Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-11-17 17:05:42    
Bibi Wang Fang na "familia ya angels"

cri

Mama huyo anaitwa Wang Fang. Yeye ni mama wa mtoto mwenye ugonjwa wa mtindio wa ubongo mjini Nanning katika mkoa unaojiendesha wa kabila la Wazhuang wa Guangxi, China. Katika miaka mingi iliyopita, alitumia fedha zake zote kuanzisha kituo cha kuwasaidia watoto wenye ugonjwa wa mtindio wa ubongo, yaani "familia ya angels", na kuzisaidia familia maskini zenye matatizo ya kiuchumi kutibu watoto wenye ugonjwa huo. Kwa hiyo alisifiwa na Umoja wa Mataifa, na kupata "tuzo ya utoaji mchango mkubwa kwa kuwahudumia walemavu".

Mwaka 1992, Bibi Wang Fang alizaa watoto pacha wapendwa Baobao na Beibei. Lakini bado hakuonja furaha ya kuwa mama, Baobao alithibitishwa kuwa mtoto mwenye ugonjwa wa mtindio wa ubongo, ambao ulimfanya Bibi Wang Fang akate tamaa.

"Siwezi kuelezea hisia zangu wakati huo, sikujua namna ya kuikabili hali hiyo."

Kuanzia siku mtoto wake alipothibitishwa kuwa na ugonjwa huo, Bibi Wang Fang alimpelekea mtoto wake kuonana na madaktari. Hadi hivi sasa bado haijawezekana kutibiwa ugonjwa huo, ila kuboresha kwa njia ya mazoezi maalum. Baobao alipokuwa na umri wa miaka 7, bibi Wang Fang alianza kutafuta shule inayoweza kumpokea binti yake na kumfanya aweze kukua kama walivyo watoto wengine wa kawaida, lakini alishindwa.

Ili kumtibu Baobao, bibi Wang Fang alijuana na wazazi wa watoto wenye ugonjwa wa mtindio wa ubongo duniani na maofisa wengi wa mashirika ya kuwasaidia wenye shida. Wakati alipowasiliana nao, bibi Wang Fang aliona kuwa, kutokana na sababu mbalimbali, watoto wengi wenye ugonjwa wa mtindio wa ubongo hawakupata huduma za kupunguza ugonjwa na mazoezi kwa wakati, hivyo walikosa fursa nyingi za matibabu na ufufuzi. Ili kubadili hali hiyo, bibi Wang Fang alikuwa na wazo moja, yaani kuanzisha kituo kinachoweza kutoa huduma za kuwasaidia kufufua uwezo wa Baobao na watoto wengine wenye ugonjwa wa mtindio wa ubongo. Mwaka 2002 wakati siku ya watoto duniani ya tarehe 1 Juni ilipowadia, kituo hicho kilianzishwa, bibi Wang Fang alikiita "familia ya angels". Alisema,

"Nataka kuwafanya watu wengi zaidi wajue kuwa watoto wenye ugonjwa pia ni malaika, na nina matumaini kuwa 'familia ya angels' ni mahali ambapo malaika hao huruka, pia nina matumaini kuwa watu wengi zaidi watakuja kuwafuatilia watoto hao kama malaika."

"Familia ya angels" kwa urefu ni kituo cha utoaji huduma za kuwasaidia watoto wenye ugonjwa wa mtindio wa ubongo kufufua uwezo wao kilichopo mjini Nanning. Wakati kituo hicho kinaanzishwa kulikuwa na wafanyakazi watatu, na watoto watano wenye ugonjwa huo. Lakini baada ya kujulikana kwa kituo hicho, familia zinazotaka kuwapelekea watoto wenye ugonjwa wa mtindio wa ubongo zimekuwa nyingi siku hadi siku, na bibi Wang Fang pia alifanya kwa awezavyo kupunguza gharama ili kupunguza mzigo mzito wa kiuchumi wa wazazi hao, na kuwafanya watoto wengi zaidi wa familia zenye matatizo ya kiuchumi waweze kupata fursa ya kupewa huduma. Lakini baada ya muda mfupi, mapato ya "familia ya angels" hayakuweza kulingana na malipo. Bibi Wang Fang alisema,

"Mwaka 2005 tulipata matatizo makubwa ya kiuchumi, tulikopa pesa kutoka kwa marafiki wote."

Ili "familia ya angels" inaweza kupata maendeleo, Bibi Wang Fang aliacha kazi yake, lakini hakujuta, bali anaona fahari kwa kuweza kubeba jukumu la jamii. Bibi Wang Fang alisema,

"Kila siku ninawasiliana na watoto hao, naona faraja ninaposikiliza maneno machache waliyosema. Baada ya miaka kadhaa baadhi ya wazazi wa watoto hao wamejiamini na kuwa na furaha kubwa, vilevile wana matumaini kwa siku za usoni. Nina imani kubwa zaidi kwa siku za usoni."

Baada ya "familia ya angels" kuanzishwa, Bibi Wang Fang kwa mara ya kwanza alianzisha mbinu ya uelimishaji ya kuwapa wanafunzi mwangaza na kuwahamasisha wajipenyeze zaidi katika elimu mkoani Guangxi, ambayo imepata mafanikio.

Miaka miwili iliyopita, msichana Xianxian mwenye umri wa miaka 5 alikuja "familia ya angels" kupata mafunzo ya kupunguza ugonjwa wake. Mama wa Xianxian alisema,

"Zamani hata hakuweza kuinamisha kichwa chake, sasa baada ya kutibiwa kwa zaidi ya miaka miwili, kichwa chake kinaweza kuinama kidogo. Anafurahi kuja hapa, na anapofurahi anatamka kidogo, naona kituo hicho kweli ni kizuri."

Katika miaka 6 iliyopita, "familia ya angels" imetoa huduma mbalimbali kwa watoto zaidi ya 80 wenye ugonjwa wa mtindio wa ubongo na familia zaidi ya 500 nchini China, vilevile ilitoa mafunzo kwa watoto wa nchi za nje. Hivi sasa, watoto wengi wameingia shuleni baada ya kupewa mafunzo.

"Familia ya angels" baada ya kuanzishwa, imefuatiliwa na sehemu mbalimbali duniani. Shirika la afya duniani WHO, World Vision na idara nyinginezo zilitoa misaada mbalimbali kwa "familia ya angels". Sekta mbalimbali za jamii pia zinatoa misaada kwa "familia ya angels". Hivi sasa, kila Yuan 100 zinazotumiwa na "familia ya angels", Yuan 52 zinachangiwa na jamii.

Imefahamika kuwa, kiwango cha kutokea kwa wagonjwa wa mtindio wa ubongo ni mbili hadi tano katika elfu, hivi sasa mkoani Guangxi, watoto 60,000 hivi wenye umri wa miaka 0 hadi 14 wanapata ugonjwa huo. Kuanzia mwaka 2006, Bibi Wang Fang alianza kutembelea familia za watoto wenye ugonjwa huo vijijini mkoani Guangxi. Bibi Wang Fang alisema, matumaini yake makubwa ni kujenga shule kubwa inayotoa huduma za kuwasaidia watoto hao kufufua uwezo wao, kutoa elimu na mafunzo ya ufundi wa kazi. Bibi Wang Fang alisema,

"Nina matumaini kuwa watoto hao wanaweza kujifunza ufundi, na kushiriki kwenye jamii. Nina matumaini kuwa 'familia ya angels' zitakuwa nyingi katika siku za usoni."