Miaka 30 imepita tokea China ifungue mlango kiuchumi. Katika miaka hiyo, maingiliano ya kiutamaduni kati ya China na nchi za nje yamepelekea mabadiliko makubwa kutoka maingiliano ya kiraia hadi ya kiserikali na hivi sasa yameingia katika kipindi cha kufana.
Mliosikia ni opera ya Kibeijing iitwayo "Shajiabang", ambayo ni opera inayoeleza hadithi iliyotokea katika vita vya ukombozi. Opera hiyo ilioneshwa karibu kila siku katika miaka ya 60 ya karne iliyopita, kipindi ambacho maisha ya kiutamaduni yalikuwa duni sana. Katika kipindi hicho, familia ya kawaida ilikuwa haina televisheni, katika miji kulikuwa hakuna ukumbi wa Kara Ok na disco, opera kama ya "Shajiaban" ilikuwa inaoneshwa karibu kila siku.
Bwana Zhang Yu mwenye umri wa miaka 50 ameshuhudia maingiliano ya kiutamaduni kati ya China na nchi za nje yalivyobadilika kutoka machache hadi kuwa mengi. Hivi sasa bwana huyo amekuwa meneja mkuu wa Kundi la Maingiliano ya Utamaduni na Nchi za Nje. Mwaka 1982 baada ya kuhitimu masomo yake ya chuo kikuu Bw. Zhang Yu alikuwa mtumishi wa serikali katika Idara ya Maingiliano ya Kiutamaduni na Nchi za Nje katika Wizara ya Utamaduni ya China. Mwanzoni ujumbe alioupokea ulikuwa ni wa serikali kutoka Asia, Afrika na Latin Amerika tu. Mwaka 1990 Bw. Zhang Yu alijiuzulu na kuanza biashara ya utamaduni na maonesho ya michezo ya sanaa. Alisema,
"Baada ya miaka 30, hivi sasa maonesho ya michezo ya sanaa yamekuwa mengi, kila mwezi na hata kila wiki yanakuwapo maonesho ya kila aina katika miji mingi. Kwa mfano, katika Jumba la Taifa la Michezo ya Sanaa na majumba mengine mjini Beijing kila siku jioni huwa na maonesho kutoka nchini na nchi za Ulaya, Asia, Afrika, Latin Amerika na nchi za Kiarabu. Maonesho hayo yamestawisha maingiliano ya kiutamaduni kati ya China na nchi za nje. Mabadiliko makubwa yametokea katika maingiliano ya kiutamaduni kati ya China na nchi za nje katika miaka 30 iliyopita."
Bw. Zhang Yu alisema, hali ya sasa ambayo maonesho ni mengi na aina ni nyingi katika soko la michezo ya sanaa ilikuwa haitamaniki kabla ya miaka 30 iliyopita.
Mliosiki ni muziki uitwao "Nyota" uliotungwa na mwanamuziki mashuhuri wa Japani Bw. Shinji Tanimura. Mwanamuziki huyo aliwahi kushiriki "Tamasha la Usiku wa Asia" lililofanyika katika siku za Michezo ya Olimpiki ya Beijing.
Katika kipindi cha Michezo ya Olimpiki ya Beijing, idara husika zilishirikisha shughuli nyingi za utamaduni na zilivutia makundi ya wasanii zaidi ya 100 kutoka nchi 80 kujiunga na shughuli hizo. Baadhi ya vyombo vya habari vilisema China imekuwa nchi yenye biashara moto moto ya vitu vya sanaa na maonesho ya michezo ya sanaa. Wafanyabiashara wa nchi za nje walioko nchini China wamekuwa wakiongezeka siku hadi siku.
Bibi Lisa Cliff mwenye umri wa miaka 41, mwaka 1991 alikuja China kutoka Marekani, hapo mwanzo alikuwa ni mwandishi aliyejitegemea, baadaye aliwekeza biashara ya sanaa za uchoraji na ufinyanzi wa sanamu, alianzisha maduka mawili ya vitu vya sanaa, moja katika sehemu ya biashara SOHO na jingine katika sehemu ya sanaa ya Namba 798 mjini Beijing. Bibi Lasa Cliff ambaye hadi sasa amefanya baishara ya vitu vya sanaa kwa miaka mingi amejawa na uhakika na biashara yake. Alisema,
"Vitu vya sanaa vya China vinanivutia sana. Baada ya kuja China nimeshuhudia hali ya soko la vitu vya sanaa ilivyobadilika kuwa nzuri kila kukicha, mabadiliko hayo ikiwa pamoja na serikali ya China kuzidi kuruhusu sanaa za tamaduni tofauti kuingia nchini, hususan baada ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing kumalizika. Nina uhakika na ufanisi wa biashara yangu."
Sehemu ya sanaa ya Namba 798 yenye duka la vitu vya sanaa la Lisa Cliff hapo awali ilikuwa ni sehemu ya viwanda na mabohari, kuanzia mwaka 2002 wasanii wengi waliingia sehemu hiyo na kuanzisha maduka ya picha za kuchorwa, na kampuni za ubunifu na mabaa. Sehemu hiyo imekuwa sehemu kubwa ya sanaa inayojulikana nchini China na imewavutia wawekezaji wengi kutoka nchi za nje kama Bibi Lisa Cliff.
Ili kukidhi mahitaji ya wateja, mashirika ya utamaduni nchini China pia yanajitahidi kuingiza maonesho ya makundi ya sanaa ya nchi za nje. Bw. Xiao Le anao ukumbi wa muziki uitwao "Mao Live House", katika ukumbi huo karibu kila siku kuna maonesho ya muziki wa rock-and-roll kutoka nchi za nje, wapenzi wa muziki wa rock-and-roll wanapata furaha tele wanaposikiliza muziki huo. Bosi Xiao anaridhika na biashara yake. Alisema,
"Nimeanza biashara yangu mwaka 2000, katika miaka hiyo wasanii wengi walikuja kufanya maonesho yao katika ukumbi wangu, kati yao baadhi ni wasanii waliofanya maonesho ya mzunguko kutoka nchi moja hadi nyingine, na wengine ni wasanii mashuhuri duniani. Maonesho ya hapa yanawavutia sana vijana na biashara yangu ni nzuri."
Naibu mkurugenzi wa idara ya soko la utamaduni katika Wizara ya Utamaduni ya China Bw. Tuo Zuhai alisema, serikali ya China imetoa sera ya uwazi kwa utamaduni wa nje na kuwakaribisha wawekezaji wa nje washiriki kwenye ushindani katika sekta ya utamaduni, na serikali ya China itayatendea mashirika ya nje sawa na yake ya wenyeji. Alisema,
"Masoko ya utamaduni nchini China yamefunguliwa kwa kiwango kikubwa kwa nchi za nje. Kati ya masoko hayo, masoko ya maonesho ya michezo ya sanaa, masoko ya burudani na masoko ya VCD yote yamekuwa wazi kwa nchi za nje."
Kutokana na uchumi unavyoendelea, shughuli za utamaduni zinazoongozwa na serikali pia zimekuwa nyingi, China imekuwa na maingiliano mengi na nchi za nje, hali mbaya ya zamani ambayo maingiliano yalikuwa ni kwa nchi za Asia, Afrika na Latin Amerika tu mwanzoni mwa mageuzi, imebadilika kabisa.
Idhaa ya kiswahili 2008-10-23
|