Kampuni ya bidhaa za Kiislamu ya Abudunla ya Ningxia ni kampuni inayoshughulikia uvumbuzi, utengenezaji na uuzaji wa bidhaa za kikabila ambazo nyingi zinauzwa katika nchi za nje. Thamani ya uuzaji kwa mwaka ni zaidi ya yuan milioni 2. Lakini katika miaka kadhaa iliyopita, kampuni hiyo bado ilipata hasara. Meneja mkuu wa kampuni hiyo Bw. Yue Wenhai alisema,
"Mimi ni mwislamu. Kwenye Koran kuna maneno yasemayo usipe moyo na usikate tamaa, ukiwa na moyo wa kidhati, utapata ushindi mwishowe.' Siku zote maneno hayo yananihimiza na kunihamasisha kufanya juhudi za kuendeleza kampuni yangu."
Bw. Yue alisema maneno hayo kwa imani kubwa. Alieleza maendeleo ya kampuni yake na matatizo mbalimbali aliyokumbana nayo wakati alipoanza shughuli yake, akisema,
"Kwa kweli mwanzoni nilikabiliwa na matatizo mengi. Katika miaka ya 80, nilianzisha chapa ya Selangmu ambayo ni chapa ya vyakula vya kiislamu. Nafikiri kutengeneza chakula cha Kiislamu kunakabiliwa na vizuizi vingi, kwa sababu chakula kinaweza kuhifadhiwa kwa muda mfupi tu. Baada ya kushughulikia utengenezaji wa vyakula kwa miaka mitatu, hali ya kampuni yangu ilikuwa mbaya sana."
Wakati kampuni ya Bw. Yue ilipokaribia kufungwa, serikali ya mkoa unaojiendesha wa Ningxia ilichukua shughuli za bidhaa za Kiislamu kuwa ni moja kati ya shughuli 6 zenye sifa ya kipekee zinazohimizwa kuendelezwa zaidi wakati wa kipindi cha mpango wa 11 wa maendeleo ya miaka mitano, Bw. Yue aliona fursa ya kubadilisha hali mbaya ya kampuni yake. Akiwa ni mtu ambaye anaweza kuongea kwa lugha ya kiarabu na ana marafiki wengi, alianza kukagua masoko ili kubadilisha shughuli za kampuni yake. Alisema,
"Kufungua kwa soko la mkoa wa Ningxia kwa nchi za nje kumeziwezesha bidhaa za kampuni yetu kuingia kwenye nchi za Kiarabu kwa urahisi zaidi. Nilijifunza somo la Kiarabu, na wanafunzi wenzangu wamesambaa katika nchi za kiarabu. Kutokana na maelezo yao na ukaguzi wangu kuhusu masoko, niligundua kuwa kuna fursa nyingi za kuendeleza shughuli za kiislamu mkoani Ningxia. Tena mawasiliano ya kiuchumi na kibiashara kati ya mkoa wetu na nchi za kiaarabu yanaimarishwa siku hadi siku, hivyo shughuli hiyo ina uwezo mkubwa wa kupata maendeleo."
Bw. Yue alisema mkoa wa Ningxia unasifiwa kuwa ni mkoa wa Waislamu nchini China. Utamaduni wa Kiislamu unahusiana na mambo mengi mkoani humo, hivyo si kama tu mkoa huo una sifa nzuri ya kikanda, bali pia una maliasili nyingi na mazingira mazuri. Licha ya hayo, sera ya China inaunga mkono maendeleo ya shughuli za kutengeneza bidhaa za Kiislamu. Mambo hayo yalimfanya Bw. Yue awe na imani kubwa ya kubadilisha shughuli za kampuni yake. Baada ya kufanya ukaguzi, aliamua kutengenzea kofia zinazovaliwa wakati wa kusali.
Mwaka 2007 Bw. Yue akichukua kofia kadhaa alishiriki kwenye maonesho ya bidhaa zinazosafirishwa nje na zinazoagizwa kutoka nje ya China. Mfanyabiashara wa Malaysia alipoona kofia zake, alitaka kuagiza bidhaa zake. Wakati huo kampuni ya Bw. Yue haikuwahi kutengeneza kofia kwa wingi, tena vitambaa na mtindo wa kofia za Wamalaysia ni tofauti na bidhaa zake. Lakini fursa mpya inayoweza kuboresha hali ya kampuni yake ilimfanya Bw. Yue kukubali kusaini mkataba, akisema,
"Baada ya kusaini mkataba, nilikuwa na imani kubwa, lakini bado kulikuwa na tatizo moja, yaani sikuwa na wafanyakazi na zana za kutengenezea kofia, hivyo nilitafuta wafanyakazi na mafundi hapa na pale, nilikwenda mikoa ya Gansu na Qinghai, na mwishowe nilikwenda Xi'an kwa sababu nilisikia kuwa mafundi wa huko wanaweza kutengeneza kofia. Nilikutana nao, walinisaidia na kunifundisha jinsi ya kutengeneza kofia. Aidha nilinunua zana za kutengenezea kofia huko Yiwu na Shaoxing mkoani Zhejiang. Hivyo wakati huo kazi ilikuwa ngumu sana. Nilimaliza kutengeneza kofia zilizoagizwa na mfanyabiashara wa Malaysia miezi mitatu baada ya kusaini mkataba."
Kampuni ya Bw. Yue zilisifiwa kwenye na mfanyakazi wa Malaysia kutokana na kukamilisha kazi kwa wakati. Mafanikio hayo yaliimarisha imani yake, na baadaye alisaini mikataba kadhaa na makampuni ya nchi za Saudi Arabia. Kutokana na sifa nzuri ya kampuni yake na bidhaa zake, na mitindo ya bidhaa inayofurahishwa na Waislamu, wafanyabiashara wa Saudi Arabia wote wanaridhika. Tarehe 14 mwezi Machi mwaka huu, kampuni yake ilisaini mkataba wenye thamani ya yuan milioni 21 na kampuni moja ya Saudi Arabia. Bw. Yue alisema,
"Bidhaa za kampuni yetu ziliingia kwenye soko la kimataifa ndani ya mwaka mmoja na miezi mitatu. Mwaka jana kampuni yetu ilikuwa haipati kibali cha kufanya biashara katika nchi za nje. Mwaka huu kampuni yetu imekubaliwa kuuza bidhaa moja kwa moja katika nchi za nje. Kutokana na uungaji mkono wa kamati ya mji na idara ya biashara ya mji wa Yinchuan, nimepata idhini ya kuuza bidhaa nje kwa kujitegemea."
Bw. Yue alisema mpango wake wa kuanzisha tawi la kampuni yake nchini Saudi Arabia umeidhinishwa na serikali, akisema,
"Serikali ilitunga sera mbalimbali nzuri, na ilisema kama sina fedha za kutosha itanisaidia. Nikianzisha vituo vya kuuza bidhaa na jumba la maonesho ya bidhaa katika nchi za nje, serikali kwenye ngazi ya mkoa wa Ningxia na mji wa Yinchuan itanipatia fedha za kuendeleza shughuli zangu."
Bw. Yue alisema serikali si kama tu inayapatia makampuni binafsi uungaji mkono wa kisera, bali pia inayapatia uungaji mkono wa kifedha, ili kuyahimiza kuanzisha shughuli zao katika nchi za nje. Mambo hayo yamemhimiza Bw. Yue kuweka malengo makubwa zaidi. Alipotaja lengo la muda mrefu la kampuni yake, alisema,
"Tumegundua dosari letu, hatuwezi kutengeneza bidhaa za bei nafuu kwa muda mrefu, tunatakiwa kutengeneza bidhaa za kiwango cha juu. Nimepanga kuuza bidhaa za kiwango cha juu katika soko la kimataifa katika miaka mitatu hadi miaka mitano ijayo."
Bw. Yue alisisitiza kuwa ana imani na matumaini makubwa juu ya mustakabali wa kampuni yake.
|