Sherehe kubwa na ya kushangaza dunia nzima iliyofanyika tarehe 8 Agosti katika ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing na sherehe iliyojaa furaha na nderemo iliyofanyika tarehe 24 Agosti katika ufungaji wa michezo hiyo, sherehe hizo mbili zote ziliwapa watu kumbukumbu zisizosahaulika. Mwongozaji mkuu katika kuandaa sherehe hizo ni Bw. Zhang Yimou.
Tarehe 8 Agosti sherehe yenye mada ya "amani" iliyofanyika katika ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing iligusa hisia za watu wengi duniani. Mwenyekiti wa Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa Bw. Jacques Rogge alisema, "Watu wengi wanasema sherehe hii ya ufunguzi ni sherehe nzuri isiyokuwa na kifani katika historia ya michezo ya Olimpiki." Makala ya mhariri wa Shirika la Habari la Ufaransa AFP ilisema, "Sherehe ya ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing imeeleza historia ndefu ya China tangu enzi za kale mpaka nchi kubwa ya kisasa." Tovuti ya mtandao wa internet ya gazeti la Uingereza "The Independent" ilisema sherehe hiyo ya ufunguzi wa michezo ya Olimpiki ilieleza historia ya miaka elfu tano ya China kwa saa chache na imeonesha utamaduni wa kale zaidi duniani.
Bw. Zhang Yimou mwenye umri wa miaka 57 mwaka 1982 alihitimu kwenye kitivo cha upigaji wa picha za filamu katika Chuo Kikuu cha Filamu cha Beijing. Mwaka 1985 alipata tuzo nchini China kutokana na filamu aliyopiga iitwayo "Ardhi ya Udongo Manjano" na tuzo za aina tatu katika Tamasha la Kimataifa la Filamu la Hawaii.
Baada ya kupiga filamu ya "Ardhi ya Udongo Manjano" Bw. Zhang Yimou alianza kuwa mwongozaji wa filamu badala ya mpigaji filamu. Mwaka 1987 filamu ya "Mtama Mwekundu" ambayo ilipigwa chini ya mwongozaji wake kwa mara ya kwanza ilitingisha watazamaji na ilipata tuzo katika Tamasha la Kimataifa la Filamu la Berlin. Kuanzia mwaka 1990 Bw. Zhang Yimou aliongoza upigaji wa filamu nyingi na kupata tuzo katika mashindano mengi ya kimataifa ya filamu kutokana na kuwa filamu hizo zimeonesha utamaduni wa China unaong'ara. Bw. Zhang Yimou alisema,
"Najitahidi kukuza mazingira ili kuleta hali ya kuwavutia watu."
Kuanzia mwaka 2001 Bw. Zhang Yimou alikuwa amezama kwa moyo wote katika kazi yake ya maandalizi ya kuomba kuwa mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing. Mwaka 2006 alichaguliwa kuwa mwongozaji mkuu wa sherehe ya ufunguzi wa michezo hiyo baada ya kufanikiwa katika zabuni iliyoshindaniwa na wataalamu wengi wa utamaduni.
Kuhusu kazi hiyo Bw. Zhang Yimou aliona amepata shinikizo kubwa. Alisema,
"Kwa kweli mimi si mgeni kuhusu mambo ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing, kwani toka Beijing ilipoomba kuwa mwenyeji wa kufanya michezo hiyo miaka saba iliyopita mpaka maonesho ya michezo ya sanaa ya China kwa dakika nane katika Michezo ya Olimpiki ya Athens yote nilishiriki, lakini wakati nilipopewa jukumu la kuongoza sherehe ya ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing niliona nimepata shinikizo kubwa kuliko nilivyofikiri hapo kabla, matatizo mengi ambayo hayawezi kuepukika lazima uyakabili."
Kwa ajili ya sherehe ya ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki, wataalamu wengi walishirikishwa kutoka kila pembe nchini China, walifanya mikutano mingi isiyohesabika, katika mikutano hiyo Bw. Zhang Yimou alishikilia msimamo wake imara wa kuonesha kwanza sanaa."
Msimamizi mkuu wa muziki kwenye ufunguzi na ufungaji wa Micheo ya Olimpiki ya Beijing Bw. Chen Qigang alisema,
"Kundi la uongozaji wa sherehe liliundwa na wataalamu kutoka sehemu mbalimbali, wote walikuwa wataalamu wakubwa, ni vigumu kuwaongoza. Bahati nzuri mwongozaji mkuu wa kundi hilo alikuwa Zhang Yimou ambaye alikuwa na msimamo wake imara bila kuyumbayumba. Bw. Zhang Yimou alisema, mambo yote ni ya pili ila tu sanaa. Ingawa alikuwa anashikilia msimamo wake huo lakini hakuwa mkaidi wa kukataa mapendekezo ya wengine."
Bw. Zhang Yimou alisema anaridhika na juhudi za kundi lake la uongozi. Alipozungumzia picha ndefu ya mtindo wa Kichina iliyozongoreshwa kwenye ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing alifurahi na kupongeza sana kundi lake. Picha hiyo ilipozongolewa pole pole imeonesha picha za wachezaji hodari wa zamani wa nchi 204. Bw. Zhang Yimou alisema,
"Picha hiyo ndefu ilionesha moja kwa moja mada ya michezo hiyo 'Dunia Moja na Ndoto Moja'. Naona hakuna jambo lolote linaloweza kuwakusanya pamoja vijana hodari kutoka nchi 204 isipokuwa michezo ya Olimpiki, ningependa kuipatia picha hiyo jina la 'maskani yetu ya pamoja', kwa sababu picha hiyo imeundwa na wachezaji wote hodari duniani."
Wakati watu bado hawajasahau upekee wa sherehe ya ufunguzi, tarehe 24 sherehe ya ufungaji iliyovutia zaudu ya michezo hiyo ilifanyika kwa shangwe.
Sherehe ya ufungaji wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing ilikuwa kama bahari ya furaha, vyombo vingi vya habari vilisifu sherehe hiyo kuwa ni "tamasha kubwa la dunia". CNN ilisema, sherehe ya ufungaji imepeleka kileleni michezo hiyo ya Olimpiki iliyovunja rekodi nyingi za dunia na kuonesha sura nzuri ya China kimataifa, na ilisifu kwamba "Ingawa moto mtakatifu umezimwa michezo inaonekana kama bado inaendelea."
|