Tarehe 8 Tamasha la Kimataifa la Ngoma za Jadi kwa mara ya kwanza lilifanyika huko Urumqi, mji mkuu wa mkoa wa Xinjiang, China. Wasanii 1,300 wa makundi kumi kadhaa kutoka nchini China na nchi za nje walishiriki kwenye tamasha hilo.
Tamasha hilo ni la sanaa ya hali ya juu ya ngoma za jadi za mkoa wa Xinjiang na nchi za nje. Naibu mwenyekiti wa Shirikisho la Wasanii wa Ngoma la China Bw. Feng Shuangbai alisema, mkoani Xinjiang kuna utamaduni mkubwa wa ngoma za jadi, serikali ya China inathamini sana utamaduni huo na kuuhifadhi kwa njia za kila aina, ikiwa ni pamoja na kufanya tamasha na makongamano. Alisema,
"Ngoma za kikabila na hususan ngoma za kiasili hazijawahi kuthaminiwa na serikali kama hivi leo, na huku wasanii wanatilia maanani kuzifanya ziende na wakati kwa kuonesha maisha ya sasa bila kupoteza mtindo wake wa asili."
Kwenye ufunguzi wa tamasha hilo, mwandishi wa habari alizungumza na mchezaji mkuu wa "ngoma ya Maisilaipu" ya kabila la Wa-Uygur mkoani Xinjiang Bi. Rena, ambaye pia alikuwa ni mkimbizaji mwenge wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing mkoani Xinjiang, alisema "Maisilaipu" kwa lugha ya Ki-Uygur maana yake ni "shamrashamra ya ngoma". Kwenye ufunguzi ngoma hiyo ilichezwa kwa kuonesha mtindo mpya wa mavazi na vitendo. Alisema walifanya mazoezi kwa miezi minne ili kuweza kucheza ngoma hiyo. Alisema,
"Kufanyika kwa tamasha hilo la kimataifa katika mkoa wetu ni fursa adimu kwa sisi wasanii wa Xinjiang. Tuliwaalika wataalamu kadhaa kutoka Beijing kutusaidia kisanaa, ingawa walichoka sana lakini walifurahi kuona jinsi ngoma zetu za kikabila zinavyovutia. Tunafurahi kupata fursa hii ya kuonesha ngoma zetu ili tuifahamishe dunia kuhusu mkoa wa Xinjiang ulivyo."
Katika siku za tamasha hilo makundi kumi kadhaa kutoka mkoani na nchi za nje yalionesha michezo yao katika majumba zaidi ya kumi mijini Urumqi na Changji mkoani humo, makundi 21 ya ngoma ya Xinjiang kutoka makabila mbalimbali yalionesha ngoma zao za asili.
Mliosikia ni muziki wa ngoma ya "Spring ya Mukamu" iliyochezwa na Kundi la Wasanii la Mukamu la Xinjiang.
Ngoma ya Mukamu mkoani Xinjiang ni sanaa iliyotungwa na kabila la Wa-Uygur. Tarehe 25 Novemba mwaka 2005 sanaa hiyo iliidhinishwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO kuwa ni "mfano wa utunzi wa utamaduni wa asili usioonekana duniani". Mkuu wa Kundi la Wasanii la Mukamu alisema, kundi hilo lilianzishwa mwaka 1989, ni kundi pekee linalojishughulisha na kazi ya kurithi, kukusanya na kutafiti sanaa ya Mukamu na kuionesha jukwaani. Serikali ya China inazingatia sana kuhifadhi sanaa hiyo, na sasa kila wilaya mkoani Xinjiang imekuwa na idara ya kuhifadhi sanaa hiyo, na katika Chuo cha Sanaa cha Xinjiang kimeanzisha taaluma ya sanaa ya Mukamu na vijana wanaojifunza sanaa hiyo wamekuwa wengi. Ili kuonesha sanaa hiyo wasanii 152 wa kundi hilo walitumia siku nyingi kufanya mazoezi. Alisema,
" Ngoma ya 'Spring ya Mukamu' tuliitayarisha kwa zaidi ya miaka miwili. Jukwaani kwanza tunataka kuonesha asili yake ikiwa ni pamoja na maneno na muziki wake, ila tu mavazi na vitendo. Tamasha hilo la kimataifa ni fursa nzuri kwetu kuonesha sanaa ya kale ya Mukamu."
Licha ya makundi ya wasanii ya Xinjiang pia kulikuwa na makundi mengine kutoka nchi na sehemu tisa zikiwemo Russia, Misri, na Polynesia iliyo chini ya himaya ya Ufaransa. Mkuu wa Kundi la Wasanii la Chuo Kikuu cha Chihuahua kutoka Mexico Profesa Antonio Rubio Sagarnaga alisema, tamasha hilo limewaletea fursa nzuri ya kuelewa utamaduni wa makabila tofauti nchini China. Alisema,
"Tamasha hili ni fursa nzuri kwa Wachina kuelewa utamaduni wa nchi za nje, wasanii wa ngoma wana lugha ya namna moja, ingawa watu wa makabila tofauti wana lugha tofauti lakini lugha yao ya ngoma ni ya namna moja, wanaweza kuelewa utamaduni wa makabila tofauti. Ni matumaini yangu kuwa tamasha hili litaendelea kufanyika katika mji huu mzuri. Maisha ya binadamu hayawezi kutengana na ngoma."
Tamasha la Kimataifa la Ngoma za Jadi mkoani Xinjiang linafanyika kwa siku kumi. Licha ya kuonesha michezo ya ngoma katika siku za tamasha hilo pia kulikuwa na baraza la ngoma, maonesho ya utamaduni wa Xinjiang, maonesho ya utamaduni usioonekana wa mkoa huo na maonesho ya picha zilizochorwa na wasanii na wakulima.
|