Vileta bahati vya michezo ya Olimpiki ya Beijing ni Fuwa watano, na Fuwa mmoja aitwaye Jingjing, sura yake inayopendeza ilisanifiwa kutokana na Panda mmoja mwenye jina hilo hilo anayeishi mkoani Sichuan, kusini magharibi mwa China. Panda ni wanyama adimu ambao wako kwenye hatari ya kutoweka, wanapatikana nchini China tu. Katika kituo cha kuwatunza Panda mkoani Sichuan, kijana Shi Bin anabeba jukumu la kumtunza Panda Jingjing. Hivi karibuni kijana huyo aliteuliwa kuwa mkimbiza mwenge wa michezo ya Olimpiki ya Beijing, alisema atatumia nafasi hiyo kueneza mtizamo wake kuhusu michezo ya Olimpiki isiyochafua mazingira.
Kijana Shi Bin alihitimu kutoka Chuo kikuu cha kilimo cha Sichuan mwaka 2004, na kupata ajira kwenye kituo cha kuwatunza panda cha Sichuan. Kazi aliyopewa ni kuwatunza Panda wachanga. Mbali na kuwalisha Panda, kusafisha mizizi na kuondoa kinyesi, kazi muhimu ya kijana huyo ni kucheza na Panda na kuweka kumbukumbu kuhusu hali ya afya zao. Kazi ni nyingi, hata hivyo kijana Shi Bin haoni uchovu, na upendo mkubwa kwa Panda umejengeka moyoni mwake. Alisema "Panda ni alama ya shughuli za uhifadhi wa mazingira nchini China na hata duniani. Natambua umuhimu mkubwa wa kazi yangu ya kuwalea Panda wachanga mpaka wawe wakubwa. Ninajivunia kufanya kazi ya kuwatunza Panda."
Panda Jingjing alizaliwa mwaka 2005, na Shi Bin alipewa kazi ya kumtunza mwaka huo. Familia ya Panda Jingjing ina uhusiano wa karibu na michezo. Mama yake Yaya alizaliwa mwaka 1990 michezo ya Asia ilipofanyika mjini Beijing, baba yake Kobe alipewa jina hilo na mwenyekiti wa heshima wa kamati ya Olimpiki ya kimataifa Bw. Juan Antonio Samaranch, na Kobe mwenyewe alikuwa ni kileta bahati cha michezo ya Olimpiki ya Barcelona ya mwaka 1992.
Shughuli za kuwachagua wakimbiza mwenge wa michezo ya Olimpiki ya Beijing zilipoanza mwezi Juni mwaka 2007, Bw. Shi Bin akiwa ni mtunzaji wa Panda Jingjing aligombea nafasi hiyo. Alisema "Nilishiriki kwenye shughuli hizo nikilenga kutumia nafasi hii kueneza uhifadhi wa Panda."
Kwenye shughuli hizo, kutokana kuwa mtunzaji wa Panda Jingjing na kuwa na uchangamfu mkubwa kwa michezo ya Olimpiki, Bw. Shi Bin alifaulu mitihani mbalimbali na kuingia kwenye fainali zilizofanyika hapa Beijing. Mwezi Agosti ni kipindi cha kujifungua kwa Panda, ambapo kijana Shi Bin amekuwa na pilikapilika nyingi. Hata hivyo kiongozi wake Bw. Huang Xiangming alikubali kijana huyo ajiandae na uteuzi wa wakimbiza mwenge bila kuja kazini. Bw. Huang alisema "Tulimpa nafasi ya kujiandaa na shughuli za kuchaguliwa kuwa wakimbiza mwenge, tulimwunga mkono ashiriki kwenye shughuli hizo."
Bw. Shi Bin alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, gharama za kumtunza Panda mmoja huwa ni Yuan elfu 50 hivi kwa mwaka. Hivi sasa idadi ya Panda inaongezeka kwenye kituo hicho, inahitaji viwanja vingi zaidi kwa Panda kucheza na fedha nyingi zaidi za kufanya utafiti. Ndiyo maana anataka watu wengi zaidi wachangie shughuli za kuwatunza Panda. Katika shughuli hizo, alichukua picha nyingi za Panda Jingjing na vijitabu vya ujuzi wa kuhifadhi Panda, aliwapa wengine picha na vijitabu hivyo kama zawadi. Zaidi ya hayo akipata nafasi, alieleza mara kwa mara umuhimu wa kuhifadhi Panda na kujibu maswali mbalimbali kuhusu shughuli hizo. Kijana Shi Bin alisema "Nilipokuwa mjini Beijng, watu wengi walipofahamishwa kuwa mimi ninafanya kazi ya kuwatunza Panda, waliniuliza maswali mengi kuhusu Panda. Niliwajibu kwa makini, nikiwaelimisha ujuzi kuhusu uhifadhi wa Panda."
Hivi sasa kijana huyo Shi Bin amechaguliwa kuwa mkimbiza mwenge, alisema kutokana na kuwa Panda amemsaidia kutimiza ndoto ya kushiriki kwenye michezo ya Olimpiki, kwa hiyo anapaswa kutumia fursa hiyo ya kuwa mkimbiza mwenge kuwahamasisha watu wengi zaidi wafuatilie uhifadhi wa Panda na kuwasaidia Panda. Hivi sasa kijana huyo anawaalika mara kwa mara wakimbiza mwenge na walinzi wa mwenge wajitolee kufanya kazi katika kituo cha kuwatunza Panda, na kuwaalika wanafunzi watembelee kituo hicho. Alisema "Kwenye shughuli za kuwachagua wakimbiza mwenge, tulipewa mtihani wa kila mmoja atunge kauli mbiu ya kuelezea kwa nini anataka kuteuliwa kuwa mkimbiza mwenge. Nilichoandika ni 'hifadhi mazingira ya asili na kuwatunza Panda'. Nina matumaini kuwa kutokana na shughuli hizo za uteuzi, watu wengi zaidi watajitokeza katika kuwafuatilia, kuwatunza na kuwahifadhi Panda."
Bw. Shi Bin alisema anaisubiri kwa hamu kubwa siku ambayo mwenge wa michezo ya Olimpiki utakimbizwa mkoani Sichuan, na anatiwa moyo kila anapotazama mabango mbalimbali yaliyowekwa kando za barabara ya kuhesabu siku zilizobaki kabla ya kufunguliwa kwa michezo ya Olimpiki ya Beijing. Hivi sasa mbali na kazi ya kila siku, anafanya mazoezi ya kujenga mwili, kwani anapenda kuonesha sura yake nzuri atakapokimbiza mwenge wa michezo ya Olimpiki.
|