Kutokana na kuwa kwenye mwinuko mkubwa kutoka usawa wa bahari, mkoa unaojiendesha wa Tibet wa China unajulikana kama sehemu iliyoko karibu zaidi na jua. Hivi sasa wakazi wa kawaida wa mkoa huo kutumia majiko ya nishati ya jua na vyombo vya kuongeza joto ya maji kwa nishati ya jua kumekuwa mtindo wa kisasa wa maisha ya familia nyingi.
Tsomo ni mkazi wa Lhasa, mji mkuu wa mkoa wa Tibet, alijulisha kuwa tangu mwaka jana familia yake iliponunua chombo cha kuongeza joto ya maji kwa nishati ya jua mabadiliko makubwa yametokea katika maisha yake, alisema,
"Tangu tuanze kutumia chombo cha kuongeza joto ya maji kwa nishati ya jua, ni rahisi kwetu kusafisha mboga, kupika chakula na kuogea. Mchana tunatia maji baridi kwenye chombo hicho, usiku tunaweza kupata maji moto. Zamani tulichemsha maji kwa kutumia kuni, na moshi ulikuwa unajaa nyumbani."
Nishati ya jua ni nishati mpya, na ina umaalumu wa kuwa safi, kutosababisha uchafuzi kwa mazingira na ni nishati endelevu ikilinganishwa na nishati za jadi. Hivi sasa kutokana na upungufu wa nishat za jadi, nishati ya jua imekuwa nishati isiyo na uchafuzi kwa mazingira inayohimizwa kutumiwa duniani. Kwenye mkoa wa Tibet nchini China, maliasili ya nishati hiyo ni kubwa sana. Naibu mchunguzi wa kituo cha utafiti na mfano wa matumizi ya nishati cha Tibet Bw. Wang Haijiang alisema,
"Kipimo cha maliasili ya nishati ya jua ni muda wa kuwepo kwa mwangaza wa jua kwa mwaka na nguvu ya mwanga wa jua. Kwenye mkoa wa Tibet, muda unaokuwa na mwangaza wa kutosha wa jua kwa mwaka ni saa karibu 3,000, na ni mara mbili kuliko sehemu nyingine zilizoko kwenye latitudo moja na mkoa huo nchini China, kwa upande wa nguvu ya mwangaza wa jua, katika mkoa wa Tibet nguvu hiyo ni kubwa zaidi kwa asilimia 20 kuliko kigezo husika, na ni mara mbili kuliko sehemu nyingine zenye latitudo moja. Mkoa wa Tibet ni sehemu yenye maliasili nyingi zaidi ya nishati ya jua nchini China, na pia unachukua nafasi ya mbele duniani. Hivyo tunasema mkoa wa Tibet unafaa kuendeleza matumizi ya nishati ya jua."
Serikali ya mkoa unaojiendesha wa Tibet siku zote inatilia maanani sana shughuli za kuendeleza na kutumia nishati safi, na kutekeleza kwa nyakati tofauti miradi husika kadha wa kadha yenye ufanisi mkubwa wa kiuchumi na kijamii, ikiwemo Mpango wa Jua la Tibet, Mpango wa Mwangaza wa Sayansi, Mpango wa Mwanga na Umeme kwenye sehemu ya Ali mkoani Tibet. Hatua hizo zimeharakisha shughuli za matumizi ya nishati ya jua mkoani Tibet. Naibu mtafiti wa kituo cha utafiti na vielelezo vya nishati cha Tibet Bw. Wang Haijiang alisema,
"Mkoa wa Tibet ulianzisha shughuli za kutumia nishati ya jua katika miaka ya 80 ya karne iliyopita. Sasa miaka zaidi ya 20 imepita, shughuli hizo zimepata mafanikio ya mwanzo, vifaa vya kupikia chakula kwa nishati ya jua vinavyotumiwa kwenye mkoa huo vimefikia karibu laki 2.5. Mkoa wa Tibet unachukua nafasi ya kwanza nchini China katika matumizi ya nishati ya jua."
Vyombo vya kutumia nishati ya jua kuanza kutumiwa na wakazi wa wa kawaida mkoani Tiebt kumewawezesha wanufanike na teknolojia ya kisasa, na kuhimiza maendeleo ya shughuli za matumizi ya nishati ya jua. Meneja wa mauzo wa Kampuni ya Vyombo vya Kuongeza joto ya Maji kwa Nishati ya Jua ya Huangming bibi Ouyang Wenxia alijulisha kuwa, mwaka jana kampuni yao iliuza vifaa vya kuchemsha maji kwa nishati ya jua karibu elfu kumi kwenye mkoa wa Tibet, na wateja wao wanaongezeka siku hadi siku.
Katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya mkoa wa Tibet inatilia maanani sana shughuli za matumizi ya nishati ya jua, na imetenga fedha zaidi kwa ajili ya shughuli hizo, hasa kwa idara husika za utafiti. Hivi sasa vyombo vinavyotumiwa zaidi na watu ni vyombo vya kupikia chakula na vya kuongeza joto ya maji kwa nishati ya jua, kuhusu hali hiyo mkurugenzi wa ofisi ya maabara ya kituo cha utafiti na vielelezo vya nishati cha Tibet Bw. Tsering Norbu alisema, kituo hicho kitaendelea kutafiti matumizi mengine ya nishati ya jua. Bw. Tsering Norbu alisema,
"Taa za barabarani na kwenye viwanja vya majani zinaendeshwa kwa mwangaza wa jua, kunapokuwa na giza taa hizo zinawaka zenyewe, hata wakati wa kutokea kwa siku tano mfululizo zisizo na jua, taa hizo zinaweza kuwaka. Kwa vyombo vya kuongeza joto ya maji kwa nishati ya jua, wakati wa siku za baridi, vinaweza kutoa maji moto ya kuongeza joto nyumbani, na wakati wa siku za joto, maji moto hayo yanatumiwa katika maisha ya watu, na hata yanaweza kunywewa."
Je, lini aina mbalimbali za matumizi ya nishati ya jua kwenye kituo cha utafiti na vielelezo vya nishati cha Tibet yataenezwa kwa wakazi wa kawaida mkoani Tibet, ili kuwafanya wanufaike zaidi na nishati hiyo? Imefahamika kuwa serikali ya mkoa wa Tibet imetunga mpango wa kutimiza hali hiyo. Mtafiti wa kituo cha utafiti na vielelezo vya nishati cha Tibet bibi Yun Yan alisema, kati ya mwaka 2006 hadi mwaka 2010, serikali imepanga kujenga kituo cha kuzalisha umeme wa kilowati elfu kumi kwa nishati ya jua kwenye sehemu ya Ali kwa kutenga Renminbi Yuan milioni 600, aidha mfumo wa kupeleka umeme vijijini utaanzishwa ili kukidhi mahitaji ya umeme ya wakulima na wafugaji wanaishi kwenye sehemu za mbali.
Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya wakulima na wafugaji wanaonufaika na vyombo vya nishati ya umeme mkoani Tibet imefikia karibu laki 3, na mkoa wa Tibet umekuwa mkoa unaotumia zaidi nishati ya jua nchini China.
Idhaa ya kiswahili 2008-06-16
|