Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-10-28 16:43:12    
Sanxingdui yenye vitu vingi vya ajabu

cri

Leo tunawaletea makala ya pili ya kipindi maalumu cha chemsha bongo kuhusu ufahamu wa vivutio vya mkoa wa Sichuan, makala hiyo inahusu "Sanxingdui yenye vitu vingi vya ajabu".

Kabla ya kusoma makala hiyo, tunatoa maswali mawili: 1. Sanxingdui ilistawi kwa miaka mingapi? 2. Miongoni mwa vitu vingi vilivyofukuliwa kwenye mabaki ya Sanxingdui, ni vitu vya aina gani, ambavyo vinaweza kuonesha kiwango cha ufundi wa wakati ule, je, ni vitu vya jade au ni vya shaba nyeusi? Tafadhali sikilizeni kwa makini makala tunayowasomea ili muweze kupata majibu

Zamani "Sanxingdui" ilipokuwa ikiitwa kuwa "Kijiji cha Sanxing", hakuna mtu aliyeweza kufikiria kwamba mkulima Bw. Yan wakati alipolima shambani kwake angeweza kugundua maajabu kwenye sehemu hiyo, ambayo ilikuwa mji mkuu wa nchi ya Shu kati ya miaka 5,000 na 3,000 iliyopita, ustaarabu wake uliendelea kwa muda wa miaka 2,000. Ugunduzi huo umekamilisha zaidi historia ya ustaarabu wa China, na kuonesha kuwa ustaarabu wa Mto Changjiang unaowakilishwa na ustaarabu wa Sanxingdui ni sawa kabisa na ustaarabu wa Mto Manjano, ambao ni chanzo cha ustaarabu wa China.

Kijiji cha Sanxing kiko kwenye mkoa wa Sichuan, kusini magharibi mwa China, na ni mwendo wa saa moja kwa magari kutoka Chengdu, mji mkuu wa mkoa huo. Jumba la makumbusho lilijengwa kwenye mabaki hayo ya kistoria kabla ya miaka zaidi ya 10 iliyopita, ambalo linaitwa "Sanxingdui".

Mwelezaji wa jumba la makumbusho la Sanxingdui, Bi. Qiu Xueqing alisema, kugunduliwa kwa mabaki hayo ya ustaarabu kwenye nyuzi 30 ya latitude kuna umuhimu mkubwa.

"Kwenye mstari wa latitude nyuzi 30 vilevile kuna kilele cha Mlima Zhumulangma, ustaarabu wa Maya na Bermuda Delta, ambazo zote zina mambo mengi ya ajabu. Sanxingdui ni mji wa kale na ni nchi ya kale yenye vitu vingi vya utamaduni iliyogunduliwa kwenye sehemu ya kusini magharibi mwa China."

Uchunguzi uliofanyika unaonesha kuwa, kabla ya miaka 3,000 iliyopita, mji huo mzima ulitelekezwa ghafla, ambapo ustaarabu uliofikia kiwango cha juu wakati ule ulisitishwa mara moja pia. Miaka michache iliyopita, kugunduliwa kwa mabaki ya Jinsha yaliyoko kwenye kiunga cha mji wa Chengdu, kunawafahamisha watu kuwa, vitu vya utamaduni vilivyogunduliwa kwenye sehemu hizo mbili ambazo zinakaribia kufanana kabisa. Hivyo, mabaki ya Jinsha, ambayo yalichelewa kwa miaka 500 hadi 1,000 kuliko mabaki ya Sanxing, yanachukuliwa na wasomi wengi kuwa ni endelezo la ustaarabu wa sehemu hiyo. Baadhi ya watu wanasema, mji mkuu wa Sanxingdui ulihamishwa kwenye sehemu yalipo mabaki ya Jinsha. Kuhusu chanzo halisi cha kutelekezwa kwa mji huo uliostawi kwa kiasi cha miaka 2,000, watu wanasema kwa namna mbalimbali, baadhi ya watu wanasema ilitokana na mafuriko ya maji, wengine wanasema ilitokana na vita, na watu wengine wanasema ilitokanana na maambukizi ya maradhi, lakini hadi hivi sasa bado haijagunduliwa kumbukumbu ya historia.

Vitu vilivyofukuliwa kwenye Sanxingdui ni vya ajabu sana. Bi. Qiu Xueqing alipojibu maswali yetu alisema, vitu vya Sanxingdui vinavyovutia watu zaidi ni vyombo vya shaba nyeusi, baadhi ya sanamu za shaba nyeusi zinashangaza watu, kwani sanamu hizi ni zenye macho makubwa na zenye pua zinazochongoka, jinsi ilivyo ni tofauti sana na za watu wa Asia. Bi. Qiu alieleza zaidi kuhusu kinyago kimoja cha shaba nyeusi ambacho ni alama ya Jumba la makumbusho, alisema:

"kinyago hicho ni cha kwanza kwa ukubwa wake duniani, pia ni chenye thamani kubwa nchini China. Inasemekana kuwa sura ya kinyago hiki inafanana sana na sura ya mfalme wa kwanza wa nchi ya Shu.

Kitu kingine kilichomvutia mtalii kutoka Ufaransa Bw. Humbert Droz kati ya vitu vingine vilivyooneshwa kwenye jumba la makumbusho ni Mti Tongtian, maana yake kwa Kichina ni mti mkubwa unaofikia mbinguni. Alisema:

Vitu hivyo viliwahi kuoneshwa nchini Ufanrasa miaka kadhaa iliyopita. Ingawa najua China ni nchi yenye histori ya miaka mingi, lakini nilipoona tena mabaki hayo ya kale bado nilishangaa sana.

Mti huo umebaki na kipande chenye urefu wa mita 3.6. Watu wa kale wa China waliona kuwa mti ni badiliko la ulimwengu, jua, mwezi na nyota ni matunda ya mti. Mwelezaji Bi. Qiu aliwafahamisha watazamaji, akisema,

"Si kazi rahisi kutengeneza mti huo wa shaba nyeusi, mti huo wenye mtindo maalumu sana haupatikani sehemu yoyote nyingine duniani, kazi ya kusubu pia ilikuwa yenye ufundi mkubwa sana.

Mbali na kiwango cha juu cha ufundi wa utengenezaji wake katika wakati ule, miti ya shaba nyeusi inaonesha ufahamu wa watu wa kale wa China kuhusu mbingu na ulimwengu. Kuhusu suala hilo, tulimwuliza mshauri wa Jumba la makumbusho, Bw. Ao Tianzhao, mtafiti huyu mwenye umri wa zaidi ya miaka 70, amefanya utafiti kuhusu utamaduni wa Sanxiangdui kwa zaidi ya nusu karne. Alisema:

"Umaalumu unaoonekana katika vyombo vya shaba nyeusi vilivyofukuliwa kwenye Sanxingdui ni kuungana kabisa kwa nguvu za mungu na madaraka ya mfalme. Vilevile huko kulikuwa ni kituo cha kuhiji, nchi ya Shu ya kale iliandaa shughuli za kutambika ili kuwavutia watu wa makabila wenye dini mbalimbali waende kuhiji huko."

Vyombo vya shaba nyeusi vilivyofukuliwa huko Sanxingdui vinaonesha vilivyo kiwango cha ufundi wa kazi wa miaka ile ya zamani. Vitu vingine vilivyofukuliwa huko Sanxingdui ambavyo vinawashangaza watu ni pembe za ndovu na simbi nyingi za baharini. Kwa hali ilivyo ya kijiografia ya hivi sasa ya mkoa wa Sichuan, huko panakosekana mazingira ya kuishi ndovu, kwa sababu uko mbali sana na bahari. Mwelezaji Bi. Qiu alisema,

"Kulikuwa na msomi aliyesema, pembe za ndovu zililetwa kwenye 'njia ya hariri ya kusini'. Vitu vya aina nyingine muhimu vilivyoletwa huko katika njia hiyo ni simbi wa baharini, ambao idadi ya simbi zilifukuliwa kwenye Sanxingdui ni karibu 5,000. Simbi, ambao wanaishi baharini, hawawezi kupatikana katika Chendu, mji wa sehemu ya ndani ya bara la China. Hii inaonesha kuwa njia ya biashara ya nchi ya Shu ya kale ilikuwa ndefu sana, ambayo ilifikia Asia ya magharibi na Asia ya kusini."

Utamaduni wa Sanxingdui unawaonesha watu vitu vingi vya ajabu, hivyo Jumba la makumbusho ya Sanxingdui limetembelewa na idadi kubwa ya watazamaji tangu ilipofunguliwa zaidi ya miaka 10 iliyopita. Mabaki ya utamaduni wa Sanxingdui yameoneshwa kwenye mabara manne ya dunia isipokuwa bara la Afrika. Naibu mkuu wa jumba la makumbusho la Sanxingdui, Bw. Zhangjizhong alisema, vitu vizuri vya ajabu vya mabaki pamoja na ustaarabu wa kale wa Sanxingdui ni kivutio kikubwa kwa watalii wa nchi za nje.