Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-07-10 17:11:22    
Utamaduni wa kabila la waQiang la China utarudi tena

cri

Tarehe 12 Mei, tetemeko kubwa la ardhi lilitokea mkoani Sichuan China. Tetemeko hilo licha ya kusababisha watu wengi kupoteza maisha na kujeruhiwa, pia lilileta hasara kubwa ya mali ya urithi wa utamaduni na utamaduni usioonekana. Baadhi ya watu wanaofundisha utamaduni wa kikabila walikufa, majumba mengi ya makumbusho yaliporomoka, na uharibifu huo ni mkubwa zaidi katika sehemu wanazoishi watu wa kabila la Waqiang na makabila mengine madogo madogo nchini China. Katika pilikapilika za kujenga upya sehemu hizo serikali za mitaa na wataalamu husika wanatilia sana maanani kuhifadhi na kurudisha utamaduni wa jadi wa kikabila.

Mliosikia ni muziki wa filimbi uliopigwa na msanii Bw. He Wangquan wa kabila la Waqiang.

Kabila la Waqiang lina historia ya miaka 3,000. Katika zama za kale, watu wa kabila hilo walikuwa wanaishi katika sehemu ya kaskazini-magharibi ya China, na baadaye walihamia mkoani Sichuan, kusini magharibi mwa China. Watu wa kabila hilo wamezoea kuishi katika majumba ya mawe yanayojengwa kwenye kwenye sehemu ya kati ya milima, ndio maana watu wanasema, ni "kabila la watu wanaoishi mawinguni". Majumba yao yanayojengwa kama ngome, ni aina ya kipekee duniani. Mapambo yao ya mavazi, ngoma zao na ala zao za muziki pia hazipatikani mahali pengine. Hivi sasa kabila la Waqiang lina watu zaidi ya laki tatu na wengi wao wanaishi katika sehemu ambazo zilikumbwa na maafa makubwa zaidi ya tetemeko la ardhi lililotokea tarehe 12 Mei. Tetemeko la ardhi lenye nguvu ya 8 kwenye kipimo cha Richter liliharibu makazi yote ya kabila la Waqiang, msanii He Wangquan alinusurika kwa bahati, marafiki na wenzake wote walikufa na data za muziki pia zimepotea kabisa. Alisema

"Makazi yetu yaliyojengwa kama ngome yalibomoka, vitu vingi vya kale ndani ya majumba ya makumbusho viliharibika, na data nyingi za muziki na ngoma za kabila letu zilifukiwa kwenye ya kifusi, jumba la utamaduni la wilaya ya Wenchuan liliporomoka na wafanyakazi wote walikufa, wao ni marafiki zangu, tulizoeana sana na mara kwa mara tulikuwa tunafundishana ufundi wa kisanaa."

Majumba mawili ya makumbusho ya utamaduni wa kabila la Waqiang katika wilaya ya Beichuan na Maoxian yaliharibika vibaya, vitu vya kale vyenye thamani kubwa zaidi ya 400 na data zilizokusanywa kwa muda mrefu zilifukiwa kwenye kifusi. Majengo pamoja na madaraja ya kabila la Waqiang yalitoweka ndani ya dakika chache tu. Watu wa kabila la Waqiang hawana lugha ya kuandikwa, utamaduni wa kabila hilo unategemea wazee kufundisha kizazi hadi kizazi, na sasa hakuna uhakika ni wazee wangapi bado wako hai ambao wanafahamu historia ya utamaduni wa waqiang.

Bw. He Changquan anayejishughulisha na kazi za kuhifadhi na kuenzi utamaduni wa kabila lake. Alitengeneza mwenyewe filimbi ya kabila la Waqiang. Filimbi hiyo ina kama penseli, na mwanzi unaotengenezwa kwa filimbi hiyo lazima upatikane kwenye mlima wenye urefu wa mita zaidi ya mita 3,000 juu ya usawa wa bahari na kusuguliwa suguliwa kwa mikono baada ya kurowekwa ndani ya mafuta ya kupikia kwa miezi kadhaa, ufundi wa kutengeneza filimbi hiyo ni mkubwa. Licha ya kutengeneza filimbi pia anashughulika na kukusanya muziki wa filimbi na kufundisha muziki wa filimbi katika shule za msingi na sekondari. Hivi sasa ametilia maanani zaidi kukusanya muziki wa kabila lake ili aurithishe kwa kizazi kijacho.

Kama ilivyo kwa Bw. He Wangquan, serikali ya China na wataalamu wa mali za urithi wa utamaduni pia wamekuwa wakijitahidi kuokoa utamaduni wa kabila la Waqiang. Tarehe 24 Mei katika sehemu zilizokumbwa na maafa ya tetemeko la ardhi waziri mkuu Bw Wen Jiabao alipozungumza na waandishi wa habari wa nchini China na nchi za nje alisema, utamaduni mkubwa wa kabila la Waqiang unapaswa kuhifadhiwa. Naibu mkurugenzi wa Kituo cha Taifa cha Hifadhi ya Utamaduni Usioonekana Bw. Zhang Qingshan alisema hivi sasa pande zote husika zinafanya juhudi kadiri ziwezavyo kupunguza hasara zilizotokea kwenye utamaduni wa kabila la Waqiang. Alisema,

"Toka mwanzo tumekuwa na fikra ambazo licha ya kuwapangia wenyeji maisha pia tunapaswa kuhifadhi mali za urithi wa utamaduni. Wazee walitutoka pamoja na utamaduni mwingi waliourithi, hili ni jambo ambalo hatuna uwezo wa kulizuia, tunachoweza sasa ni kupunguza hasara kadiri tuwezavyo."

Siku chache tu baada ya tetemeko la ardhi kutokea, Idara Kuu ya Vitu vya Kale ya China ilituma wataalamu kwenda huko kutathmini uharibifu wa vitu na majengo ya kale, Wizara ya Utamaduni ya China iliwashirikisha wataalamu kujadili namna ya kurudisha utamaduni wa kabila la Waqiang na Shirikisho la Wasanii pia lilituma kikundi cha kufanya uchunguzi kuhusu hali ya uharibifu wa mali za urithi wa utamaduni wa kabila la Waqiang na kufahamu ni wazee wangapi bado wapo na kuandaa mpango wa ukarabati kama ni ushauri kwa serikali. Naibu mkurugenzi wa Kituo cha mali za urithi wa utamaduni usioonekana Bw. Zhang Qiangshan alisema ukarabati ni lazima ufanyike kwa kuheshimu utamaduni wa asili wa kabila la Waqiang. Alisema,

"Uharibifu uliosababishwa na tetemeko la ardhi ni mkubwa, vijiji vipya vinatakiwa kujengwa kwa kulingana na utamaduni wa kabila la Waqiang, hili ni jambo ambalo lazima lizingatiwe kabla ya kuanza kujenga."

Hivi karibuni serikali ya China imetangaza "Sheria ya Ukarabati katika Wilaya ya Wenchuan baada ya Tetemeko la Ardhi". Sheria hiyo inasema ni lazima ukarabati uheshimu na kutunza utamaduni wa jadi wa kikabila. Naibu waziri wa utamaduni Bw. Zhou Heping alisema,

"Wizara ya Utamaduni imeanzisha shughuli za kuhifadhi utamaduni wa kabila la Waqiang na imedhamiria kujenga majumba ya makumbusho ya utamaduni wa jadi wa kabila la Waqiang."

Idhaa ya kiswahili 2008-07-10