Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-10-22 18:14:19    
Utafiti kuhusu chombo cha kuchunguza sayari ya mwezi wapamba moto nchini China

cri

Chombo cha kuchunguza sayari ya mwezi ni chombo maalum kinachoweza kusafiri kwenye sayari ya mwezi, kukusanya sampuli na kufanya uchunguzi kuhusu sayari hiyo. Kutokana na uwezo wa China wa kuchunguza anga ya juu kuendelea kuinuka, idara nyingi za utafiti wa sayansi nchini China zimeanzisha utafiti kuhusu teknolojia za eneo hilo.

Kwenye maabara moja mjini Shanghai, mwandishi wetu wa habari aliona chombo kimoja cha majaribio cha kuchunguzia sayari ya mwezi ambacho kina magurudumu sita na kina rangi ya dhahabu kikitembea kwenye ardhi yenye matuta mengi iliyotengenezwa kwa kutumia udongo wa volkano kama ule wa kwenye sayari ya mwezi. Naibu mkurugenzi wa ofisi ya teknolojia mpya katika taasisi ya utafiti wa miradi ya safari za anga ya juu ya Shanghai Bw. Hu Zhenyu alisema, chombo hicho chenye urefu wa mita 1.5, upana mita moja na uzito kilo 120 ni chombo cha kizazi cha tatu kilichotengenezwa nao, na uwezo wake umeinuka kwa kiasi kikubwa kuliko vile vya vizazi vilivyopita. Bw. Hu Zhenzhong alisema:

"mifumo yake ya kutembea na ya udhibiti yote inatumia zana zinazotumika kwa ajili ya safari za anga ya juu, chombo cha No. 3 kimepiga hatua mbele kuliko kile cha No. 2, na kimethibitisha kuwa usanifu wetu unaweza kutumika kihalisi."

Imefahamika kuwa kutoka chombo cha majaribio kama hicho hadi chombo halisi cha kuchunguza sayari ya mwezi bado kuna matatizo mbalimbali ya kiteknolojia yanayotakiwa kuondolewa. Kwa mfano, uzito wa vitu kwenye sayari ya mwezi ni moja ya sita ya ule wa kwenye dunia, udongo wa sayari ya mwezi ni laini sana, kwa hiyo chombo hicho lazima kiwe na uwezo wa kufanya kazi kwenye mazingira hayo; aidha, ardhi ya mwezi ina matuta mengi pamoja na mashimo na mawe mengi, katika mazingira hayo chombo hicho si kama tu hakiwezi kuteleza wala kupinduka, bali pia kinatakiwa kuweza kufanya vitendo mbalimbali kama vile kwenda mbele, kurudi nyuma, kugeuka na kupaa juu.

Bw. Hu Zhenyu alisema, chombo cha kuchunguzia mwezi kilichosanifiwa nao kimepata maendeleo katika teknolojia muhimu za mifumo ya utoaji umeme, uongozaji wa usafiri na utumiaji wa data. Kwa mfano, chombo hicho kiliwekwa vifaa vya kisasa vya kupiga picha ambavyo ni kama macho ya binadamu, si kama tu vinaweza kukisaidia chombo hicho kuona vizuri hali ya kwenye sayari ya mwezi, bali pia vinaweza kupima umbali kati yake na vizuizi vilivyoko mbele. Nyuma ya chombo hicho kuna kifaa cha kuhifadhi joto ili kukiwezesha chombo hicho kizoee mazingira ya nyuzi 150 hadi 180 chini ya sifuri kwenye sayari ya mwezi. Aidha, kasi ya chombo hicho inaweza kufikia mita 200 kwa saa.

Mbali na idara za utafiti mjini Shanghai, hivi sasa idara zaidi ya 40 nchini China, zikiwemo chuo kikuu cha viwanda cha Harbin, chuo kikuu cha usafiri wa ndege na safari za anga ya juu cha Beijing, kundi la teknolojia za safari za anga ya juu la China, zote zinafanya utafiti kuhusu chombo cha kuchunguzia sayari ya mwezi. Hali hii imeonesha maendeleo ya kasi ya teknolojia za kuchunguza anga ya juu nchini China.

Wasikilizaji wapenda, mliyosikia ni sauti na nyimbo zilizotumwa duniani na saitelaiti ya kwanza ya China ya kuchunguza sayari ya mwezi Chang'e No.1 kwenye njia yake ya kuzunguka mwezi yenye umbali wa kilomita laki 3.8 kutoka kwenye dunia. Saitelaiti hiyo iliyorushwa mwezi Oktoba mwaka jana mpaka sasa imetuma data nyingi za uchunguzi wa mwezi duniani. Lakini saitelaiti hiyo ni hatua ya kwanza tu kwa mradi wa China wa kuchunguza sayari ya mwezi na kazi nzima za kuchunguza anga ya juu. China inalenga kutuma chombo cha uchunguzi kwenye mwezi na kufanya uchunguzi kwa kutembea kwenye sayari hiyo ifikapo mwaka 2012, na kurudisha sampuli za udongo wa mwezi mwaka 2020.

Kutokana na hali hiyo, chombo cha kuchunguza sayari ya mwezi kikiwa ni kifaa muhimu cha mradi wa kuchunguza mwezi, idara nyingi za utafiti zimeweka mkazo katika kazi zake za utafiti, taasisi ya utafiti wa magari ya kaskazini ya China ni mojawapo. Chombo cha kuchunguza mwezi kilichosanifiwa na taasisi hiyo kina umbo linalofanana na kile cha taasisi ya Shanghai, pia kina magurudumu sita. Lakini msanifu wake Bw. Su Bo alisema, chombo hicho kina uwezo mkubwa zaidi wa kutembea, siri yake ni usanifu maalum wa magurudumu yake.

Mtafiti wa taasisi hiyo Bw. Mao Ming alisema, walikusanya aina nyingi za udongo wa volkano ili kuiga mazingira ya ardhi ya mwezi. Majaribio yameonesha kuwa chombo kilichosanifiwa na taasisi hiyo kinaweza kuvuka kizuizi chenye urefu wa sentimita 60. Bw. Mao Ming alisema:

"sayari ya mwezi imefunikwa na udongo wa volkana, na una aina mbalimbali ambazo tulijaribu kuziiga. Tulikusanya udongo wa volkano kwenye sehemu za kaskazini mashariki mwa China, tulichanganya udongo tofauti na kuufanyia upimaji na utafiti, ili kutafuta aina gani ya gurudumu linaweza kutembea kwa ufanisi zaidi kwenye udongo kama huo."

Kutokana na kazi za utafiti huo wa taasisi mbalimbal nchini China, kwa uhakika baada ya muda mfupi vyombo mbalimbali vya kuchunguza sayari ya mwezi vitatolewa. Kiongozi mkuu wa mradi wa China wa kuchunguza mwezi Bw. Luan Enjie hivi karibu alidokeza kuwa chombo halisi kitakachotumika kwenye sayari ya mwezi baada ya miaka kadhaa kitakuwa na usanifu unaokusanya busara za taasisi mbalimbali.