Kabila la Wali ni moja kati ya makabila yenye historia ndefu zaidi katika sehemu za kusini mwa China, idadi ya watu wake ni zaidi ya milioni 1.3, na watu hao hasa wanaishi kwenye kisiwa cha Hainan kilichoko kusini mwa China.
Wilaya ya Baoting iko kwenye umbali wa kilomita karibu 260 kutoka Haikou, mji mkuu wa mkoa wa Hainan. Katika wilaya hiyo kuna miti mingi na hali nzuri ya hewa. Kati ya idadi ya watu laki 1.6 ya wilaya hiyo, watu wa kabila la Wali ni karibu laki moja. Bw. Gao Yunliang mwenye umri wa miaka 76 anaishi kwenye kijiji cha Tongzha cha tarafa ya Jiamao ya wilaya hiyo, na yeye ni fundi mwashi maarufu wa kujenga nyumba. Wakati alipokuwa kijana, kazi yake ilikuwa ni kujenga nyumba za jadi za kabila la Wali kwa nyasi zilizokauka. Nyumba hizo ndogo za nyasi zinajulikana kama nyumba za mashua, kwa kuwa umbo la nyumba hizo linafanana na mashua iliyowekwa chini juu. Wataalamu wa ujenzi wanasema nyumba hiyo imeonesha busara ya watu wa kabila la Wali, kwani ingawa zinajengwa kwa malighafi rahisi, lakini ina umaalumu mwingi: nyumba hizo ni kubwa, na mapaa yake yako chini. Ili kuzuia upepo na mvua kubwa zinazotokea mara kwa mara mkoani Hainan; nyumba hizo zinagawanyika katika sehemu mbili na kuwa na milango miwili, katikati ya nyumba hiyo kuna nguzo tatu kubwa zaitwazo "Gee", nguzo hizo ni alama ya wanaume, na kando ya nguzo hizo tatu kubwa, kuna nguzo sita dogo zaitwazo "Geding", ambazo ni alama ya wanawake. Wakati watoto wanapokua na kuwa watu wazima, watajenga nyumba nyingine karibu na nyumba za wazazi wao.
Hivi sasa familia ya Bw. Gao Yunliang imeacha nyumba ya nyasi, na wanaishi kwenye nyumba yenye ghorofa mbili ambayo eneo lake ni mita za mraba zaidi ya mita tatu. Bw. Gao Yunliang alisema,
"Nilipokuwa kijana nilikwenda nje mara chache tu. Nilikuwa fundi wa kujenga nyumba za nyasi, na kazi yangu ilikuwa kuwaelekeza wanakijiji wenzangu kujenga nyumba yenye umbo la mashua. Lakini sikujua kujenga nyumba kwa kutumia saruji na chuma. Sasa mimi nina umri mkubwa, ni nadra kufanya kazi ya kilimo. Watoto wangu wanafanya kazi kwa bidii na kupata pesa za kujenga nyumba hizo kubwa, naona nyumba hii ni nzuri."
Nyumba hiyo kubwa ilijengwa na mtoto wake Gao Jinfeng kwa gharama ya Yuan za Renminbi laki mbili. Mwaka 2000, Bw. Gao Jinfeng alijifunza ufundi wa kupanda miti ya matunda na mboga, halafu alianzisha bustani ya miti ya matunda. Sasa kwenye bustani yake, kuna miti ya matunda karibu 700. Alisema mwaka wa nne tangu miti hiyo ipandwe, matunda yalianza kupatikana, na alipata mapato ya yuan zaidi ya elfu 40. Akiwa mtu wa kwanza aliyejifunza ufundi wa kupanda miti ya matunda Bw. Gao Jinfeng amenufaika sana, alisema,
"Pesa za kujenga nyumba hii hasa zilitokana na mauzo ya matambuu, na nyingine zilipatikana kutokana na mauzo ya matunda, mboga, nafaka na nyama ya nguruwe waliofugwa na mke wangu. Saa tunapata mapato mazuri, katika robo ya kwanza ya mwaka huu, tumepata yuan kati ya elfu saba na nane, na mwaka jana kwa kuuza matambuu tu, tulipata yuan karibu elfu kumi."
Familia ya Gao Jingfeng ni moja kati ya familia kubwa katika kijiji cha Tongzha, na kuna watu karibu 20. Licha ya watoto wake watatu, pia anawatunza watoto wengine 6 yatima. Zamani familia hiyo haikuwa na bustani ya miti ya matunda, waliwatunza watu hao wengi kwa mapato ya kilimo. Mke wa Bw. Gao Jinfeng bibi Ji Meilian alijifunza kufuga nguruwe kutoka kwa watu wa kabila la Wahan ili kumudu maisha ya familia yake kubwa, kila siku aliamka mapema, kuandaa chakula na kuwalisha nguruwe, na kufanya kazi za kilimo kwenye shamba. Sasa watoto wake wamekuwa watu wazima, na wameanza kumsaidia bibi Ji Meilian kufanya kazi. Kutokana na kuwalea watoto yatima, na kuwatendea wazazi wake vizuri, mwaka 2007 bibi Ji Meilian alipewa heshima ya mfano mzuri wa maadili mkoani Hainan.
Watu wa kabila la Wali wanapenda kuimba. Wakati wanapofanya kazi mashambani, kufanya harusi na mazishi, na kuwakaribisha wageni, wanaimba nyimbo ili kuonesha hisia zao. Kila wakati wa sikukuu ya mwaka mpya, nyimbo zinasikika hapa na pale kwenye sehemu za kabila la Wali, na wakati huo watoto wa familia ya Gao Yunliang walioko nje pia wanarudi nyumbani ili kusherehekea sikukuu kwa pamoja. Huu ni wakati wa furaha kubwa kwa Bw. Gao Yunliang. Alisema,
"Tutanunua fataki na vitu vingine vya kusherehekea mwaka mpya, kama watu wa kabila la Wahan wanavyofanya. Familia yetu ni kubwa, tunachinja nguruwe na kutengeneza pombe sisi wenyewe. Watoto wanaofanya kazi kwenye sehemu za nje wanarudi na kukusanyika nyumbani. Siku ya pili ya sikukuu ya mwaka mpya tutakwenda kuwatembelea jamaa na marafiki zetu, ambapo jamaa na marafiki hao pia watatutembelea wakiwa na zawadi nyingi, na tunawaandalia chakula kizuri."
Hivi sasa maisha ya watu wa kabila la Wali yameboreshwa sana kuliko yale ya zamani, watu wanaofanya kazi kwenye sehemu nyingine wanaongezeka, na wamepanua upeo wao. Ofisa wa kabila la Wali wa tarafa ya Jiamao Bw. Lin Kaixue alisema ili kuwahimiza watu wa makabila madogo madogo kufanya kazi za vibarua mijini, serikali ya sehemu hiyo ilitenga fedha maalumu ili kuwapa mafunzo husika. Alisema,
"Watu wengi wanafanya kazi za vibarua mjini Guangdong. Kazi za vibarua mkoani Hainan ni za muda mfupi. Wakulima wakimaliza kazi zao za kilimo, watakwenda nje kutafuta kazi za muda za kupanda matunda kwa watu wengine, na hata baadhi yao wanakwenda pwani kujifunza uvuvi. Sasa serikali inatoa mafunzo kwa watu wanaotaka kufanya kazi za vibarua, na inatenga fedha maalumu kwa ajili ya mafunzo hayo."
|