Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-09-25 17:14:39    
Msanii wa kuchora picha kwenye gamba la yai

cri

Kuchora picha kwenye gamba la yai ni sanaa ya jadi nchini China. Sanaa hiyo licha ya kuwapendeza Wachina pia inawavutia sana watalii wa nchi za nje ambao wananunua mayai hayo na kurudi nayo nyumbani. Mayai ya aina yoyote yanafaa kuchorwa. Kabla ya kuchora picha kwenye gamba, kwanza yai linatakiwa kutolewe ute wake na kuwa tupu kwa kutoboa kitundu kidogo, kisha lisafishwe ndani kwa dawa na gamba ling'arishwe. Baada ya picha kuchorwa ni haja kutulizwa ili isifutike. Bi. Liu Jinru ni msanii mkubwa wa kuchora picha kwenye gamba la yai mjini Beijing. Alisema,

"Katika maisha yetu mayai ni kitu cha kawaida kabisa, tunayatumia na tunayatupa magamba yao, lakini sisi wasanii tunayafanya magamba yawe ya thamani kwa kuchora mandhari ya maumbile au watu ingawa nafasi ya gamba la yai ni ndogo sana."

Kazi ya kuchora picha kwenye gamba la yai si rahisi hata kidogo. Bi. Liu Jinru alieleza,

"Kuchora picha kwenye gamba la yai ni tofauti na kuchora picha kwenye karatasi kwa sababu ya umbo lake la mviringo. Picha kwenye gamba hilo inatakiwa iwe nzima unapotazama kwa kuzungusha yai hilo, na kwa sababu ganga la yai halishiki rangi, mfululizo wa kuchora ni kinyume na kuchora picha kwenye karatasi."

Bi. Liu Jinru alionesha picha zake alizochora kwenye mayai ya aina mbalimbali, picha ni nzuri za kushangaza, na kati ya mayai hayo lililo kubwa zaidi ni yai la mbuni. Alieleza kwamba kwa sababu picha ni tofauti, hivyo muda wa kuchora pia ni tofauti, na picha iliyo ya hali ya juu pengine inahitaji siku kadhaa na hata mwezi mmoja kwa kuikamilisha.

Picha za vileta bahati nzuri yaani wanasesere wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing waitwao "Fu Wa" zilichorwa vizuri sana. Alisema, amechora picha hizo kuipongeza michezo hiyo. Alisema,

"Nikiwa msanii nataka kuweka kumbukumbu hili la kihistoria, nimechora wanasesere wanaocheza michezo ya aina 28 ya Olimpiki. mayai hayo nataka kuwapa watoto wangu ili walikumbuke tukio hilo kubwa tunalolitamani kwa miaka mia moja."

Baada ya kuangalia picha alizochora kwenye mayai, mwandishi wa habari Xu Zhiming alisifu sana. Alisema,

"Kweli leo nimetia macho nuru, aina zote za michezo ya Olimpiki zimechorwa vizuri sana kwa vitendo."

Bi. Liu Jinru alieleza kwamba kwa ajili ya sanaa ya aina hiyo iweze kurithishwa kizazi hadi kizazi ameanzisha mafunzo ya bure katika sehemu za makazi. Alisema,

"Hapo awali sanaa ya aina hiyo ilitokana miongoni mwa raia, na sasa tuirudishe tena miongoni mwa raia, wasanii wenzangu wanawajibika kuwafundisha vijana ufundi wa sanaa hiyo ili iweze kurithishwa kizazi hadi kizazi, kwa kufanya hivyo sanaa hiyo haitatoweka!"

Naibu mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Waandishi wa Habari cha Michezo ya Olimpiki ya Beijing Bw. Zhu Shaochen baada ya kuangalia picha za mayai alisema,

"Kwa kweli baada ya kuangalia picha hizo nimekuwa na hisia nyingi. Sanaa kama hiyo imeonesha utamaduni mkubwa wa China, nadhani waandishi wa habari wa nchi za nje pia wanavutiwa kwani kutokana na sanaa hiyo wanaweza kufahamu kiasi fulani utamaduni wa China. Wasanii hao wazee wanastahili kuheshimiwa, wamefanya juhudi nyingi za kuiwezesha baadhi ya sanaa za jadi kuendelea kutoka kizazi hadi kizazi, wanastahili kupewa heshima nyingi!"

Idhaa ya kiswahili 2008-09-25