Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-11-14 16:15:32    
Tamasha la kimataifa la michezo ya sanaa lafanyika mjini Shanghai

cri

Tamasha la 10 la kimataifa la michezo ya sanaa linafanyika katika mji wa Shanghai, mji mkubwa uliopo mashariki mwa China. Wasanii kutoka Australia, Canada, Japani, Marekani, Ujerumani, Misri na nchi nyingine wamekusanyika huko kwa furaha. Katika muda wa mwezi mmoja wasanii hao watafanya maonesho zaidi ya 52 ya michezo ya sanaa.

Tamasha hilo limeanza tarehe 18 mwezi uliopita, mliosikia hivi punde ni sehemu ya muziki wa opera ya ngoma ya China "Kibanda cha Peony". Hii ni opera iliyohaririwa kwa mujibu wa hadithi ya kale nchini China. Baada ya kuhaririwa na wataalamu hadithi hiyo yenye historia ya miaka 400 inavutia sana.

Tamasha la kimataifa la michezo ya sanaa la Shanghai licha ya kuwa linaonesha michezo ya sanaa ya jadi ya China na pia limekuwa na umaarufu mkubwa katika nchi za nje. Naibu mkurugenzi wa maandalizi ya tamasha hilo ambaye pia ni naibu waziri wa utamaduni wa China Bi. Zhao Shaohua alieleza,

"Tamasha la kimataifa la michezo ya sanaa la Shanghai limefanyika kwa miaka tisa na kupata mafanikio, na limekuwa Tamasha kubwa la wasanii wa China na wa nchi za nje, ambapo wasanii wamepata fursa ya kuonesha michezo yao mipya, Tamasha hilo ni kama daraja la maingiliano ya kiutamaduni kati ya China na nchi za nje."

Kutokana na tamasha hilo linavyozidi kujulikana, makundi mengi makubwa na maarufu ya michezo ya sanaa duniani yanashiriki kwenye tamasha hilo.

Mliosikia ni muziki wa dansi ya "Karamu ya Usiku" iliyochezwa na wasanii wa Hungary. Hii ni dansi inayokaribishwa sana popote inapochezwa duniani. Uhodari na uchangamfu mkubwa wa wasanii katika maonesho yao unawafurahisha sana watazamaji.

Mwanafunzi mmoja wa chuo kikuu aliyetazama dansi hiyo alisema,

"Hamu yangu imetosheka sana leo! Hapo kabla sikupata fursa ya kutazama dansi ya Hungary, leo nimetia macho nuru. Nitatazama michezo mingi ya tamasha hilo."

Licha ya dansi ya Hungary, opera ya dansi iliyochezwa na wasanii wa Zurich ya "Ndoto katika Usiku wa Majira ya Joto", nyimbo alizoimba mwimbaji maarufu wa Japan Bi. Ayumi Hamasaki, na michezo ya sarakasi iliyooneshwa na wasanii wa China na wa nchi za nje, dansi ya ballet na maonesho ya mavazi, yote hayo yamechangia uhondo wa tamasha hilo.

Katika kipindi cha tamasha hilo shughuli nyingine za umma pia zinafanyika mjini humo. Shughuli hizo zinagawanyika katika aina tatu. Moja ni maingiliano ya kiutamaduni kati ya miji na sehemu. Nyingine ni shughuli za kuonesha utamaduni wa mjini Shanghai ikiwa ni pamoja na maonesho ya utamaduni wa kimaisha na vitu vya sanaa za mikono vya wakazi wa Shanghai. Zaidi ya hayo, wakazi wa mji wa Shanghai wanafanya maonesho ya michezo ya sanaa katika mitaa mbalimbali mjini humo.

Bibi Chen aliyeshiriki kwenye maonesho ya dansi alisema,

"Kadiri tunavyozidi kucheza siku baada ya siku ndivyo tunavyozidi kujiamini, tuna furaha kwa kucheza na tunazidi kujihisi kama tumekuwa vijana."

Moja ya shughuli muhimu katika tamasha hilo ni biashara ya kimataifa ya maonesho ya michezo ya sanaa, shughuli hiyo imewavutia wasanii na wajumbe wa makundi ya wasanii zaidi ya 400 na katika muda wa siku kadhaa tu nchi zaidi ya 30 zimesaini makubaliano ya kuonesha michezo yao nchini China.

Bw. Mike Spear ni msimamizi mkuu wa Kampuni ya Kurekodi CD ya Tuffgong iliyopo Jamaica alisema,

"Tulikwenda mara nyingi nchini Japani kwa ajili ya kutafuta soko barani Asia. Tamasha hili la Shanghai linafanyika vizuri sana. Niliwahi kushiriki matamasha ya Mexico na Marekani, naona tamasha la Shanghai ni tofauti na matamasha hayo, lakini tamasha hili linafanikiwa kwa namna yake. Tunatafuta ushirikiano hapa China kwa sababu soko la China linakuwa wazi zaidi kwa bendi za Amerika ya Kusini."