Wanamichezo wa China walikuwa na matumaini ya kujipatia ushindi na kunyakua medali za dhahabu kwenye michezo ya Olimpiki ya Beijing. Katika miaka ya karibuni wakati uchumi uliohusiana na michezo ya Olimpiki ulipata maendeleo siku hadi siku, wanaviwanda wa China walifanya juhudi kujipatia "medali ya dhahabu", yaani umaarufu duniani.
Katika miaka 7 iliyopita wakati mji wa Beijing ulipokubaliwa kuwa mwenyeji wa kuandaa michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 katika miaka 7 iliyopita, kampuni ya Lenovo ilikuwa kampuni maarufu ya elektroniki na upashanaji habari nchini China, lakini kwenye soko la kimataifa, kampuni hiyo bado haijajulikana na watu wengi. Meneja mkuu wa kampuni hiyo Bw. Yang Yuanqing alipozungumzia kazi ngumu ya kuingia kwenye soko la kimataifa alisema,
"Ni changamoto kubwa kwa makampuni ya nchi zinazoendelea ikiwemo China kuwafanya wateja wa nchi za nje zitambue chapa za bidhaa zetu. Ni lazima tufanye juhudi kubwa zaidi ambazo huenda ni mara mbili hadi tatu kuliko juhudi za makampuni ya nchi zilizoendelea."
Baada ya mji wa Beijing kufanikiwa kugombea nafasi ya kuandaa michezo ya Olimpiki, kampuni ya Lenono pia ilipata fursa ya kuingia kwenye soko la kimataifa. Mwaka 2004, kampuni hiyo ilisaini mkataba na Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa, na kuwa mmoja kati ya wenzi wa ushirikiano wa kamati hiyo duniani. Hii ni mara ya kwanza kwa kampuni ya China kuwa mwenzi rasmi wa Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa. Bw. Yang Yuanqing alisema,
"Mwaka 2004, tuliposaini mkataba wa udhamini na Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa, tulikuwa na matumini kuwa wakati kampuni yetu itakapohudumia michezo ya Olimpiki, pia itaweza kuingia kwenye masoko ya kimataifa kwa fursa ya kuandaa michezo ya Olimpiki ya Beijing."
Kushirikiana na michezo ya Olimpiki kumeisaidia kampuni ya Lenonvo kuongeza umaarufu duniani, na kuingia kwenye soko la dunia.
Kwenye orodha ya makampuni 500 yenye nguvu kubwa zaidi duniani ya mwaka 2008 iliyotolewa mwezi Julai na gazeti la Fortune la Marekani, kampuni ya Lenovo ambayo thamani ya mauzo kwa mwaka ni dola za kimarekani bilioni 16.78 ilichukua nafasi ya 499, na hii ni mara ya kwanza kwa kampuni hiyo kuwekwa kwenye orodha hiyo.
Kampuni ya Lenovo ilifanya juhudi kubwa wakati China ilipoandaa michezo ya Olimpiki ya Beijing, na wakati wa michezo ya Olimpiki, hivyo iliuza vizuri bidhaa zake. Naibu meneja mkuu wa kampuni hiyo anayeshughulikia uuzaji duniani wakati wa michezo ya Olimpiki ya Beijing Bi. Li Lan alisema,
"Tulifanya matangazo kwa njia ya televisheni katika nchi mbalimbali duniani zikiwemo Marekani, India, Australia na Ulaya. Kutokana na matangazo ya michezo ya Olimpiki, vyombo vya habari kwa njia za televisheni na mtandao wa Internet vina athari kubwa. Hivyo tumefanya matangazo kwa njia hizo katika nchi na sehemu nyingi duniani. tumesaini mikataba na wanamichezo 15, ambao wameshiriki kwenye mpango wetu wa mabingwa duniani."
Kama kampuni ya Lenovo, makampuni mengi ya China yalichukulia michezo ya Olimpiki ya Beijing kuwa ni fursa nzuri zaidi ya kuongeza umaarufu wa chapa za bidhaa zao na kupanua masoko yao duniani. Makampuni zaidi ya 40 ya China yalisaini mikataba na kuwa wenzi wa ushirikiano, wafadhili au makampuni yaliyotoa bidhaa na huduma kwenye michezo ya Olimpiki ya Beijing. Makampuni hayo ni pamoja na kampuni ya China Mobile, ambayo ni kampuni kubwa zaidi ya simu za mikononi nchini China, na kampuni ya Haier ambayo ni kampuni maarufu ya vyombo vya umeme vinavyotumiwa nyumbani. Na makampuni ambayo hayakupata fusra kuwa wafadhili wa michezo ya Olimmpiki yalichukua njia mbalimbali kuongeza umaarufu wa chapa za bidhaa zao. Kwa mfano, baada ya kushindwa kugombea nafasi ya kutoa sare za michezo kwenye michezo ya Olimpiki, kampuni ya Lining ambayo ni kampuni kubwa zaidi ya bidhaa za michezo ilichukua hatua ya kuwasaidia wanamichezo na timu maarufu duniani.
Michezo ya Olimpiki ya Beijing si kama tu imeyapatia makampuni ya China fursa nzuri ya kujionesha, bali pia imeyapatia makampuni hayo fursa nzuri ya kuwasiliana na kushirikiana na makampuni maarufu duniani. Kampuni ya China Mobile iliwaalika viongozi wa makampuni mengi makubwa ya simu na mawasiliano ya habari duniani kuja Beijing kutazama michezo ya Olimpiki ya Beijing na kujadili mambo ya ushirikiano. Meneja mkuu wa kampuni hiyo Bw. Wang Jianzhou alisema,
"Kampuni yetu ikiwa ni mwenzi wa ushirikiano wa michezo ya Olimpiki ya Beijing, imewaalika viongozi wa makampuni mengi duniani ambayo yana uhusiano wa kibiashara na kampuni yetu kuja Beijing kutazama michezo ya Olimpiki. Tunafurahi kuona kuwa baada ya kuwaalika, karibu wote walikubali."
Watu wengi wanaona kuwa, makampuni ya China yamepata faida kwenye michezo ya Olimpiki ya Beijing. Kwa sababu michezo ya Olimpiki ni michezo inayowavutia watu wa dunia nzima. Chapa za bidhaa za makampuni ya China zitawachia kumbukumbu watazamaji wa michezo ya Olimpiki duniani kwa njia ya televisheni na mtandao wa Internet. Bw. Yang Yuanqing alisema,
"Tunaona michezo ya Olimpiki ya Beijing ni fursa ambayo ni lazima tuitumie. Hii ni fursa ambayo ni nadra kupatikana kwa China na kwa makampuni ya China."
|