Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-10-07 16:37:57    
Barua 1007

cri
Wasikilizaji wapendwa ni watangazaji wenu Chen na Pili Mwinyi tunawakaribisha katika kipindi hiki cha sanduku la barua. Leo kwanza tunawaambia habari kuhusu kipindi kipya cha chemsha bongo.

Wasikilizaji wapendwa, tukitaja Mkoa wa Sichuan nchini China labda siyo marafiki wengi wa nje ya China wanaujua, lakini tukitaja Panda, huenda watu wengi wanawapenda wanyama hao wanaoonekana ni wapole sana. Panda wengi kabisa wanaishi mkoa wa Sichuan, kusini magharibi mwa China, Mkoa wa Sichuan ni maskani ya Panda.

Mbali na Panda, katika mkoa wa Sichuan, kuna Bonde la Jiuzhaigou, sehemu hiyo ni kama peponi; pia kuna Mlima Ermei ambao ni sehemu takatifu ya dini ya Kibudhaa inayojulikana nchini na nje; utamaduni wa sehemu ya Sanxingdui yenye miujiza unawavutia watu wengi; sehemu kubwa yenye mianzi ya Shunan inayopendeza, opera ya Chuan inayoshangaza watu na vyakula mbalimbali vitamu vyote vinawavutia watalii wa nchini na nje.

Kama unataka kuelewa zaidi Mkoa wa Sichuan, karibuni katika kipindi maalum cha chemsha bongo kuhusu Vivutio vya Mkoa wa Sichuan, ambapo tutawasomea makala 7 kila wiki kwenye kipindi cha Safari nchini China cha kila jumatatu, na matangazo ya makala yatarudia kwenye kipindi cha Sanduku la barua cha kila jumanne na kila jumamosi.

Kama ilivyokuwa kwenye mashindano ya miaka iliyopita, kila baada ya kusoma makala moja, tutauliza maswali mawili. Baadaye kamati yetu ya uthibitishaji itachagua wasikilizaji washindi wa nafasi ya kwanza, pili na tatu pamoja na nafasi maalum. Washindi watakaopata nafasi za kwanza, pili na tatu watapewa kadi ya kumbukumbu na zawadi; na wasikilizaji washindi watakaopata nafasi maalum wataalikwa kuja China na kutembelea mkoani Sichuan nchini China

Sasa tunawaletea barua tulizotumiwa kutoka kwa wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu Philip Ng'ang'a Kiarie ambaye barua zake huhifadhiwa na Karie Ndumbi Shule ya msingi ya Muchagara sanduku la posta 601 Maragua-Kenya ametuletea barua akisema, kwanza salamu zake ziwaendee watangazaji wote wa idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa. Anaomba nafasi hii ili aweze kuwasilisha mwito wa kuwa na amani na upendo kwa Wakenya. Pili anaichukua fursa hii kuwataka wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa waendelee zaidi kuwafahamisha na kuwaelimisha wasikilizaji kuhusu jinsi nchi ya Jamhuri ya watu wa China ilivyo na utulivu, upendo na amani na huwa inatilia mkazo katika kujiendelesha kiuchumi na kibiashara baina ya makabila mbalimbali wa nchi ya Jamhuri ya watu wa China.

Anawapongeza wasimamizi na watangazaji wote wa idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimtaifa kwa kuwatangazia makala nne ya shindano la chemsha bongo lisemalo tukutane Beijing mwaka 2008 kwenye michezo ya Olimpiki. Anangojea kwa matumaini kutangazwa kwa washindi alishiriki kwenye shindano hili la chemsha bongo na atatosheka na matokeo ya washindi na nafasi atakayoishinda. Anataka kutujulisha kwamba hakosi kusikiliza vipindi na matangazo ya idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa kila siku licha ya matangazo na vipindi tele tele. Kipindi cha kuwa nasi jifunze Kichina kimempa moyo sana katika hali ya kujifunza, kuongea na kutamka maneno ya Kichina amekuwa akifuatilia kwa makini na amepata fursa nzuri ya kujifunza maneno ya Kichina kupitia idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa.

Baadhi ya maneno ambayo humvutia sana na kumpa moyo wa kuendelea kujifunza maneno ya Kichina ni Maneno ya Kichina ya kusalimiana na kuagana katika herufi ya Kiswahili: Ni hao ?habari gani, Ni hao ma, hujambo, Ni maana yake ya kichina ni wewe, hao maana yake ni nzuri, ma ni kisaidizi cha sentensi kwa kuuliza; Hao jiu bu jian-- hatujaonana siku nyingi, Hao jiu, maana yake ya kichina ni siku nyingi, bu jian , hatujaonana; Zui jin zen me yang ? habari za siku hizi au hali gani, zui jin, maana yake ya kichina ni hivi karibuni, siku hizi, zen me yang, maana yake ni hali gani. Anatarajia ya kwamba makala yake hii tutatangaza tukifuata utaratibu tulioutumia kwenye vipindi vya kuwa nasi jifunze Kichina za hapo awali.

Tumefurahishwa na bidii za msikilizaji wetu huyo Philip Ng'ang'a Kiarie wakati wa kujifunza Kichina, kweli amejifunza kwa bidii sana, hata ameandika kwa Kiswali maneno ya Kichina aliyojifunza kutoka kwa matangazo yetu kwenye radio. Juhudi zake hizo zimetutia moyo kuchapa kazi zaidi kuandaa vizuri vipindi vyetu kwa ajili ya wasikilizaji wetu.

Na msikilizaji wetu huyo Philip Ng'ang'a Kiarie pia anaomba tumtumie jarida lolote ambalo linaelezea maskani nzuri ya watu wa China ambayo yatatangazia habari kuhusu utamaduni wa jadi wa watu wa China. Hata pia jarida la China Today na China Pictoriah.

Na anaomba kwa heshima tumsomee salamu zake kwa watu wafuatao: Philip ng'ang'a kiarie akiwa wilaya ya Murang'a kusini mkoa wa kati nchini Kenya; Stephen Magoye Kumarinja, Harishon Kisivuli Lumumba, Yakubu Zaidi, Ram Opele na wengine wote.

Ujumbe wake unasema, yeye ni shabiki mpya wa salamu na ana furaha tele kuwasiliana na nyinyi kupitia kipindi chetu cha salamu zetu katika idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa"

Na pia anataka salamu zake ziwaendee ndugu zake John Waweru a.k.a Wamusiiya, Francis Kanyoro na David Njoroge wote wakiwa wilaya ya Murang'a kusini mkoa wa kati nchini Kenya.

Ujumbe wake unasema, tuzidi kufuatilia matangazo na vipindi vya idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa.

Idhaa ya kiswahili 2008-10-07