Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-06-26 17:52:19    
Msanii wa utamaduni wa jadi Zhang Hai

cri

Msanii Zhang Hai wa kabila la Wadong wilayani Sanjiang katika mkoa wa Guangxi, kusini mwa China ni mwanamuziki na mtengenezaji hodari wa ala ya muziki ya kikabila iitwayo lusheng ambayo amejifunza mwenyewe. Alitembeatembea katika vijiji vingi wanakoishi Wadong kurithisha ufundi wake wa kutengeneza ala hiyo.

Lusheng ni ala ya muziki iliyotengenezwa kwa mianzi, ala hiyo imekuwa na historia ya miaka zaidi ya 2,000 nchini China na imeenea zaidi katika maeneo wanayoishi watu wa makabila madogo madogo kusini mwa China, hususan Wamiao na Wadong ambao kila wanaposherehekea sikukuu yao fulani wanapiga ala hiyo huku wakiimba na kucheza ngoma.

Bw. Zhang Hai mwenye umri wa miaka 54 alizaliwa katika kijiji cha Dudong ambacho kinasifiwa kama ni "maskani ya nyimbo". Baba yake alikuwa mwimbaji na ni hodari wa kupiga ala ya lusheng, lakini bahati mbaya alifariki dunia wakati Zhang Hai alipokuwa na umri wa mwaka mmoja tu. Bw. Zhang Hai alisema amerithi kipaji cha muziki kutoka kwa baba yake. Alisema, kwa mara ya kwanza aliposikiliza muziki wa ala ya lusheng alianza kuipenda sana ala hiyo. Alisema,

"Wakati tamasha la muziki wa lusheng lilipofanywa nilikuwa naumwa na tumbo, muziki ulinivutia sana lakini sikuweza kutoka nyumbani, nililia machozi."

Mama wa Zhang Hai alikuwa mkulima, alikuwa peke yake akiishughulikia familia yake kwa kazi ya kilimo, maisha yalikuwa ni magumu sana. Zhang Hai aliacha kwenda shuleni na kuchunga ng'ombe alipokuwa na umri wa miaka 9. Kutokana na kupenda sana kupiga ala ya lusheng kila aliporudi nyumbani kutoka malishoni alipiga ala hiyo. Mama yake alimkataza sana kwa sababu aliona ala hiyo haikuweza kusaidia chochote katika hali yao umaskini, alimtaka ashike jembe badala ya ala. Bw. Zhang Hai alijifunza kisiri siri kila alipopeleka ng'ombe malishoni.

Zhang Hai alipokuwa na umri wa miaka 14 alikuwa pamoja na wenzake kijijini walikwenda mlimani kutengeneza bwawa la maji ili apate kipato cha kusaidia familia yake, na kazi ya Zhang Hai ilikuwa ni kuwapikia wafanyakazi wenzake chakula, na wakati wa kupumzika alipiga ala ya lusheng. Alisema,

"Nilipopiga ala ya lusheng wafanyakazi wote walitega masikio. Walijiuliza, ni nani huyu anayepiga ala vizuri namna hii? Baadaye kutokana na kujulikana kwangu nilijiunga na kikundi kimoja cha wasanii na kuonesha muziki hapa na pale mkoani. Katika miaka ya 70 ya karne iliyopita utamaduni wa jadi nchini China ulikumbwa na hali mbaya, muziki wa ala ya lusheng ulikuwa nadra sana kusikika, ilimpasa arekodi muziki wa ala hiyo uliotangazwa mara chache redioni. Katika siku asipokuwa na shughuli alikuwa pamoja na vijana wenzake kwenda katika vijiji vingine kuimba "nyimbo za kuuliza na kujibu". Alisema,

" 'Nyimbo za kuuliza na kujibu' ni aina pekee ya kupendana kwa vijana wa kabila la Wadong. Katika usiku, wasichana na wavulana wanapiga ala ya lusheng, huku wakiulizana na kujibiana kwa kuimba kwa ajili ya kutafuta wapenzi wao. Muziki mzuri alioupiga Zhang Hai uliwavutia sana wasichana, ndio kutokana na uhodari huo Zhang Hai alipata mpenzi wake.

Jina la Zhang Hai lilikuwa linajulikana wilayani kadiri siku zilivyopita. Mwaka 1985 alijiunga na kundi la wasanii la wilaya ya Sanjiang na tokea hapo amepata kazi yake anayoishughulikia maishani mwake. Baadaye aliona kwamba muziki unaofaa kwa ala ya lusheng ulikuwa ni mchache, hivyo alidhamiria kutunga yeye mwenyewe. Alisema,

"Napenda kutunga muziki wa kabila langu la Wadong kwa sababu nilikulia katika familia ya kabila hilo na naelewa sana maisha ya Wadong."

Kutokana na kupiga muziki wa ala ya lusheng kwa miaka mingi aligundua kwamba ala hiyo haiwezi kutoa hisia vya kutosha. Kuanzia miaka ya 80 alianza kujaribu kuifanyia ala hiyo mageuzi. Baada ya kufanya majaribio mengi, mwishowe alifanikiwa kuigeuzia ala hiyo iliyokuwa na paipu sita za mwanzi kuwa na paipu 24. Ala hiyo baada ya kufanyiwa mageuzi inaweza kupiga muziki wa aina mbalimbali.

Bw. Zhang Hai amekuwa fundi mkubwa wa kutengeneza ala ya lusheng. Mwaka 2007 alipata tuzo ya mrithi wa utamaduni wa jadi nchini China.

Bw. Zhang Hai anapenda sana utamaduni wa kabila lake la Wadong, ana matumaini ya kwamba utamaduni huo utarithishwa kizazi baaada ya kizazi. Lakini kutokana na kumomonyolewa na utamaduni wa kisasa vijana wanaoweza kupiga ala ya lusheng wanapungua sana. Zhang Hai alisafiri kutoka kijiji kimoja hadi kingine jumla vijiji 15 wilayani akifundisha ufundi wake wa upigaji wa ala ya lusheng.

Kwa sababu karibu wenyeji wote wanamfahamu, kila afikapo anakaribishwa kama mgeni wa heshima. Aliwaongoza wanafunzi wake wadogo kwenda vijijini kupiga muziki kwa ala ya lusheng, na wazazi wengi walichukua watoto wao kwenda kusikiliza na kumtaka awafundishe watoto wao. Zhang Hai alisema,

"Sasa wanafunzi wangu wamekuwa na msingi mzuri wa upigaji, niliwaambia wafundishe wengine baada ya mimi kuondoka humu duniani ili ala hiyo ya kabila letu iweze kupigwa kizazi baada ya kizazi."

Binti na mpwa wa Zhang Hai walianza kujifunza upigaji wa ala ya lusheng walipokuwa na umri wa miaka 7. Sasa watu wa familia yake mara kwa mara wanafanya maonesho ya muziki huku na huko wakiwafurahisha wenyeji kwa utamaduni wa kabila lake la Wadong.