Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-06-24 18:37:07    
Eneo la sayansi na teknolojia la Zhongguancun kuendeleza shughuli za kubana matumizi ya nishati na kuhifadhi mazingira

cri

Eneo la sayansi na teknolojia la Zhongguancun lilianzishwa mwaka 1988. Kwenye eneo hilo kuna makampuni zaidi ya elfu 18 ya teknolojia za hali cha juu ya China na ya nchi za nje. Mwandishi wetu wa habari alipotembelea eneo hilo, aliona mazingira mazuri na miundo mbinu iliyokamilika. Mkurugenzi wa kamati ya usimamizi ya eneo hilo Bw. Dai Wei alisema, katika miaka ya hivi karibuni, ili kujenga eneo linalohifadhi mazingira ya viumbe, eneo hilo lilichukua hatua kuboresha mazingira ya eneo hilo, kujenga miundo mbinu inayobana matumizi ya nishati na kuhifadhi mazingira, vikiwemo vifaa vya kuzalisha umeme kwa nishati ya jua, na kukarabati miundo mbinu ya zamani kwa kutumia teknolojia zinazohifadhi maingira. Bw. Dai alisema,

"Tunafanya juhudi kutumia teknolojia za matumizi ya nishati endelevu, na kubana matumizi ya nishati kwenye majengo ili kubana matumizi ya umeme. Pia tunatumia vifaa vya kisasa vya kutoa maji, kutumia tena maji yaliyotumiwa na kutumia mvua ili kubana matumizi ya maji. Tunafanya juhudi kuhifadhi mimea mbalimbali kwenye eneo hilo, kupanda miti mingi zaidi na kuongeza matumizi ya nishati endelevu."

Kujenga eneo linalohifadhi mazingira ya viumbe hakuhusiani tu na kazi hizo za kimsingi. Eneo la Zhongguancun pia limeendeleza makampuni mengi ya kisasa yanayoshughulikia teknolojia za kubana matumizi ya nishati na kuhifadhi mazingira. Kwa mfano kampuni ya teknolojia ya Originwater iliyoko kwenye eneo hilo ilivumbua teknolojia ya Membrane Bioreactor, ambayo ni teknolojia ya kisasa duniani. Kampuni hiyo inatumia teknolojia hiyo kusafisha maji taka.

Kampuni ya Tsinghua Tongfang ni kampuni kubwa inayoshughulikia teknolojia ya upashanaji habari nchini China, lakini pia inatumia teknolojia za kuhifadhi mazingira kwenye utengenezaji wa bidhaa za upashanaji habari, televisheni, kompyuta na majengo yanayosimamiwa kwa kompyuta. Ofisa mhusika wa kampuni hiyo Bw. Fan Xin alisema,

"Tunashughulikia miradi mingi ya kuondoa sulfide kwenye vituo vikubwa vya kuzalisha umeme, na tumepata maendeleo makubwa kwenye shughuli hiyo. Pia tunashughulikia miradi mingi mikubwa ya kuweka mataa ikiwemo mradi wa michezo ya Olimpiki. Wakati tunaposhughulikia miradi hiyo, tunatumia teknolojia za kubana matumizi ya nishati na kuhifadhi mazingira."

Kampuni ya Dynamic Power ya Beijing ni kampuni nyingine inayoshughulikia utengenezaji wa bidhaa zinazobana matumizi ya nishati na kuhifadhi mazingira. Vichujio vya viyoyozi vilivyovumbuliwa na kampuni hiyo si kama tu vina uwezo mkubwa wa kusafisha hewa, bali pia vinafanya kazi kwa ufanisi mkubwa na vinabana matumizi ya nishati. Vyombo hivyo inafurahiwa sana kwenye masoko na vinatumiwa na watu wengi, kwa mfano vimetumiwa kwenye ujenzi wa majengo ya kijiji cha vyombo vya habari cha michezo ya Olimpiki ya Beijing.

Habari zinasema katika eneo la Zhongguancun, kuna makampuni mengi yanayoshughulikia teknolojia za kubana matumizi ya nishati na kuhifadhi mazingira kama makampuni ya Originwater, Tsinghua Tongfang na Dyanamic Power. Hadi kufikia mwaka 2007, makampuni ya aina hiyo yaliyoko kwenye eneo la Zhongguancun yalikuwa karibu 2000. Thamani ya uzalishaji ya makampuni hayo ilikuwa yuan bilioni 80 hivi, ambayo ilichukua moja ya kumi ya thamani yote ya uzalishaji ya eneo hilo.

Mkurugenzi wa kamati ya usimamizi ya eneo hilo Bw. Dai Wei alisema kwenye eneo hilo kuna maabara nyingi za ngazi ya kimataifa na vituo vya utafiti vinavyoshughulikia teknolojia za kubana matumizi ya nishati na kuhifadhi mazingira. Robo ya rasilimali za sayansi na teknolojia husika za China ziko kwenye eneo hilo, na teknolojia nyingi mpya zimevumbuliwa kwenye eneo hilo. Hivyo eneo hilo linachukua kazi ya kujenga eneo linalohifadhi mazingira ya viumbe kuwa ni kazi muhimu zaidi katika siku za usoni.. Bw. Dai alisema,

"Katika miaka ya hivi karibuni, eneo la Zhongguancun lilipata maendeleo ya haraka kwenye shughuli za kuhifadhi mazingira na nishati. Makampuni yamepata maendeleo makubwa. Tumepanga kuendeleza shughuli za kiwango cha juu zikiwemo uvumbuzi wa teknolojia za nishati na uhifadhi wa mazingira, matumizi ya teknolojia mbalimbali kwa pamoja, na utoaji wa vifaa na huduma za uzalishaji, ili kuanzisha shughuli husika za kiwango cha juu zenye ufanisi mkubwa.

Bw. Dai alisema katika miaka kumi ijayo, eneo la Zhongguancun litachukua hatua mbalimbali zikiwemo kutunga mipango na kutoa uungaji mkono wa kifedha, ili kufanya juhudi zote kuunga mkono maendeleo ya shughuli husika.

Hivi sasa eneo la Zhongguancun limeanza kutunga mpango wa maendeleo ya shughuli za kubana matumizi ya nishati na kuhifadhi mazingira, na limetunga vigezo husika na kuchukua hatua mbalimbali za uhakikisho. Aidha eneo hilo limeamua kuanzisha miradi 10 muhimu ikiwemo miradi ya matumizi ya mvua, kubana matumizi ya nishati kwenye majengo, na kukusanya na kushughulikia takataka za bidhaa za elektroniki, na litajenga miradi mbalimbali ya vielelezo ili kusukuma mbele maendeleo ya shughuli hizo.

Licha ya hatua hizo, eneo la Zhongguancun pia limetunga kanuni za kutoa uungaji mkono wa kifedha kwa shughuli hizo. Miradi inayohusu nishati mpya, matumizi ya nishati endelevu, uhifadhi wa maliasili ya maji na kubana matumizi ya nishati utapata uungaji mkono wa kifedha ambao unaweza kufikia yuan milioni 5. Naibu mkurugenzi wa kamati ya usimamizi ya eneo hilo Bw. Li Shizhu alisema,

"Fedha hizo zitatumiwa kununua bidhaa na huduma za makampuni ya eneo la Zhongguancun. Uungaji mkono wa kifedha kwa kila mradi hautazidi asilimia 40 ya thamani ya uwekezaji wa mradi, na hautazidi yuan milioni 5."

Mkurugenzi wa kamati ya usimamizi ya eneo hilo Bw. Dai Wei alisema kubana matumizi ya nishati na kuhifadhi mazingira ni shughuli mpya. Shughuli hizo zikipata uungaji mkono wa kisera na kufuatiliwa na jamii, zitapata maendeleo ya haraka na zitakuwa na mustakabali mzuri.