, na pesa hizo zimeongezeka kwa yuan milioni 200 ikilinganishwa na zile zilizotengwa kati ya mwaka 2001 na mwaka 2005. Hali hii inaonesha kuwa serikali kuu ya China inatilia maanani sana shughuli za kuhifadhi mabaki ya kale ya utamaduni mkoani Tibet."
Bw. Yudawa alisema miradi mitatu ya kuhifadhi na kukarabati Kasri la Potala, Hekalu la Norbulingka na Hekalu la Sajia ilianza rasmi mwezi Mei mwaka 2002, na pesa zote Yuan milioni 330 zilizotumiwa kwenye miradi hiyo zilitengwa na serikali kuu ya China. Hivi sasa, miradi midogo 134 ya miradi hiyo mitatu ilianza, kati ya hiyo miradi 129 imekamilika, na miradi hiyo mitatu itakamilika kabisa ndani ya mwaka huu.
Idhaa ya kiswahili 2008-06-02
|