Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-10-13 21:17:07    
Mandhari ya ajabu ya Mlima Tianmen

cri

Sehemu ya Zhangjiajie iliyopo mkoani Hunan, katikati ya China, inajulikana kwa mandhari yake ya majabali mengi yaliyochongoka kama msitu, na katika sehemu hiyo upande wa kusini kuna kivutio kinachovutia watalii kutokana na tundu moja kubwa lililopo kwenye kilele cha Mlima Tianmen.

Mlima Tianmen uko kwenye umbali wa kilomita 8 kutoka kusini ya mji wa Zhangjiajie, urefu wake ni mita 1518 juu ya usawa wa bahari na eneo la kilele chake ni kilomita 2.2. Mwaka 260 wa zama za kale mkuu mpya wa wilaya aliyekuwa njiani kwenda kushika madaraka yake alipofika huko, sehemu ya katikati ya kilele cha Mlima Tianmen iliporomoka na kuacha tundu kubwa. Mfalme aliporipotiwa habari hiyo aliona tukio hilo ni ishara ya baraka, aliupatia mlima huo jina la Mlima Tianmen, maana yake ni mlima wenye mlango wa mbinguni. Tokea hapo mlima huu ulianza kujulikana.

Mzee Chen Ziwen anaishi chini ya mlima huo tangu alipokuwa mtoto, alieleza kuwa, kabla ya miaka 1500 iliyopita mfalme Yu Wenyong wa Enzi ya Zhou ya Kaskazini aliongoza maofisa wake kufika huko kufanya tambiko. Mzee Chen Ziwen alisema,

"Mfalme alitaka kufanya tambiko, lakini kwa kawaida wafalme walikuwa hufanya tambiko katika milima mitano mikubwa nchini China na Mlima Tianmen haumo kati yao, mfalme huyo aliutukuza mlima huo kuwa mlima mwingine sawa na milima mitano mikubwa, akawaongoza maofisa wake kupanda mlima huo kutambika."

Kwa hivyo, Mlima Tianmen unajulikana toka enzi za kale. Tundu kwenye kilele limekuwa alama ya Mlima Tianmen. Tundu hilo lina urefu wa mita 131, upana wake ni mita 57 na urefu kutoka mbele mpaka nyuma ni mita 60, pengine ukubwa wa tundu hilo ni mkubwa zaidi kuliko mengine duniani. Ukiangalia kutoka mbele kwa mbali, tundu hilo ni kama dirisha kubwa la kasri la peponi, na ukiangalia kutoka upande mmoja, tundu hilo linaonekana kama handaki lisilo na mwisho. Katika siku yenye hali ya hewa nzuri, mawingu membemba yanaelea mbele ya tundu, na baada ya mvua, tundu hilo linaonekana kuwa nusu yake iko nyuma ya mawingu, mandhari nzuri ilivyo kama ya peponi.

Ukiangalia kutoka kilele cha mlima huo, unaweza kuona mbali na milima yote yanaonekana kuwa ni midogo. Kwa sababu mlima Tianmen ni wima sana, katika zama za kale watu walikuwa hawawezi kuupanda. Hivi leo ngazi 999 zimejengwa kwenye Mlima Tianmen, watalii wanaweza kupanda mpaka kileleni. Wachina wanachukulia 9 ni namba kubwa kabisa na inaashiria baraka, kwa hiyo ngazi 999 pia zinamaanisha ngazi ya kufikia peponi.

Mtalii Bibi Zhang Leilei kwa mara ya kwanza alitembelea mlima huo, alifikiri kupanda mlima mkubwa kama huo ni hatari na hakika atachoka sana wakati wa kushuka chini. Alisema,

"Kwangu ni mara ya kwanza kupanda mlima mkubwa kama huu, ngazi yake ni finyu na mteremko wake ni mkali, hakika itakuwa shida sana kushuka."

Katika upande wa pili wa tundu la Mlima Tianmen kuna mandhari ya ajabu ya aina mbili, moja ni mianzi midogo inayoning'inia kutoka upande wa juu wa tundu hilo, upepo unapovuma, mianzi hiyo inachakacha kama sauti ya kukwaruzana. Kadhalika, matone ya maji yanadondoka dondoka kutoka paa la tundu hilo, wenyeji wa huko walisema mtu akidondokewa mdomoni matone 48 ya maji hayo atabadilika kuwa malaika.

Katika zama za kale walikuwapo watawa wengi wa dini ya Kidao ya Kichina na dini ya Kibuddha waliishi kwenye Mlima Tianmen wakijitenga na ulimwengu. Ilisemekana kwamba Bw. Wang Xu aliyekuwa mtu wa Dola la Chi katika kipindi cha Madola ya Kivita nchini China miaka zaidi ya 2000 iliyopita aliishi huko, alichagua pango moja na kujizamisha katika kutafiti na kuchunguza mbinu mbalimbamli za kivita, baadaye alikamilisha kitabu chake, hadi leo kitabu hicho bado kipo, pango hilo aliloishi lilipewa jina la Guigu.

Bw. Li Guangzhang ni mpenda utalii, alipokuwa mtoto aliishi huko na kwa mara nyingi aliingia pango la Guigu. Alisema,

"Naishi chini ya Mlima Tianmen, naupenda sana mlima huu, navutiwa sana na masimulizi kuhusu pango la Guigu. Baada ya mimi kuwa mtu mzima nilitamani kuingia pango hilo ili nifahamu hali ilivyo mule ndani. Pango hilo lina urefu wa mika 120, mara ya kwanza nilipoingia niliogopa sana, lakini sasa sina hofu kwa sababu nimeingia mara nyingi."

Ni ajabu kwamba kwenye genge la upande wa kushoto wa mlima huo hakuna dalili ya maji yaliyotiririka, hata mvua kubwa inaponyesha hali ni vivyo hivyo. Wenyeji walisema, kama maji yakirowa genge hilo inamaanisha hali ya hewa itakuwa mbaya kiasi kwamba ama ukame ama mafuriko yatatokea. Lakini kwa nini? hadi sasa hakuna yeyote anayeweza kueleza sababu yake.

Katika miongo kadhaa iliyopita tundu la Mima Tianmen lilikuwa linakabiliana moja kwa moja na mlango wa kusini ya mji wa Zhangjiajie, lakini sasa nafasi yake limebadilika na halikabiliani moja kwa moja na mlango wa mji huo, maana tundu hilo limehamia pole pole bila watu kujua. Mpiga picha za kamera Bw. Luo Zhaoyong alisema,

"Nimeshughulika na kazi ya kupiga picha zaidi ya miaka 30, zamani niliweza kuona tundu la Mlima Tianmen kutoka mlango wa kaskazini wa mji wa Zhangjiajie, lakini sasa limehamia upande wa magharibi."

Katika eneo la Mlima Tinmen kuna chuo kimoja cha elimu ambacho kiliwavutia wasomi wengi. Katika zama za kale shughuli za elimu za chuo hicho zilistawi sana, maofisa wengi wakubwa waliwahi kusoma huko na walitoa michango mikubwa kwa ajili ya ustawi wa taifa. Mzee Chen Ziwen alisema,

"Mfalme wa Enzi ya Yuan, Tie Muer, alipoambiwa habari hiyo alifurahi na kukiandikia chuo hicho jina la 'Chuo cha elimu cha Tianmen'."

Tokea hapo chuo hicho kimejulikana sana nchini China, mwaka 1904 chuo hicho kimebadilishwa kuwa shule ya msingi ya ngazi ya juu."

Mlima Tianmen ni mlima wenye mandhari nzuri ya ajabu kweli, ndio maana wenyeji wa huko wanaupatia mlima huo jina jingine la "Mlima Tianmen wa Peponi".