Michezo ya Olimpiki ya 29 ilifanyika mjini Beijing kuanzia tarehe 8 Agosti mpaka tarehe 24. Michezo hiyo licha ya kuwa ni tamasha kubwa la mashindano pia ni jukwaa la kuwaoneshea wageni waliotoka kila pembe ya dunia utamaduni wa China unaog'ara.
Tarehe 8 Agosti sherehe kubwa ya ufunguzi wa michezo hiyo ilifanyika ikionesha mada ya "amani" ambayo inatetewa zaidi katika utamaduni wa jadi wa China, na kuonesha historia ndefu ya China.
Kwenye sherehe ya ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki, picha ndefu iliyozongoreshwa ilipozongoa ilieleza mavumbuzi manne makubwa ya China yaani baruti, dira, ufundi wa kutengeneza karatasi na uchapaji, na pia ilionesha ala ya kale ya muziki guqin, ngumi za taiji na njia ya hariri ambayo ilikuwa ni njia ya kufanya maingiliano ya kibiashara na ya kiutamaduni kati ya China na nchi za magharibi katika zama za kale. Watu bilioni nne duniani walikuwa mbele ya televisheni kutazama sherehe hiyo wakistaajabia utamaduni mkubwa wa China. Mwenyekiti wa Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa Bw. Jacques Rogge aliyekuwa kwenye sherehe hiyo ya ufunguzi wa michezo alisema,
"Hii ni sherehe nzuri ya ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki isiyo na mfano, wachina wanaunganisha kwa uhodari utamaduni wao wenye historia ya miaka elfu kadha na utamaduni wa sasa. Huu ni sherehe ya ufunguzi iliyo ya fahari na adhimu."
Licha ya hayo, Michezo ya Olimpiki ya Beijing iliwapa wanasiasa, waandishi wa habari na watalii kutoka nje fursa ya kuwa karibu na raia wa China na kufahamu utamaduni wa China.
Katika Bustani ya Olimpiki mjini Beijing vilikuwepo vyumba 30 vikionesha utamaduni usioonekana wa aina zaidi ya 100 wa sehemu mbalimbali za China, huko wageni wanaweza kuona udarizi mzuri wa ajabu, picha za kukatwa kwa karatasi, na kujaribu kuandika Kichina kwa brashi ya wino na kutazama opera za aina mbalimbali za Kichina na kufahamu mila na desturi za makabila tofauti ya China. Mkurugenzi wa uenezi wa habari wa Kamati ya Maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Sochi Bi. Anna Katya alisema,
"Maonesho kwenye vyumba hivyo yanavutia sana, yanatusaidia sisi wageni kufahamu historia na utamaduni wa China."
Katika kipindi cha michezo ya Olimpiki, majumba ya makumbusho zaidi ya 140 yalifunguliwa mjini Beijing na katika Jumba la Makumbusho la Mji Mkuu yalifanyika maonesho ya "Kumbukumbu za Historia ya China" ambayo vilioneshwa vitu adimu vya kale vilivyokusanywa kutoka majumba ya makumbusho 55 nchini China.
Msemaji wa Idara ya mabaki ya kale ya utamaduni ya Beijing Bi. Yu Ping alisema, mwezi Agosti katika siku zaidi ya kumi tu watazamaji wa maonesho hayo walifikia milioni 1.45, watazamaji hao walitoka karibu nchi 60. Alisema,
"Kila jumba la makumbusho lilikuwa na maonesho ya utamaduni wa aina fulani, kwa jumla aina 110 zilioneshwa mjini Beijing. Kwa hiyo maonesho hayo yameonesha utamaduni wa China kutoka pande mbalimbali."
Bi. Meit Schugelter ni mkuu wa Jumba la Makumbusho la Taifa la Denmark tena ni mshabiki wa utamaduni wa China, alisema,
"Nilitamani sana kuja China ili niweze kujionea utamaduni wake. Utamaduni wa China unanivutia kwa nguvu."
Hali ilivyo ni kwamba maonesho ya utamaduni yalikuwa yameanza mapema kwa nusu mwaka kabla ya ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing, michezo ya sanaa zaidi ya 170 ikiwa ni pamoja opera za kila aina za Kichina na michezo ya kuigiza ilioneshwa zaidi ya mara 600 kuanzia mwezi Machi.
Mkurugenzi wa kitengo cha sanaa katika Wizara ya Utamaduni ya China Bw. Yu Ping alisema,
"Monesho hayo ni makubwa ambayo hayajawahi kutokea toka Jamhuri ya Watu wa China kuanzishwa kwa sifa na idadi ya michezo hiyo, na yameonesha utamaduni wa jadi wa makabila ya China na maendeleo ya utunzi wa michezo ya sanaa."
Baada ya kutazama opera ya muziki ya "Sanamu za Askari na Farasi" inayoeleza hadithi za mfalme wa kwanza wa zama za kale nchini China Qin Shi Huang Bw. Won Sup Shin wa Korea ya Kusini alisema,
"Opera hiyo haina mazungumzo, ni rahisi kuelewa kwa wageni, kwa hiyo watu waliokuja kushiriki kwenye michezo ya Olimpiki wanaweza kufahamu historia ya China kwa kutazama opera hiyo."
Wageni wengi walivutiwa sana na utamaduni unaong'ara wa mji wa kale Beijing, walitembelea vichochora mjini, kuburudika na chai kwenye mikahawa na kusikiliza opera ya Kibeijing wakizama katika maisha ya wenyeji.
Waziri mkuu wa Estonia Bw. Andrus Ansip alikwenda kunywa chai kwenye mkahawa maafuru wa chai mjini Beijing huku akifurahia opera za jadi na jinsi waigizaji walivyobadilisha sura kwa ghafla. Alisema,
"Michezo inanivutia kweli, taifa ambalo linathamini kama hivi historia na utamaduni wake hakika litakuwa na maendeleo makubwa."
Beijing pia ni mji mkubwa wa kimataifa. Katika muda wa miezi miwili kabla na baada ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing bendi maarufu za muziki na makundi ya michezo ya sanaa duniani walikuja Beijing, wasanii kutoka nchi zaidi ya 80 walifanya maonesho ya michezo ya sanaa na shughuli za utamaduni zaidi ya 200 mjini humu.
Utamaduni mkubwa China uliooneshwa katika kipindi cha Michezo ya Olimpiki ya Beijing uliwavutia wageni. Katibu mkuu wa Shirikisho la Taekwondo la Ulaya Bw. Gerrit Eissink alisema,
"Niliwahi kushiriki kwenye michezo mingi ya Olimpiki, lakini kama Michezo ya Olimpiki ya Beijing iliyounganisha utamaduni na michezo sikuwahi kuona na kujihisi."
|