1.Bi. Wei Yuanyuan sasa ni mwalimu wa lugha ya Kiswahili wa Chuo kikuu cha lugha za kigeni cha Beijing. Kwenye Michezo ya Olimpiki ya Beijing iliyofungwa tarehe 24 Agosti, yeye alikuwa mmoja kati ya watu wanaojitolea. Bi, Wei, kwanza ujulishe kipindi chako cha kujifunza lugha ya Kiswahili?
Nilianza kusoma kiswahili katika chuo kikuu mwezi Sptemba mwaka 2000. Baada ya miaka minne ya masomo ya shahada ya kwanza, nikaendelea na masomo ya shahada ya uzamili ya Kiswahili katika chuo chetu mwaka 2004.
Kwa mujibu wa mradi wa kupelekeana wanafunzi kati ya China na Kenya, mwaka 2005 mwezi wa Sepeemba nilikwenda kusomea Kiswahili katika chuo kikuu cha Nairobi nchini Kenya.
Nilirudi China baada ya miezi 10 yaani mwezi Julai mwaka 2006.
Nilihitimu shahada yangu ya pili mwaka 2007 mwezi wa nne, baada ya kuhitimu, nikawa mwalimu wa Kiswahili katika chuo chetu mpaka sasa.
2, Uliwahi kujifunza lugha ya Kiswahili nchini Kenya, Bi, Wei, unaweza kutuelezea hali ya Afrika ya mashariki?
Wakati nilipokuwa Kenya, nilivutiwa na mambo mengi ya Afrika mashariki, ikiwa ni pamoja na mandhari nzuri ya nchi hiyio, uchangamfu na ukarimu wa watu wa huko, hata chakula cha kiafrika. Nilifurahi kupata marafiki wengi wakubwa. Mwanzoni nilikumbwa na matatizo mengi katika masomo na maisha. Wanafunzi wenzangu, walimu wote, na watu wengine wa chuo kikuu cha Nairobi walinisaidia mara kwa mara. Ninawashukuru sana watu wa Kenya kwa ukarimu wao. Nilipokuwa Kenya, kila nilipoenda mahali fulani, watu wa huko walikuwa hunisalimia kwa furaha, hata watu wengi waliniita mtoto wa Afrika. Hivyo Siku zote ninatamani sana kama nikipata fursa nitawasaidia kwa kadiri niwezavyo.
3.Michezo ya Olimpiki ya Beijing iliyofungwa hivi karibuni ilikupa fursa hiyo?
Ndiyo, kwa bahati nzuri baadaye nilikuwa mmojawapo kati ya watu wanaojitolea kwenye michezo ya Olimpiki ya Beijing, nafurahi sana nilipata fursa hii ya kuwahudumia wanamichezo wa Tanzania na Kenya katika michezo ya Olimpiki iliyofanyika Beijing.
4. Namna gani ulichaguliwa kuwa mtu wa kujitolea kwenye Michezo ya Olimpiki ya Beijing? Na mlipata mafunzo gani kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing?
Nilijiandikisha mwaka jana, mwezi wa kwanza mwaka huo, wafanyakazi wa kamati ya maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing waliniambia wanahitaji watu wanaojitolea wa lugha ya Kiswahili. Mwezi Juni, wanafunzi watatu na walimu watatu wakachaguliwa kuwa watu wanaojitolea kwenye kituo cha huduma ya lugha mbalimbali .
Tarehe 1 na 2 Julai tulishiriki katika mafunzo ya michezo ya olimpiki kwa watu wanaojitolea wa huduma ya lugha. Tulifundishwa njia za kufanya kazi na namna ya kutatua matatizo yaliyowezekana kutokea wakati wa michezo hiyo.
5. Wakati marafiki na jamaa zako walipojua kuwa utahudumia Michezo ya Olimpiki ya Beijing, walifurahi?
Sisi watu wa China sote tunaona fahari kubwa michezo ya Olimpiki ilifanyika hapa Beijing. Mimi pamoja na wanafunzi wengi wa Kiswahili tulitamani sana kufanya kazi ya ukalimani katika michezo hiyo tangu zamani. Marafiki zangu walipojua nimetimiza ndoto yangu ya kuwahudumia wachezaji wa Afrika kwenye Michezo ya Olimpiki, wote walinipa pongezi kwa furaha. Mama yangu pia aliniambia lazima nijitahidi maana watu wanaojitolea wataonesha sura ya Beijing.
6. Tujulishe kazi yenu kwenye Michezo ya Olimpiki ya Beijing.
Tulifanya kazi yetu kuanzia tarehe 24 Julai mpaka tarehe 28 Agosti, saa za kufanya kazi ilikuwa kuanzia saa 1 asubuhi hadi saa 6 usiku. Sisi watu sita tulifanya kazi kwa zamu. Kazi yetu kuu ni kutoka huduma ya ukalimani kwa njia ya simu. Wafanyakazi wa viwanja vyote vya michezo walipata matatizo ya lugha ambayo hawawezi kuyatatua, walitupigia simu ili kupata msaada. Wakati mwingine tulikwenda uwanja wa michezo ili kufanya kazi ya ukalimani.
Nafurahi sana nilipata fursa hii ya kuwahudumia wanamichezo na wageni kutoka Afrika. Nilifanya juhudi kwa niwezavyo ili wajione kama wako nyumbani hapa.
7. Watu wengi wanaojitolea walisema walijufunza mambo mengi kutoka kwa Michezo ya Olimpiki, wewe unaonaje?
Nafikiri katika michezo ya Olimpiki, wachezaji walikuwkla na matumaini makubwa ya kupata ubingwa, lakini nafikiri kama mchezaji mwenyewe amejitadihi kwa awezavyo, hata hakuweza kupata medali ya dhahabu, hana haja ya kusikitika. Maana amepata ushindi wake.
Sasa nina matumaini kuwa ninaweza kuwa mwalimu mzuri wa Kiswahili. Bila shaka nitakabiliwa na matatizo mengi katika siku za mbele. Lakini nafikiri nitafanya juhudi kubwa na kuendelea kusoma kwa bidii lugha ya Kiswahili ili niwafundishe vizuri wanafunzi wangu, nitashikilia mpaka mwisho kama alivyo mzee Akhwari, shujaa wa Tanzania kwenye Michezo ya Olimpiki.
Idhaa ya kiswahili 2008-10-17
|