Miaka 7 iliyopita, Beijing ilikubaliwa kuwa mwenyeji wa michezo ya 29 ya Olimpiki, na tokea wakati huo "kuandaa Michezo ya Olimpiki ya kuonesha mafanikio mapya ya kisayansi na kiteknolojia" ilikuwa ahadi ya makini ya China. Baada ya miaka hiyo saba, miradi mbalimbali ya Michezo ya Olimpiki ya kuonesha mafanikio mapya ya kisayansi na kiteknolojia imetimizwa nchini China na kushangaza na kufurahisha dunia.
Sherehe ya ufungaji wa michezo ya Olimpiki ya Beijing ilifanyika tarehe 24 kwenye uwanja wa michezo wa taifa "Kiota". Kwenye michezo hiyo iliyodumu kwa nusu mwezi, kuna mambo mengi yasiyosahaulika, mojawapo ni sherehe ya ufunguzi wa michezo hiyo iliyofanyika tarehe 8 mwezi Agosti.
Sherehe hiyo inasifiwa kuwa imeunganisha vizuri moyo wa Olimpiki na teknoloji za kisasa. Waziri wa taifa wa zamani wa Uturuki aliyeshughulikia mambo ya michezo Bw. Mehmet Ali Sahin alisema:
"niliwahi kushiriki kwenye sherehe ya ufunguzi wa michezo ya Olimpiki ya awamu kadhaa zilizopita, lakini naona sherehe ya ufunguzi wa michezo ya Olimpiki ya Beijing ni nzuri kabisa kuliko zote zilizopita, pia ni sherehe iliyoandaliwa kwa teknolojia nyingi zaidi na bila dosari yoyote."
Kwenye sherehe hiyo, maonesho murua ya ngoma, nyimbo na fashifashi yamewaonyeshea watamazaji kote duniani tamasha kubwa la utamaduni, ambalo liliwashangaza watu kutokana na kutegemea teknolojia mpya ya hali ya juu. Mkurugenzi wa kituo cha uendeshaji wa sherehe za ufunguzi na ufungaji wa michezo ya Olimpiki ya Beijing Bw. Wang Ning alisema, sherehe ya ufunguzi wa michezo hiyo ilitumia teknolojia mpya kumi kadhaa za kiwango cha juu, ambazo ni nyingi zaidi kuliko awamu zote zilizopita kwenye historia ya Olimpiki. Bw. Wang Ning alisema:
"sherehe hiyo ilitumia teknolojia nyingi na vifaa vingi vya kisasa, ambavyo idadi ya vifaa vilivyotumika imezidi ile ya michezo ya Olimpiki ya awamu zote zilizopita."
Imefahamika kuwa vifaa vilivyotumika kwa ajili ya sherehe ya ufunguzi wa michezo hiyo vina uzito wa zaidi ya tani 2000, kati ya vifaa hivyo, skrini kubwa ya teknolojia ya LED iliyowekwa chini ilifanya kazi muhimu katika maonesho ya sherehe hiyo, skrini hiyo yenye urefu wa mita 147 na upana mita 22 ilikuwa inaonesha picha mbalimbali kwa rangi na mwangaza tofauti na kuwapelekea watazamaji kwenye hali ya kindoto.
Mbali na hayo, muhimu zaidi ni kwamba matokeo mengi mapya ya sayansi na teknolojia yalitumika katika usanifu na ujenzi wa majumba na viwanja vya michezo, ili kuweka mazingira ya kiwango cha juu kwa wachezaji duniani. Kwa jumla mji wa Beijing vilijengwa viwanja na majumba mapya 12 kwa ajili ya michezo ya 29 ya Olimpiki, kwa mfano wa Bustani ya michezo ya mashua ya Olimpiki, inachukua eneo kubwa kabisa miongoni mwa viwanja vyote vipya vya michezo, eneo la maji peke yake linachukua mita za mraba laki 6.4, na hiyo ni bustani pekee duniani inayoweza kufanya mashindano ya aina mbalimbali ya mashua kwenye eneo moja. bustani hiyo inasifiwa sana na wachezaji wa China na wa nje. Wachezaji wa mashua wa China walisema:
"njia hii ya mashindano ni ya kiwango sanifu kabisa cha kimataifa.
Eneo hili la mashindano linavutia sana, mazingira na vifaa vyote ni vya kisasa, hii ni kweli bustani nzuri kabisa ya mashindano nchini na kote duniani."
Ujenzi wa majumba na viwanja vingi vya michezo ya Olimpiki ya Beijing umetumia teknolojia mpya. Uwanja wa michezo ya taifa "Kiota" umetumia mfumo wa vifaa vya chuma cha pua vyenye ugumu wa hali ya juu ambavyo vilisanifiwa na kutengenezwa na China kwa kujitegemea, umbo la uwanja huo wa mfumo wa vifaa vya chuma cha pua pia ni la pekee duniani; na majumba mengi ya michezo yamewekwa kuta za vioo zinazoweza kukusanya nishati ya juu zilizosanifiwa na kutengenezwa na China kwa kujitegemea, ili kutoa nishati safi kwa majumba hayo.
Kwa mujibu wa takwimu husika, teknolojia za kisasa pia zimetumika kuhakikisha wachezaji wa nchi mbalimbali wanaweza kushiriki kwenye mashindano kwa usawa na haki. Imefahamika kuwa, upimaji wa dawa za kuongeza nguvu kwenye michezo ya Olimpiki ya Beijing ni mkali zaidi kuliko michezo ya awamu zote zilizopita, kituo cha upimaji kina vifaa vya kisasa kabisa duniani, wapimaji zaidi ya elfu moja walifanya upimaji mara 4500 kwa wachezaji kwenye michezo ya Olimpiki ya Beijing.
Katika miaka ya hivi karibuni, dawa kadhaa za kuongeza nguvu zenye teknolojia ya ya hali juu zimetoa changamoto kwa idara za kupambana na matumizi ya dawa hizo duniani, aina moja kati ya dawa hizo ni hGH, ingawa upimaji wa dawa hiyo ulianza kufanyika katika michezo ya Olimpiki ya Athens mwaka 2004, lakini haikugunduliwa hata mara moja, kwa sababu dawa hiyo inakaa muda mfupi tu kwenye mzunguko wa damu mwilini, watumiaji wa dawa hiyo wanaweza kupita kwenye upimaji wakisimamisha matumizi yake kabla ya upimaji. Lakini kwenye michezo ya Olimpiki ya Beijing, hali hiyo imebadilika kabisa. Mwenyekiti wa idara ya kupambana na dawa za kuongeza nguvu duniani Bw. John Fahey alisema:
"kiwango chetu cha upimaji kimeinuka kwa kiasi kikubwa kuliko mwaka jana, kidhahiri ni juu zaidi kuliko wakati wa michezo ya Olimpiki ya Athens, hali hiyo imetoa ishara wazi kwa wachezaji wanaojaribu kutumia dawa ya hGH, kwamba wakitumia dawa hiyo pia watagunduliwa. Tumepiga hatua kubwa, ujanja kama zamani hautafua dafu tena."
|