Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-06-05 15:49:58    
Mwanamke wa Korea Kusini atakayekimbiza mwenge wa michezo ya Olimpiki ya Beijing

cri

Bi. Cho Sung Hye alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari, alisema (sauti 1) "Mimi ni raia wa Korea Kusini, na hivi sasa nimepata nafasi ya kuishi kwa muda mrefu nchini China. Mbali na hayo nilipewa tuzo ya urafiki na serikali ya China, na kuteuliwa kuwa mkimbiza mwenge wa michezo ya Olimpiki ya Beijing. Naona fahari kubwa, ninataka watu wote wafahamu furaha yangu."

Katika miaka 12 iliyopita tangu Bi. Cho Sung Hye aanze kuishi mjini Hefei, China amekuwa akitoa mchango katika kuhimiza uhusiano wa kiuchumi na kibiashara na mawasiliano ya kiutamaduni kati ya China na Korea ya Kusini. Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 50 alisema hivi sasa yeye ni kama wakazi wengine wa mji wa Hefei, hata hivyo hajabadilisha tabia ya kukaa kwenye kochi au sakafuni kwa kukunja miguu, ambayo ni tabia ya watu wa Korea.

Bi. Cho Sung Hye alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, kabla ya kuhamia nchini China, yeye alikuwa mkuu wa shule ya chekechea na mume wake alikuwa anaendesha duka la kompyuta, walikuwa na maisha mazuri huko Korea Kusini. Hata hivyo mwaka 1996 yeye na mume wake walipokea pendekezo la mtoto wake la kuhamia kwenye mji wa Hefei, China, na kuanza kufanya kazi ya ualimu wa kufundisha lugha ya Kikorea katika chuo kikuu kimoja cha huko.

Awali walipofika China walikabiliwa na tatizo la lugha na desturi tofauti za maisha. Bi. Cho Sung Hye alisema walianza kujifunza lugha ya Kichina kwa bidii, na sasa hata anaweza kuongea kidogo kwa lafudhi ya wenyeji, ambayo alijifunza sokoni.

Baada ya kuzoea maisha nchini China, mwanamke huyo kutoka Korea Kusini alianza kufanya mpango wa kufanya biashara. Alisema  "Mwaka 1996 tulipohamia nchini China, baadhi ya bidhaa za China zilikuwa zinapatikana nchini Korea Kusini, kama vile mazao ya kilimo na mahitaji ya kila siku, kwa hiyo nilipenda pia niweze kununua bidhaa za Korea Kusini nchini China."

Muda si mrefu baadaye, Bi. Cho Sung Hye alianza kutekeleza mpango wake wa kuanzisha eneo la kuuzia bidhaa za Korea Kusini mjini Hefei. Alisema  "Nikifuatana na viongozi wa idara ya kuvutia uwekezaji ya Hefei na eneo la maendeleo ya uchumi la mji huo, tulitembelea Korea Kusini mara nne, ambapo tuliandaa shughuli za kuutangaza mji wa Hefei, ili kuwavutia wafanyabiashara wa Korea Kusini waje kufanya biashara hapa Hefei, kwani nina imani kuwa mji huo ni mzuri wa kuwekezwa vitega uchumi. Mji huo una mawasiliano rahisi, mpangilio mzuri na hali nzuri ya miundo mbinu, pia serikali ya mji wa Hefei ilitoa sera nyingi zenye unafuu kwa wawekezaji wa kigeni."

Kutokana na jitihada zake, mwaka jana soko kubwa la kwanza la kuuza bidhaa za Korea Kusini lilianzishwa rasmi huko Hefei. Meneja mkuu wa soko hilo Bibi Shi alieleza kuwa, sokoni hapa zinauzwa nguo na bidhaa za mapambo kutoka Korea Kusini, pia kuna mikahawa ya chakula cha Korea Kusini. Soko hilo linawavutia wateja wengi wa China. Meneja mkuu huyo alisema (sauti 5) "Bidhaa zote kwenye soko hilo zina umaalumu wa Korea Kusini. Na Bi. Cho Sung Hye mwenyewe aliamua ni bidhaa za namna gani zinaweza kuuzwa, mtindo wa biashara na mbinu za usimamizi."

Mteja Bi. Li Xiuyun alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari, alisema  "Naona soko hilo la Korea Kusini lina mazingira mazuri, linapendeza na bidhaa za Korea Kusini ni za mtindo wa kisasa na bei zake si ghali. Inafaa watu wa kawaida kufanya manunuzi kwenye soko hilo."

Zaidi ya hayo Bi. Cho Sung Hye anajitahidi kuhimiza mawasiliano kati ya China na Korea Kusini katika sekta za utamaduni na elimu. Kutokana na juhudi zake, shule za msingi na za sekondari zipatazo kumi kadhaa mjini Hefei zilijenga urafiki na shule za Korea ya Kusini, na vyuo vikuu kadhaa huko Hefei pia kujenga mawasiliano na vyuo vikuu nchini Korea ya Kusini.

Kutokana na mchango aliotoa katika kuimarisha mawasiliano kati ya watu wa China na wa Korea ya Kusini, mwaka 2002 Bi. Cho Sung Hye alipewa tuzo ya urafiki, ambayo ni tuzo ya juu kabisa inayotolewa na serikali ya China kwa wataalamu wa nchi za nje waliotoa mchango mkubwa katika ujenzi wa kisasa na juhudi za mageuzi na ufunguaji mlango nchini China. Zaidi ya hayo aliteuliwa kuwa mkimbiza mwenge wa michezo ya Olimpiki ya Beijing.

Kuhusu mafanikio hayo, Bi. Cho Sung Hye alisema  "Ninaona sifa hizo ni kubwa sana, kwani nilifanya shughuli kadhaa tu na kupewa tuzo kubwa sana. Kwa hiyo nimeamua nia kuwa, nitajitahidi zaidi."

Bi. Cho Sung Hye alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, familia yake inapenda utamaduni wa China, wanapenda chakula cha Hefei, nyimbo za kisasa za China na filamu za Gongfu za China. Na siku nyingine pia wanawaalika marafiki wa China kuonja chakula cha Korea Kusini. Alisema kwa sasa mji wa Hefei ni maskani yake.

Idhaa ya kiswahili 2008-06-05