Wasikilizaji wapendwa karibuni katika kipindi hiki cha chemsha bongo kuhusu ujuzi wa Mkoa wa Guangxi wenye vivutio vya utalii. Leo tunawaletea makala ya nne kuhusu sehemu ya pwani yenye mandhari nzuri ya bahari, mvuto pekee wa kabila dogo na vivutio vya kisasa katika Mkoa unaojiendesha wa kabila la wazhuang nchini China.
Kwanza tunatoa maswali mawili ya makala hii. Swali la kwanza, Sikukuu yenye shamrashamra kubwa zaidi ya kabila la wajing ni sikukuu gani? Swali la pili, Mji unaosifiwa kuwa ni mji wenye hewa nyingi zaidi ya oxygen kuliko miji mingine nchini China ni mji gani? Tafadhali sikilizeni kwa makini ili muweze kupata majibu sahihi.
China ni nchi yenye makabila mengi, na watu wa kabila la wajing wenye idadi ya watu zaidi ya elfu 20 wanaishi huko Dongxing, mji ulioko kusini mwa mkoa wa Guangxi. Mji huo ulioko kwenye pwani ya bahari, utamaduni wake ni wenye mvuto pekee wa kabila la wajing.
Mliosikia ni muziki uliopigwa kwa kinanda cha Duxianqin. Kinanda hicho ni kinanda kinachopendwa sana na watu wa kabila la wajing, kina uzi mmoja tu, hivyo kinajulikana sana nchini China. Mji wa Dongxing uko kwenye sehemu ya mpaka kati ya China na Vietnam, pande zake za magharibi na kusini zinakabiliana na Mto Beilun mjini Mong Cai, Vietnam, na upande wake wa kusini mashariki unapakana na ghuba ya kaskazini. Watu wa kabila la wajing wanaoishi kwenye sehemu hiyo wanategemea kazi ya kuvua samaki kizazi baada ya kizazi. Mpaka sasa watu wa kabila la wajing wanadumisha desturi yao moja kwamba, kama mgeni anataka kula samaki, anaweza kwenda kwenye meli au mashua zilizorudi baada ya kuvua samaki kuchukua samaki na kuondoka nao, na mwenyeji hawezi kuhamaki. Ukarimu na uchangamfu walionao wajing umemfanya kila mgeni aliyefika huko awe na hamu ya kuishi maisha yenye hali ya asili na burudani ya kando ya bahari, ama kujaribu kuvua samaki mwenyewe, ili kujionea raha mustarehe.
Watu wa kabila la wajing, mbali na kusherehekea sikukuu za mwaka mpya wa jadi, sikukuu ya Duanwu ya tarehe 5 ya mwezi wa 5 kwa kalenda ya kilimo ya China, na sikukuu ya mbalamwezi ya tarehe 15 ya mwezi wa 8 kwa kalenda ya kilimo ya China kama walivyo watu wa kabila la wahan, siku ya tarehe 10 ya mwezi wa 6 kwa kalenda ya kilimo ya China kila mwaka inayoitwa "siku ya Changha" ni sikukuu yenye shamrashamra kubwa zaidi inayosherehekewa kwa shangwe zaidi na watu wa kabila la wajing. Mwongoza watalii wa sehemu hiyo Bi. Yang Jinghong alisema:
"Changha", maana yake ya kichina ni kuimba, kuimba nyimbo kuonesha heshima kwa mungu wa bahari, na kueleza hisia za mapenzi na urafiki".
Kila ifikapo "siku ya Changha", wanaume na wanawake, wazee na watoto wote wanaovaa nguo za sikukuu na wakikusanyika kwenye kibanda kilichoko kwenye umbali wa kilomita 15 katikati ya mji wa Dongxin, wanaimba nyimbo na kucheza ngoma kwa furaha kubwa, shamrashamra ya vifijo na vigelegele vinajaa huko.
Mnaosikia ni wimbo uitwao "Wanwan" unaosifu mandhari nzuri ya huko, sasa hebu tuelekee mashariki kwa kufuata mwambao wa bahari na tutafika kwenye eneo la ghuba ya San niang Wan mjini Qinzhou, tutaona bahari yenye rangi buluu, pwani inayopendeza, mawe yenye maumbo ya ajabu na pomboo wenye rangi nyeupe wa taifa la China.
Pomboo ni wanyama wanaopendwa sana kutokana na kuwa na akili, urafiki, upole na kutoogopa watu. Mahali mazuri pa kuwaangalia wanyama hao kwa karibu ni ghuba ya San niang Wan ambapo panasifiwa kama ni maskani ya "pomboo weupe wa China". Pamboo weupe wa China wana rangi ya maziwa mwili mzima isipokuwa tu rangi ya pinki kwenye tumbo na mkia, ni wanyama adimu wanaohifadhiwa katika ngazi ya kwanza nchini China. Kwenye eneo la ghuba ya San niang Wan wanaishi pomboo mia kadhaa, na mwaka mzima watu wanaweza kuwaangalia kwa karibu, kila wavuvi wanapokwenda kuvua samaki au watalii wanaposafiri baharini, pomboo hao huwafuata nyuma yao huku wakichezacheza, mandhari inayoonesha uhusiano wa mzuri kati ya wanadamu na pomboo inavutia sana.
Mandhari nyingine inayovutia kwenye ghuba ya San niang Wan ni majabali yenye maumbo huku na huko. Miamba yenye sura mbalimbali za ajabu ni mingi, baadhi imechongoka, mingine inaonekana kama mwewe anayeruka, mingine inaonekana kama Simba aliyekaa, baadhi inaonekana kama mamba anayeangalia mbinguni na mingine inaonekana kama nyangumi aliyelala.
Kuhusu jina la San niang Wan pia kuna masimulizi ya kuvutia miongoni mwa wenyeji wa huko. Inasemekana kwamba katika zama za kale kulikuwa na wavuvi watatu waliokwenda kuvua samaki baharini, lakini hawakuweza kurudi, kila siku wake zao walikuwa wakiangalia bahari kwenye ukingo wakitamani waume zao warudi, siku zikawa mwezi, miezi ikawa miaka, mwishowe mama hao watatu wakabadilika na kuwa majabali matatu. Wavuvi wa huko waliguswa sana kutokana na mapenzi na uaminifu wa kina mama hao watatu, wakayapatia majabali matatu jina la San niang yaani "kina mama watatu" na ghuba inaitwa kuwa San niang Wan.
Mandhari ya ghuba ya San niang Wan inavutia sana, kutokana na wimbo wa "Mandhari ya Usiku ya San Nyang" waliotunga wavuvi wa huko tunaweza kufahamu jinsi mandhari nzuri ilivyo.
Wimbo unasema, "Sura za mama watatu zinapendeza. Bahari kubwa na mbingu ya buluu vinavutia. Shakwe wanalialia na watalii wanachekacheka. Upepo wa bahari unawaondolea kero. Ufukwe mweupe unafunikwa na miti, na mawimbi yanapigapiga kingo."
Baada ya kufurahia mandhari ya ghuba ya San Nyiang Wan na pomboo weupe, tuliendelea na safari yetu kwenda kwenye mji wa Beihai. Mji wa Beihai ni peninsula inayozungukwa na bahari kwa pande tatu. Udongo mwekundu, bahari ya buluu, ufukwe mweupe na michikichi, yote hayo yanaunda mandhari nzuri kama picha ya kuchorwa na hali nzuri ya kimaumbile, huu ni mji unaofaa sana kuishi kwa binadamu. Huko hakuna joto katika majira ya joto wala baridi katika majira ya baridi, hewa na maji ni safi, kila ujazo wa mita moja kuna chembechembe za oxygen kati ya 2,500 na 5,000 ambazo ni mara mia moja zaidi kuliko miji ya ndani ya China, watu wanausifu mji huo kuwa ni "mji wenye oxygen nyingi nchini China".
Kutembea peku kwenye pwani ya Bahari ya Beihai yenye urefu wa kilomita 10, njia pana ya pwani, mchanga laini na bahari kubwa isiyo na upeo, yote hayo yanaweza kuwawezesha watu wapate hisia mpya tofauti, na kujionea mvuto mkubwa wa sehemu hiyo yenye mandhari nzuri. Mtalii kutoka Marekani Johny Loop alisema:
"Bahari ya Beihai ni sehemu yenye mandhari nzuri sana, rafiki yangu aliniambia kuwa, ni lazima nije hapa kwenye Bahari ya kaskazini, kwani sehemu hiyo ina mvuto wa kipekee".
Wasikilizaji wapendwa, sasa tunatoa maswali mawili: Swali la kwanza, Sikukuu yenye shamrashamra kubwa zaidi ya kabila la wajing ni sikukuu gani? Swali la pili, Mji unaosifiwa kuwa ni mji wenye hewa nyingi zaidi za oxygen kuliko miji mingine nchini China ni mji gani?
Idhaa ya kiswahili 2008-06-17
|