Kijiji cha Sangmo kilichoko umbali wa kilomita zaidi ya kumi kutoka magharibi mwa Lahsa, mji mkuu wa Tibet ni kijiji kinachofanya shughuli za utalii zinazowavutia watalii kwa mila na desturi za jadi. Leo tunawaletea maelezo juu ya maisha mapya ya wakazi wa kijiji hicho.
Bibi Yangzom mwenye umri wa miaka 87 ni mkazi wa kijiji hicho. Alisema kijiji cha Sangmo ni maarufu kwa nyimbo na ngoma kwenye mkoa unaojiendesha wa Tibet, na mwaka 2002, serikali ya Lhasa iliamua kukifanya kijiji hicho kuwa ni kijiji cha kitalii. Bibi Yangzom alisema reli ya Qinghai-Tibet imezinduliwa, na hivi sasa hali ya hewa mkoani Tibet ni nzuri, hivyo watu watakaotalii kwenye mkoa wa Tibet na kijiji cha Sangmo watakuwa wengi sana. Bibi Yangzom ni kiongozi wa utalii na mwimbaji mwenye umri mkubwa zaidi kwenye kijiji cha Sangmo, hivyo watalii wote wanaotembelea kijiji hicho wanataka kusikiliza nyimbo alizoimba.
Wapendwa wasikilizaji, mnaosikia ni wimbo maarufu wa kabila la Watibet uitwao "Zhuoma Lakang" unaoimbwa na bibi Yangzom. Aliimba hivi, milima ya nyumbani kwetu ni mizuri zaidi, maji ya nyumbani kwetu ni safi zaidi, na watu wa nyumbani kwetu ni wema zaidi. Bibi Yangzom aliimba wimbo huo kabla ya Tibet haijapata ukombozi mpaka sasa, lakini ana hisia tofauti anapoimba wimbo huo kwenye wakati tofauti. Bibi Yangzom alisema,
"Kabla ya Tibet kupata ukombozi, tulitozwa kodi kubwa. Niliendesha maisha yangu kwa kuwaimbia watu nyimbo, nilikuwa maskini sana hata sikukuwa na uwezo wa kujinunulia viatu. Baada ya Tibet kukombolewa, nilikuwa na maisha ya kawaida, na niliimba kwa ajili ya kujiburudisha. Sasa hali imebadilika, maisha yangu yameboreshwa sana, ninafurahi kuwaimbia watalii kutoka sehemu mbali."
Maana ya neno la Sangmo kwenye lugha ya kitibet ni Ardhi yenye Rutuba. Kabla ya kuwa kijiji cha kitalii, kijiji cha Sangmo hakikuwa na ardhi yenye rutuba tu, bali pia kina raslimali kubwa ya utamaduni maalumu zikiwemo nyimbo, ngoma na opera za kabila la Watibet. Lakini kwa muda mrefu, wakazi wa kijiji hicho hawakutambua kuwa raslimali hiyo ya utamaduni inaweza kuboresha maisha yao. Mkurugenzi wa baraza la kijiji cha Sangmo Bw. Tubdain alisema,
"Kwenye kijiji chetu, kuna nyimbo mbalimbali zinazolingana na kazi tofauti, kama vile nyimbo za ujenzi, kilimo mashamba na ufugaji wanyama. Lakini katika miaka kumi kadhaa iliyopita, sisi sote tuliendesha maisha kwa kutegemea kilimo tu, hakukuwa na mtu yeyote aliyetambua kuwa kuimba nyimbo na kucheza ngoma kunaweza kutuletea mapato."
Kutokana na mkoa wa Tibet kufunguka siku hadi siku, wakazi wa kijiji cha Sangmo walianza kuendeleza kilimo cha kitongoji, na hadi kufikia mwaka 2002, mapato ya wanakijiji hao kwa wastani yalikuwa yuan 2,500, wakati huo huo mapato ya wastani ya wakulima na wafugaji mkoani Tibet yalikuwa yuan 2,070. Kampuni moja ya utalii ya mji wa Lhasa ilivutiwa na kijiji hicho, na meneja wa kampuni hiyo alimwendea Bw. Badro ambaye alikuwa mkuu wa kijiji cha Sangmo. Bw. Badro alisema,
"Mwaka 2002, meneja moja wa kampuni ya utalii aitwaye Jian alikuja kijiji chetu, na kutaka kushirikiana nasi kuanzisha kampuni ya utalii wa mila na desturi za jadi kwenye kijiji chetu. Baada ya kujadiliana tuliona kuwa hili ni jambo nzuri, na litatuletea manufaa, hivyo tulikubali."
Bw. Badro alisema wakati huo kwa wanakijiji wengi kampuni ya utalii ni kitu kigeni, hivyo kulikuwa na vijana 30 tu walijiandikisha kushiriki kwenye kampuni hiyo. Baada ya kuzinduliwa, kampuni hiyo iliwapokea watalii zaidi ya 2,600 mwaka 2002. Baadaye idadi ya watalii kwenye kijiji hicho inaongezeka mwaka hadi mwaka, na hadi kufikia mwaka 2007, kampuni hiyo iliwapokea watalii zaidi ya elfu 30 kwa mwaka, ambapo mapato ya wanakijiji kwa mwezi yaliongezeka kutoka mia tatu kuwa mia nane.
Wanakijiji walioshiriki kwenye shughuli za utalii kijijini hawatakiwi kuondoka nyumbani, wanafanya shughuli za utalii huku wakifanya kazi ya kilimo, hivyo familia 70 za kijiji cha Sangmo zote zilishiriki kwenye shughuli za utalii, kati yao wengine wanatoa mahali pa kufanyia shughuli, wengine wanaanzisha hoteli ndogo, na wengine wanawaburudisha watalii kwa nyimbo na ngoma za kabila la Watibet. Bw. Li ni mtalii kutoka mkoa wa Gansu, alisema,
"Hii ni mara yangu ya kwanza kutembelea Tibet. Zamani niliona kuwa Tibet ni mkoa maskini ulio na unabaki nyumba kimaendeleo, lakini hali halisi si kama nilivyodhani. Watibet ni hodari katika kuimba na kucheza ngoma, wanaishi maisha yenye furaha, na sasa tumejua Tibet kweli."
Bw. Tenzin Kunga mwenye umri wa miaka 70 ni mkazi wa kijiji cha Sangmo, alisema baada ya kushiriki kwenye shughuli za utalii, wanakijiji wamebadilisha tabia zao na wamekuwa na sura mpya, alisema,
"Kwa mfano baada ya kuanza kupokea watalii, kijiji chetu na nyumba za wanakijiji zimekuwa safi sana. Aidha wanakijiji wanefunguka wanapowasiliana na wageni."
Bw. Tenzin Kunga amesema ukweli. Miaka kadhaa iliyopita, watoto wa kijiji cha Sangmo waliogopa wageni, lakini sasa wamekuwa viongozi wadogo wa utalii. Bw. Tenzin Kunga pia ameboresha maisha yake kwa kupitia shughuli za utalii.
Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2007, wakulima na wafugaji walioshiriki kwenye shughuli za utalii mkoani Tibet walifikia zaidi ya elfu 30, mapato ya jumla ya utalii vijijini yalikuwa yuan milioni 220, mapato ya wastani ya wakulima na wafugaji hao yalizidi yuan 6,300, na yalikuwa zaidi ya mara mbili kuliko mapato ya wastani ya wakulima na wafugaji mkoani Tibet.
|