Mji wa Xiamen mkoani Fujian ulioko kusini mashariki mwa China ni mji ulio karibu zaidi na Taiwan kwenye China bara. Kutokana na maendeleo ya mawasiliano ya kiuchumi na kibiashara kati ya kando mbili za mlangobahari wa Taiwan, wafanyabiashara wengi wa Taiwan wamekwenda Xiamen kuwekeza kuanzisha makampuni yao mjini humo. Kutokana na juhudi zao za miaka mingi na maendeleo makubwa ya uchumi wa China bara, shughuli zao zimepata maendeleo hatua kwa hatua. Katika kipindi cha leo cha nchi yetu mbioni, tunawaelezea maelezo kuhusu mfanyabiashara wa Taiwan aliyeanzisha kampuni yake mjini Xiamen.
Bw. Zeng Qinzhao ni meneja mkuu wa kampuni ya elektroniki ya Doowell mjini Xiamen. Katika miaka ya 90 ya karne iliyopita, kampuni yake iliyoko huko Taiwan ilikabiliwa na matatizo ya masoko na gharama ya nguvu kazi, hivyo alianza kufiriki kuhamishia kampuni yake nje. Alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, mwanzoni mji wa Xiamen hata China bara haikuwa chagua lake la kwanza la kuanzisha kampuni yake, alisema,
"Kabla ya kufanya ukaguzi China bara, nilifanya ukaguzi nchini Philippines, Malaysia, Indonesia na Singapore. Nilifikiri kuwa mimi ni Mchina, lakini sijawahi kutembelea China bara. Hivyo wakati huo niliamua kuwa siku moja niitembelee China bara."
Baada ya kutafakari kwa mara nyingi, Bw. Zeng Qinzhao alianzisha kampuni yake mjini Xiamen. Kama ilivyo kwa wafanyabiashara wengine wa Taiwan waliowekeza mjini Xiamen, Bw. Zeng alichagua kuanzisha shughuli zake mjini humo kwa sababu wakazi wengi wa huko wanazungumza lafudhi ya Minnan, ambayo inawawezesha wafanyabiashara wa Taiwan wenye asili ya mkoa wa Fujian wajione wako nyumbani.
Sababu kubwa zaidi iliyomfanya aanzishe shughuli zake mjini humo ni mustakabali mzuri wa kibiashara wa mji huo, Bw. Zeng alisema,
"Bidhaa nyingi za kampuni yetu zinauzwa nje. Xiamen ni mji wenye bandari, ambayo inauwezesha mji huo kuwa mji muhimu unaouza bidhaa nje. Aidha, mji wa Xiamen uko karibu na Taiwan, kuanzisha kituo cha uzalishaji hapa kunarahisisha uchukuzi wa bidhaa."
Bw. Zeng bado anakumbuka vizuri matatizo mbalimbali aliyokabiliana muda mfupi baada ya kuanzisha kampuni yake mjini Xiamen. Mwanzoni mwa miaka ya 90 ya karne iliyopita, kiwango cha maisha ya watu na hali ya uendeshaji ya makampuni ya China bara bado ilikuwa nyuma. Wakati huo kutokana na hali duni ya upashanaji habari, ombi lake la kuweka simu moja kwenye kampuni yake liliidhinishwa kwa karibu nusu mwaka, tena alitumia yuan elfu kumi kadhaa kununua waya ya simu.
Lakini Bw. Zeng hakuogopa matatizo hayo. Kwa kutumia uzoefu wake mkubwa na kushikilia kazi yake, kampuni ya Bw. Zeng inapata maendeleo na faida kubwa zaidi hatua kwa hatua. Mwaka 2007 thamani ya uuzaji wa bidhaa nje wa kampuni hiyo ilikuwa karibu dola za kimarekani milioni 400.
Bw. Zeng amefanya kazi China bara kwa miaka 16. Katika miaka hiyo iliyopita, alijionea jinsi uchumi wa China bara ulivyopata maendeleo ya kasi. Anaona kuwa mafanikio ya wafanyabiashara wa Taiwan walioko China bara yanahusiana na maendeleo ya uchumi wa China bara, alisema,
"Nimegundua kuwa kasi ya maendeleo ya kampuni yetu ni karibu sawa na kasi ya maendeleo ya uchumi wa China. Hasa katika miaka mitano iliyopita, kasi ya maendeleo ya uchumi wa China iliongezeka. Hivyo unaweza kugundua kuwa makampuni ya wafanyabiashara wa Taiwan, hasa makampuni ya teknolojia za kisasa pia yalipata maendeleo makubwa."
Mafanikio ya wafanyabiashara wa Taiwan mjini Xiamen pia yanahusiana na msaada na uungaji mkono wa serikali ya mji huo. Naibu mkurugenzi wa ofisi ya mambo ya Taiwan ya Xiamen Bw. Wang Mingshui alieleza kuwa, hauachi kuwahudumia wafanyabiashara wa Taiwan hata kwa siku moja, alisema,
"Ili kuwahimiza ndugu wa Taiwan kuwekeza mjini Xiawen, na kulinda haki na maslahi yao, mwaka 1994 bunge la umma la mji wa Xiamen lilipitisha kanuni za kulinda uwekezaji wa ndugu wa Taiwan na kanuni za kushughulikia malalamiko ya ndugu wa Taiwan. Serikali ya mji huo pia ilianzisha kituo cha kushughulikia malalamiko ya ndugu ya Taiwan kwenye ofisi ya mambo ya Taiwan ili kuwahudhumia wafanyabiashara hao."
Serikali ya mji wa Xiamen pia ilianzisha utaratibu wa kufanya makongamano na wafanyabiashara wa Taiwan ili kuwasiliana na kubadilishana nao maoni. makongamano hayo yanafanyika kila baada ya nusu mwaka. Matatizo ya wafanyabiashara wengi wa Taiwan yametatuliwa mara moja kwenye makongamano hayo, hivyo wanafurahia utaratibu huo.
Hivi sasa ndugu wa Taiwan wanaowekeza mjini Xiamen wamezoea maisha yao huko. Wafanyabiashara zaidi ya 40 wa Taiwan wamepewa sifa ya wakazi wanaoheshimiwa wa mji huo. Bw. Zeng ni mmoja kati ya wafanyabaishara hao. Alisema shughuli zake zinapata maendeleo mazuri, lakini bado ana matumaini kuwa mawasiliano ya moja kwa moja ya biashara, posta na usafiri kati ya kando mbili za mlangobahari wa Taiwan yatatimizwa mapema, alisema,
"Kuzifanya kando mbili za mlangobahari wa Taiwan zijiunge barabara ili wakazi wa pande mbili waendeleza uchumi wao kwa pamoja na kuinua kiwango cha maisha yao ni suala ambalo tunatakiwa kulishughulikia. Wakati utandawazi unapoendelea duniani, ni lazima tushirikiane, ili tutapate maendeleo zaidi duniani na kuistawisha China. Wakazi wa pande mbili wakitaka kuufanya uchumi wao uwe mzuri zaidi duniani, ni lazima waboreshe haraka mawasiliano kati yao haraka."
Bw. Zeng Qinzhao pia ni mkurugenzi wa shirika la makampuni yanayowekezwa na wafanyabiashara wa Taiwan mjini Xiamen. Alisema atashirikisha wafanyabiashara wa Taiwan mjini humo, na watafanya juhudi pamoja ili kutimiza mawasiliano ya moja kwa moja ya biashara, posta na usafiri kati ya kando mbili za mlangobahari wa Taiwan.
|