Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-07-29 15:54:59    
Makampuni ya teknolojia za hali ya juu za mji wa Beijing yapata maendeleo makubwa katika kufanya uvumbuzi kwa kujitegemea

cri

Eneo la sayansi na teknolojia la Zhongguancun liko kaskazini magharibi mwa mji wa Beijing. Kwenye eneo hilo kuna makampuni karibu elfu 20 ya teknolojia za hali ya juu. Katika miaka ya hivi karibuni, makampuni hayo yakisaidiwa na serikali, yamevumbua bidhaa na teknolojia nyingi mpya, ambazo baadhi yake zimefikia kiwango cha kisasa duniani, na makampuni hayo yamepata masoko ya nchini na nchi za nje.

Eneo la sayansi na teknolojia la Zhongguancun ni eneo lenye makampuni mengi yanayofanya uvumbuzi wa teknolojia mpya. Makampuni mengi maarufu yakiwemo Lenovo, Sohu na Huaqi yalianzishwa huko na yameingia kwenye soko la kimataifa. Ili kuyahimiza makampuni yafanye uvumbuzi kwa kujitegemea, katika miaka ya hivi karibuni kamati ya usimamizi wa eneo hilo, wizara ya sayansi na teknolojia ya China na idara husika zilianzisha majaribio kwenye makampuni 100 yanayofanya uvumbuzi.

Kampuni ya teknolojia ya upashanaji habari ya IGRS ni moja kati ya makampuni hayo. Mwaka 2005, makampuni manane ya China yanayoshughulikia kompyuta na vyombo vya umeme vya nyumbani yakiwemo makampuni ya Lenovo, Changhong na Konka yaliunda Umoja wa IGRS na kuendeleza makubaliano ya IGRS ambayo yanalenga kuunganisha pamoja kompyuta na vyombo vya umeme nyumbani. Meneja mkuu wa kampuni hiyo Bw Sun Yuning alisema hivi sasa makampuni zaidi ya 100 kutoka China, Marekani, Japan na Israel yamejiunga na Umoja wa IGRS, alisema,

"Makampuni yanayojiunga na Umoja wa IGRS yamefikia 113, ambayo bidhaa zake zinachukua asilimia 85 ya soko la televisheni na karibu nusu ya masoko ya kompyuta, simu za mkononi na vyombo vingine vya umeme vya nyumbani nchini China. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2007, bidhaa za umoja huo zinazouzwa masokoni zilikuwa zaidi ya aina 20.

Ikisaidiwa na kamati ya usimamizi ya eneo la Zhongguancun, kampuni ya teknolojia ya upashanaji habari ya IGRS imeongeza nguvu kushughulikia utafiti wa sayansi na teknolojia. Mwezi Novemba mwaka jana, vigezo vya IGRS vilichukua nafasi ya kwanza duniani kuhusu mambo yanayounganisha kompyuta, vyombo vya umeme nyumbani na vyombo vya upashanaji habari.

Ili kuyasaidia makampuni madogo na ya wastani yenye uwezo mkubwa wa kujiendeleza, na kuongeza uwezo wao wa kufanya uvumbuzi kwa kujitegemea, kamati ya usimamizi wa eneo la Zhongguancun ilitunga sera mbalimbali za kuyahimiza makampuni kufanya uvumbuzi, ikiwemo kuyaunga mkono makampuni yanayoshiriki kwenye majaribio kuimarisha utungaji wa vigezo na hakimiliki ya ubunifu, kujenga miundo mbinu muhimu ya sayansi na teknolojia na kushughulikia miradi mikubwa ya kitaifa, na kutangaza habari kuhusu makampuni hayo. Si kama tu kamati hiyo inatoa uungaji mkono wa kifedha, bali pia inashirikiana na taasisi ya sayansi ya China, wizara ya sayansi na teknolojia na idara husika, ili kuyaunga mkono makampuni hayo kwa pamoja. Kwa mujibu wa takwimu zisizokamilika, katika mwaka mmoja uliopita tangu majaribio kuanza, idara husika zimetoa uungaji mkono kwa miradi karibu 200 ya makampuni hayo, kutoa fedha karibu yuan bilioni 1, na kuhimiza uwekezaji kwenye mambo ya jamii karibuni yuan bilioni 4.

Mkurugenzi wa kamati ya eneo la Zhongguancun Bw. Daiwei alisema, baada ya majaribio hayo kuanza, makampuni hayo yameongeza matumizi ya fedha kwenye utafiti wa sayansi na teknolojia, na yakishirikiana na maabara na vyuo vikuu, yamepata mafanikio makubwa katika utafiti wa teknolojia muhimu, ambazo teknolojia nyingi mpya zimetumiwa na bidhaa mpya zinazotengenezwa kwa teknolojia hizo znauzwa masokoni. Bw. Dai alisema,

"Chombo cha kubadilisha mawimbi ya sauti kilichovumbuliwa na kampuni ya Leader & Harvest ya Beijing kinaweza kubana matumizi ya umeme kwa asilimia 30. Bidhaa hizo zinachukua nafasi ya kwanza kwenye masoko ya nchini China. Chanjo ya mafua ya ndege kwa binadamu iliyovumbuliwa na kampuni ya Sinovac Biotech ni dawa ya kwanza iliyopata idhini maalumu ya uzalishaji wa dawa nchini China."

Kwenye msingi wa makampuni hayo 100, mwezi Mei mwaka huu eneo la Zhongguancun lilichagua kundi la pili la makampuni 79 kufanya majaribio. Kampuni ya Hi-Tech Wealth ya Beijing ni moja kati ya makampuni hayo, ambayo inashughulikia simu za mkononi zinazolinda usalama wa habari. "Shangwutong" ni bidhaa zao maarufu nchini China. Hivi sasa kampuni hiyo imepata idhini 28 za hakimiliki za ubunifu, na imevumbua teknolojia 10 muhimu. Meneja mkuu wa kampuni hiyo Bw. Zhang Zhengyu anaona kuwa, uvumbuzi haumaanishi uvumbuzi wa teknolojia tu, pia unamaanisha uvumbuzi wa usimamizi unaotokana na uvumbuzi wa teknolojia, alisema,

"Uvumbuzi wa teknolojia ni kazi yetu muhimu, lakini pia tunatilia maanani uvumbuzi wa biashara na utamaduni. Tutabadilisha mzunguko mbaya wa kushindana kwa bei nafuu, tutafanya uvumbuzi ili kuinua teknolojia za kutengeneza bidhaa, kuongeza nyongeza ya thamani, na kuanzisha mzunguko mzuri."

Maneno ya Bw. Zhang Zhengyu yameonesha maoni ya makampuni mengi ya teknolojia ya hali ya juu. Si kama tu makampuni hayo yametenga fedha nyingi zaidi katika utafiti wa teknolojia, bali pia wanatafuta fursa mbalimbali ili kuanzisha chapa maarufu na utamaduni wa makampuni. Michezo ya Olimpiki ya Beijing ni fursa nzuri kwa makampuni ya China. Makampuni mengi ya eneo la Zhongguancun yanatumia fursa hiyo kuinua sifa ya chapa zao. Kwa mujibu wa takwimu zisizokamilika, miradi 78 ya eneo hilo imeshiriki kwenye ujenzi na huduma za michezo ya Olimpiki ya Beijing. Makampuni manane yamekuwa makampuni yanayoshirikiana na kutoa mchango na huduma kwenye michezo ya Olimpiki ya Beijing. Mkurugenzi wa kamati ya eneo la Zhongguancun Bw. Dai Wei alisema,

"Kampuni ya Lenovo ni kampuni pekee ya China kati ya makampuni yanayoshirikiana na kamati ya Olimpiki ya kimataifa. Kampuni ya Sohu ni kampuni inayotoa mchango kwa huduma za michezo ya Olimpiki kwenye mtandao wa Internet. Televisheni za mkononi zinazotengenezwa na kampuni ya Huaqi zilitangazwa kwenye kituo cha habari cha michezo ya Olimpiki ya Beijing. Mifumo ya utangazaji na usimamizi ya kampuni ya Zhongkedayang itatoa huduma ya matangazo ya televisheni ya michezo ya Olimpiki ya Beijing nje ya viwanja na nyumba ya michezo."