Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-11-03 16:59:25    
Mkoa wa Ningxia wahimiza utoaji mafunzo ya ufundi wa kazi

cri

Mkoa unaojiendesha wa kabila la Wahui wa Ningxia una watu wengi, lakini mashamba ya mkoa huo ni machache. Ili kuhamisha ziada ya nguvukazi vijijini, serikali ya huko inafuata hali halisi, na kuwahimiza watu hao kwenda nje ya mkoa huo kufanya kazi. Ili kuinua sifa ya watu hao, mkoa wa Ningxia unaimarisha kuhimiza utoaji mafunzo ya ufundi wa kazi.

Kuanzia mwaka 2005, mkoa wa Ningxia ulianza kutekeleza "mradi wa utoaji mafunzo kwa wakulima milioni moja", ambao umewaandaa wakulima wengi wenye ujuzi na kufahamu ufundi wa kazi. Mkurugenzi wa ofisi ya usimamizi wa kazi ya idara ya uhakikisho wa kazi ya mkoa unaojiendesha wa Ningxia Bw. Chen Xiaojun alisema, lengo la mkoa wa Ningxia kuimarisha utoaji mafunzo ya ufundi wa kazi kwa wakulima ni kuwataka watu hao waweze kuchuma fedha kwa kutegemea ufundi wao wa kazi, sio tu kutegemea nguvu zao. Alisema,

"Mwaka 2006 wastani wa mapato ya wakulima vibarua wa Ningxia ulichukua asilimia 60 tu ya ule wa mapato ya wakulima vibarua nchini China, hii inaonesha kuwa ingawa wakulima vibarua wa Ningxia ni wengi, lakini kwa jumla wanakosa ufundi wa kazi, hivyo wanafanya kazi za kutegemea nguvu zao tu, na kupelekea kupata mapato machache. Hivyo tunaimarisha utoaji mafunzo kwao, na kila mwaka mkoa wa Ningxia unatenga Yuan za RMB milioni 30 kwa ajili ya kutoa mafunzo ya ufundi wa kazi kwa wakulima vibarua, ili kuinua sifa zao."

Katika darasa moja la kituo cha utoaji mafunzo ya ufundi wa kazi kijijini Tonggui wilayani Xingqing mjini Yinchuan, mwandishi wetu wa habari alimwona mwalimu aliyekuwa anaeleza matumizi ya word, na wakulima waliokaa mbele ya kompyuta walisikiliza kwa makini, walisikiliza huku wakifanya mazoezi. Pia kuna wanawake wengi wanaokwenda pamoja na watoto wao.

Mkazi wa kijiji hicho Bibi Duan Xueqing ana umri wa miaka 34. Ana watoto wawili. Ingawa ana kazi nyingi za nyumbani, lakini anakwenda kujifunza kompyuta. Alimwambia mwandishi wetu wa habari akisema:

"Kama una ujuzi utautumia siku moja. Kati ya wakulima, wanawake wengi wana nafasi, nadhani baada ya mimi kupata elimu, watoto wangu wanaweza kujifunza kutoka kwangu."

Imefahamika kuwa, katika kituo cha utoaji mafunzo licha ya kufundisha elimu ya matumizi ya kompyuta, pia kinafundisha ufundi ukiwemo kazi ya kushughulikia tanuri, ujenzi, eletroniki, ngozi za kutengeneza viatu na ufumaji, hivyo kinapendwa na kuungwa mkono na watu wengi.

Mkuu wa idara ya ajira ya wilaya ya Xingqing Bw. Jiang Hongtao alisema, katika miaka mitatu iliyopita, wilaya ya Xingqing ilitoa mafunzo kwa nguvukazi za ziada za vijijini 30,000, ambapo asilimia 85 ya watu hao walihitimu, na asilimia 82 ya watu walipata ajira. Bw. Jiang alisema,

"Wakulima wetu wengi wanapenda kuhudhuria semina za mafunzo. Zamani hakukuwa na semina za mafunzo, na wakulima hawakuwa na hati ya mafunzo ya ufundi, hivyo mishahara yao ilikuwa midogo. Lakini baada ya kupewa mafunzo, wamekuwa na ufundi wa kazi, hivyo mapato yao yanaongezeka, na wakulima wanapata manufaa halisi."

Mkazi wa kijiji cha Tonggui wilayani Xingqing Bw. Duan Hongfu ana umri wa miaka 40, katika majira ya baridi alikuwa anakwenda kushughulikia kazi ya tanuri ili kuongeza mapato yake. Lakini kwa kuwa yeye si fundi maalum, hivyo kila mwezi alipata mshahara wa Yuan za RMB 200 au 300 hivi. Mwezi Marchi mwaka jana, alihudhuria semina ya mafunzo ya ufundi wa kazi ya tanuri, na alipata hati ya msingi. Katika majira ya baridi ya mwaka jana, mshahara wake uliongezeka kwa mara nne.

Mafunzo ya ufundi wa kazi sio tu yanawasaidia wakulima vibarua waweze kufanya kazi kwa "kutegemea ufundi wao", bali pia yanafumbua macho yao, na kubadili mawazo yao, ambayo yanawafanya watambue umuhimu wa elimu na ufundi wa kazi. Imefahamika kuwa, asilimia 40 ya wakulima vibarua waliohudhuria semina za ufundi walirudi darasani tena kwa mara nyingi, ili ufundi wao uinuke zaidi. Bibi Ma Yahong kutoka kijiji cha Qiying wilayani Haiyuan mjini Guyuan ni mmoja yao.

Bibi Ma Yahong ana umri wa miaka 20, mwaka jana aliwahi kuhudhuria semina ya mafunzo ya kompyuta kwa nusu mwaka, baadaye alikwenda kufanya kazi mjini Suzhou, na kila mwezi mshahara wake ulikuwa Yuan za RMB 1,400. Lakini hakuridhika na kazi hiyo, hivyo alirudi tena kwenye kituo cha utoaji mafunzo ya kompyuta ya Qingsong mjini Yinchuan. Alisema:

"Kazi niliyoifanya mjini Suzhou ilikuwa nzuri, lakini kwa ujumla, naona sitaweza kujifunza mambo mengi kutokana na kazi hiyo, hivyo nilichuma pesa na kurudi kituoni hapo kuendelea na masomo. Baada ya kuwa na ufundi wa kazi, nitaweza kufanya kazi za aina nyingi zaidi, hivyo ni muhimu kuwa na hati ya mafunzo ya ufundi wa kazi. Aidha, nikiwa na hati ninaweza kuanzisha shughuli mimi mwenyewe."

Mkurugenzi wa ofisi ya usimamizi wa kazi ya idara ya uhakikisho wa kazi ya mkoa unaojiendesha wa Ningxia Bw. Chen Xiaojun alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, hivi sasa mkoani Ningxia wakulima wenye ufundi wanaongezeka kwa asilimia 16 kila mwaka. Kwa kupitia kukusanya habari, mwandishi wetu wa habari aliona kuwa, mafunzo ya ufundi wa kazi yanaongeza sifa ya wakulima vibarua.