Sanaa ya picha za Puhui za mwaka mpya wa jadi wa China katika mji wa Gaomi mkoani Shandong imekuwa na historia ya miaka zaidi ya 500. Sanaa hiyo ilipita vipindi tofauti vya ustawi, picha hizo ziliwahi kuwa bidhaa zilizonunuliwa sana lakini baadaye hali ya sanaa hiyo ilididimia. Katika miaka ya hivi karibuni, wasanii wa picha hizo wameifufua sanaa hiyo kwa kufanya juhudi nyingi.
Gaomi ni mji wenye utamaduni mkubwa kutokana na kuwa na historia ya miaka zaidi ya 2,200, sanaa kama ufinyanzi wa sanamu, picha za kukatwa kwa karatasi na picha za Puhui za sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China zinasifiwa kuwa ni "sanaa za aina tatu za ajabu". Mwaka 2006 sanaa ya picha za Puhui za mwaka mpya wa jadi wa China mjini Gaomi iliwekwa kwenye orodha ya mali za taifa za urithi wa utamaduni usioonekana nchini China.
Picha za Puhui ni sanaa ya aina kipekee ya uchoraji, katika sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China watu wananunua picha za aina hiyo na kubandika nyumbani kwa matumaini mema. Katika miaka mingi ya maendeleo, sanaa hiyo imekuwa na mitindo tofauti ambayo kila mtindo una sifa yake, na mtindo wa picha za Puhui unapendeza zaidi kati ya mitindo yote. Kuna masimulizi mengi kuhusu historia ya kupatikana kwa picha za Puhui, mwelezaji wa jumba la makumbusho la mji wa Gaomi alisema sanaa hiyo ilipatikana katika karne ya 13. Alisema,
"Kwa mujibu wa masimulizi ya wazee, sanaa hiyo ilianza kutokea katika Enzi ya Yuan ambayo ilikuwa toka mwaka 1206 mpaka 1368 nchini China, wakati huo picha za Puhui zilichorwa kwa ajili ya kuwakumbuka mababu, na kila picha ilikuwa kubwa. Hiki ni chanzo cha sanaa ya picha za Puhui."
Mkuu wa jumba hilo Bw. Wang Dong alisema, sanaa hiyo ilikuwa inafahamika sana katika Enzi ya Qing, karne ya 17. Alisema,
"Sanaa hiyo ilirithishwa kizazi hadi kizazi na ilipokuwa mwishoni mwa Enzi ya Qing ilikuwa ikifana. Kwa mujibu wa kumbukumbu za wilaya ya Gaomi, picha hizo zilikuwa sehemu isiyoweza kukosekana katika maisha ya wakazi wa mji wa Gaomi."
Bila kujali kama maelezo gani ni sahihi, lakini yote yameonesha kuwa sanaa hiyo ina historia ndefu na ni muhimu katika maisha ya watu. Wataalamu wanaona kuwa sanaa ya picha za Puhui ni kama sanaa nyingine, kwamba ni lazima ziendane na wakati, zinapaswa kuonesha mada tofauti katika nyakati tofauti za kihistoria. Katika historia mjini Gaomi yaliwahi kutokea maduka mengi ya kuuza picha hizo, na biashara ilistawi. Katika majira ya baridi ambapo watu walikuwa hawana shughuli za kilimo wafanyabiashara walifika kwa wingi mjini Gaomi kununua picha hizo na kuziuza mahali pengine, hususan kusini mwa China.
Sababu ya kuuzwa haraka kwa picha za Puhi mjini Gami ilikuwa ni namna ya zilivyotengenezwa na mtindo wake. Wasanii wanatumia makaa ya kijiti cha mti kuchora rasimu ya picha, kisha wanatumia brashi ya wino kufuatisha michoro na kuchonga michoro hiyo kwenye mbao na kuchapisha kwa karatasi iliyofunikwa juu ya mbao hiyo baada ya kupakwa wino. Kazi ya kukamilisha picha hiyo ni ngumu, naibu mwenyekiti wa Shirikisho la Wasanii wa Uchoraji mkoani Shandong Bw. Shan Yinggui alisema,
"Kutokana na matengenezo yake yasiyo ya kawaida, sanaa ya ya picha za Puhui ina tofauti na mitindo mingine."
Sanaa ya picha za Puhui ilipokuwa katika kipindi cha ustawi iligawanyika katika aina mbili, moja ni ya jadi na nyingine ni ya mchanganyiko wa mitindo mingine na kuwa picha za kuvutia kwa rangi zake. Profesa wa Chuo Kikuu cha Sanaa ya Uchoraji cha China Bw.Bo Songnian alisema,
"Tofauti na picha za aina nyingine za mwaka mpya wa jadi wa China ni kwamba picha hizo zimekuwa kama picha za jadi za Kichina zilizochorwa kwa brashi ya wino, na kuonesha mambo yanayofurahisha wakulima."
Katika miaka ya 30 ya karne iliyopita sanaa ya picha za Puhui za mwaka mpya wa jadi wa China ziliwahi kuwa katika hali duni kwa sababu uchapaji wa picha kwa mashine wakati huo ulikuwa umestawi, hali hiyo ikiwa pamoja na wasanii kutokuwa na hamu ya kushughulika na sanaa hiyo kutokana na vurugu za vita, biashara ya picha hizo ilikuwa inafifia. Msanii wa sanaa hiyo Zhang Chuhua alisema,
"Hali ya sanaa hiyo ilitegemea kadiri wakulima wanavyoipenda, wakipenda inastawi, wasipoipenda inafifia."
Katika muda wa miaka ya 30 hivi kutokana na uchumi wa China kuendelea kwa kasi, tabia ya wananchi wa China kubandika picha hizo nyumbani wakati wa mwaka mpya wa jadi wa China imebadilika, wananunua picha hizo kwa ajili ya kumbukumbu badala ya kubandika. Na ili kustawisha sanaa ya picha za Puhui, serikali na makundi yasiyo ya serikali yalifanya juhudi nyingi. Mkuu wa Idara ya Utamaduni ya Mji wa Gaomi Bw. Gao Yuanxing alisema katika zama za leo kazi ya kurithi sanaa hiyo ni muhimu sana. Alisema,
"Idara ya Utamaduni ya Mji wa Gaomi imekusanya nguvu nyingi kuokoa sanaa hiyo. Hivi sasa kazi ya kuchapisha kitabu kinachoeleza sanaa ya picha za mwaka mpya wa jadi wa China iko karibu kukamilika."
Katika miaka ya hivi karibuni sanaa hiyo imeanza kufundishwa katika shule za msingi na sekondari. Profesa Bo Sonnian alisema utamaduni usioonekana unafungamana moja kwa moja na shughuli za watu, kama utamaduni fulani wa kiasili ukikosa warithi, utamaduni huo utatoweka na hauna tena uhusiano na maisha ya watu. Bahati nzuri sanaa ya picha za Puhui imepata nguvu ya uhai. Alisema,
"Sanaa ya picha za Puhui ni ya jadi, lakini bado inafungamana na maisha ya leo, kwa hiyo mustakbali wake utakuwa mzuri."
Idhaa ya kiswahili 2008-07-10
|