Eneo la uendelezaji wa uchumi la Yangpu liko kwenye peninsula ya Yangpu kaskazini magharibi mwa mkoa wa Hainan, na pia liko kando ya mlango bahari wa Qiongzhou na ghuba ya Beibu, kadhalika eneo hilo liko kwenye njia muhimu ya usafirishaji kati ya Singapore, Hongkong Shanghai na Osaka, hivyo ni sehemu muhimu inayounganisha Asia ya Kusini mashariki na Mashariki ya Kati.
Kutokana na kuwa na bandari nzuri ya kimaumbile na kuwa kwenye sehemu muhimu ya kijiografia, mji wa Yangpu unafuatiliwa mara kwa mara. China ilitunga mpango wa kujenga bandari huko Yangpu kabla ya mkoa wa Hainan kuanzishwa. Na baada ya mkoa huo kuanzishwa, mji huo umekuwa mji muhimu katika kutekeleza mpango wa mageuzi na ufunguaji mlango mkoani humo.
Mwanzoni mwa miaka ya 90 karne iliyopita, uwekezaji wa kupita kiasi kwenye ujenzi wa nyumba ulifanyika kwenye sehemu mbalimbali mkoani Hainan, ukiwemo mji wa Yangpu. Mwaka 1993 China ilitoa sera ya udhibiti na marekebisho ya uchumi kwa ujumla, na uwekezaji wa kupita kiasi ulizuiliwa, na maendeleo ya mji huo yalikwama kwa miaka 10. Mkurugenzi wa ofisi ya mipango ya ujenzi ya idara ya usimamizi wa eneo la uendelezaji wa uchumi la Yangpu Bw. Zhang Jin alisema,
"Wakati huo watu wengi walisema mji huo haukupata maendeleo, shughuli zote za uwekezaji zilisimamishwa, kwani wafanyabiashara wa nje hawafanyi tena mipango zaidi ya shughuli zao kwenye mji huo. Barabarani kulikuwa na watu wachache na magari machache, na kulikuwa na ng'ombe na mbuzi wengi."
Katika miaka zaidi ya 10 iliyopita, ingawa uchumi wa mji wa Yangpu ulikwama kwa muda, lakini mkoa wa Hainan haukuacha kuendeleza mji huo. Tangu mwaka 2002, mkoa huo uliamua kufuata njia ya kuendeleza mji huo inayoongozwa na serikali, pia ulitoa mkakati wa kuhimiza maendeleo ya mji huo kwa kutegemea makampuni makubwa na miradi mikubwa, na unatekeleza sera mbalimbali za kuwavutia wafanyabiashara na uwekezaji, ambazo zimeleta mabadiliko makubwa na ustawi mjini humo, Bw. Zhang alisema,
"Mipungate na mawe ambayo yalionekana hapa na pale zamani yamepungua, miundo mbinu imeboreshwa. Aidha, uchumi unakua kwa kasi kubwa mwaka hadi mwaka."
Habari zinasema kuanzia mwaka 2004 hadi mwaka jana, thamani ya uzalishaji mai ya mji wa Yangpu iliongezeka na kufikia yuan bilioni 7.4 kutoka yuan bilioni 1.9, na thamani ya biashara ya nje iliongezeka na kufikia dola za kimarekani bilioni 4 kutoka dola za kimarekani milioni 470.
Mkurugenzi wa idara ya usimamizi wa eneo la uendelezaji wa uchumi la Yangpu Bw. Ding Shangqing alisema, mwaka jana thamani ya uzalishaji wa viwanda ya eneo hilo ilichukua karibu asilimia 40 ya thamani ya uzalishaji ya mkoa wa Hainan, na thamani ya biashara ya nje ya eneo hilo inachukua karibu asilimia 60 ya mkoa huo. Hii inaonesha kuwa, Yangpu kimsingi umekuwa mji wenye maendeleo makubwa ya viwanda mkoani humo, ambao unasukuma mbele uchumi wa mkoa huo, Bw. Ding alisema,
"Mji wa Yangpu unachukua moja ya elfu moja ya eneo la mkoa wa Hainan, lakini ni chanzo cha karibu asilimia 40 ya thamani ya uzalishaji mali wa viwanda mkoani humo. Kiasi hicho huenda kitaendelea kuongezeka, ambacho na huenda kitafikia asilimia 50 hadi 60 katika miaka mitatu ijayo, na kufikia asilimia 70 hadi 80 katika miaka mitano hadi kumi ijayo."
Bw. Ding Shangqing alisema tangu mji huo uanzishe eneo la uendelezaji wa uchumi, umetenga yuan bilioni 6.8 kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu na majengo ya huduma, yakiwemo barabara, majengo ya kutoa maji na magati. Miundo mbinu na majengo ya huduma yanayokamilika yamekuwa jambo muhimu linalowavutia wawekezaji.
Katika miaka ya karibuni, shughuli za kuwavutia wafanyabiashara na uwekezaji mjini Yangpu zimepata maendeleo makubwa. Hivi sasa miradi ya viwanda ambayo inajengwa au imeanza kufanya kazi imefikia 30. Viwanda vya utengenezaji wa karatasi, kemikali za mafuta na gesi na uzalishaji wa umeme kimsingi vimeanzishwa. Mradi wa kusafisha mafuta uliowekezwa na kampuni ya kemikali za mafuta ya China, mradi wa kutengeneza rasilimali za kutengeneza karatasi unaowekezwa na kampuni ya utengenezaji wa karatasi wa Jinahai ya Indonesia na kiwanda cha kuzalisha umeme kwa gesi cha Yangpu ni miradi mikubwa inayojengwa mjini humo.
Mwezi Septemba mwaka jana, eneo la uendelezaji wa uchumi la Yangpu liliamuliwa kuwa bandari ya nne inayotekeleza sera ya ushuru yenye unafuu nchini China baada ya Shanghai, Tianjin na Dalian. Jambo hilo limesaidia maendeleo ya mji wa Yangpu. Bw. Ding Shangqing alisema,
"Jambo hilo limeongeza nguvu ya mji wa Yangpu. Katika miezi sita iliyopita tangu kuanzishwa kwa bandari hiyo inayotekeleza sera ya ushuru yenye unafuu, shughuli za kuwavutia wafanyabiashara zitaendelezwa vizuri."
Mkurugenzi wa ofisi ya maendeleo ya uchumi ya idara ya usimamizi wa eneo la uendelezaji wa uchumi la Yangpu Bw. Guo Zhao alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, wafanyabiashara wa nje wanafuatilia zaidi mji wa Yangpu, alisema,
"Mwanzoni tulipanga kujenga eneo la uendelezaji wa uchumi linalofungua mlango. Lakini zamani wafanyabiashara wengi wa nje walipokuja hapa, waligundua kuwa hali ya hapa bado haikufaa kwa uwekezaji, hivyo hawakuanzisha shughuli zao hapa. Lakini hivi sasa hali hiyo imebadilika, makampuni mengi ya kimataifa yanafuatilia sana mji wa Yangpu na kushiriki kwenye uwekezaji wa hapa."
Habari zinasema bandari inayotekeleza sera ya ushuru yenye unafuu linajengwa kwa vipindi vitatu. Inakadiriwa kuwa ujenzi wa kipindi cha kwanza utakamilika mwezi Oktoba mwaka huu. Bw. Ding Shangqing alisema, mji wa Yangpu utaendeleza kituo cha usafirishaji wa bidhaa za mafuta na kemikali. Ana imani kubwa kuhusu maendeleo ya mji huo katika siku za usoni, alisema,
"Hivi sasa ni kipindi kizuri zaidi kwa maendeleo ya mji wa Yangpu, pia ni kipindi chenye fursa nyingi. Tukiwa ni wakazi wa Yangpu, tuna imani kubwa kuhusu mji huo. Tunaamini kuwa baada ya juhudi za miaka mitatu hadi mitano ijayo, mji wetu utakuwa mji wenye maendeleo makubwa ya viwanda mkoani Hainan, na kuwa kielelezo cha utekelezaji wa sera ya mageuzi na ufunguaji mlango mkoani humo."
|